Jumatatu, 18 Desemba 2023

WATUMISHI IJC MWANZA WAJUMUIKA KULA KALAMU

Na. Stephen Kapiga-Mahakama, Mwanza.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Mwanza Mhe. Dkt. Ntemi Kilekamajenga amejumuika na Watumishi wa Mahakama ya Tanzania wa Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki jijini Mwanza, na kufanya sherehe ya kupongezana kwa kazi walizotimiza kwa mwaka 2023 kwa kula pamoja ng’ombe mmoja aliyetolewa kama zawadi kwa watumishi hao.

Ahadi ya kujumuika pamoja na kula kalamu hiyo ilitolewa na Mhe. Dkt. Kilekamajenga kwa kuahidi kutoa ng’ombe mmoja kama watafikia malengo waliojiwekea kama Kanda ya Mwanza walipokuwa kwenye kikao kazi cha kila mwanzo wa wiki mwanzoni mwa mwezi Aprili, 2023 kwa watumishi wote wanaofanya kazi ndani ya jengo la Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki jijini Mwanza.

“Naahidi kuwa endapo kasi ya usikilizaji wa mashauri itaongezeka hasa kwa ngazi ya Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Mwanza ikifanikiwa kushusha idadi ya mashauri na kuufikia 600 basi nitatoa ng’ombe mmoja kama zawadi kwa watumishi wote ili tujumike kwa kalamu ya mafanikio hayo”, alisema Mhe. Dkt. Kilekamajenga.

Akisoma taarifa ya matokeo ya utendaji kazi huo, Kaimu Naibu Msajili Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Mwanza Mhe. Protas Kubaja alisema kuwa, wakati wa kuweka malengo hayo kituo cha Mahakama kuu ya Tanzania Kanda ya Mwanza kwa mwezi huo Aprili kilikuwa na jumala ya mashauri takribani 1200 na mpaka kufikia mwanzoni mwa mwezi Novemba,2023 yalikuwa mashauri 600 tu ndiyo yalikuwa yanaendelea Mahakamani.

“Mhe Jaji Mfawidhi napenda kutoa taarifa hii kuwa, watumishi kwa pamoja wamefanikiwa kufikia lengo lililowekwa kwa kuweza kushusha idadi ya mashauri mpaka kufikia mashauri 600 mwanzoni mwa mwezi Novemba 2023 ambayo ndio yalikuwa yakisomeka kama mashauri yaliyobakia “Pending cases” katika mfumo wa awali wa JSDS2.” alisema Mhe Protas Kubaja.

Aidha, Mhe. Dkt. Kilekamajenga aliwapongeza watumishi wote kwa ushirikiano waliouonesha na hivyo kuweza kufikia lengo walilojiwekea la kuondosha idadi ya mashauri kwa kasi nzuri ya usikilizaji wa mashauri hayo na hatimaye kufikia mashauri chini ya 600 kwa mwezi Novemba 2023.

“Kwa kweli nimeamini kuwa Mwanza mkiamua jambo lenu huwa hamkwami. Nawapongeza wote tulioweza kushirikiana na kufanikisha kumaliza mashauri hayo. Japo kwa sasa katika mfumo huu mpya wa kuratibu na kusimamia mashauri ‘e –CMS’ bado kuna changamoto ndogondogo naamini mpaka kufikia mwezi Februari 2024 zitakuwa zimepatiwa ufumbuzi na hivyo kutuwezesha kuweza kujua mashauri yetu kama kituo yapo katika hali gani”, alisema Mhe.Dkt. Kilekamajenga.

Kwa upande wao watumishi wa Mahakama ya Tanzania wanaofanya kazi katika Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki Mwanza waliupongeza Uongozi wa Mahakama Kuu Mwanza kwa kuandaa sherehe hiyo ambayo ilifana sana na hivyo kuwapa morali ya kufanya mengi zaidi kwa mwaka ujao wa 2024 na kuweza kuendeleza utamaduni wa kukutana pamoja.

“Jambo hili ni zuri na ninaupongeza uongozi kwa kuweza kuliona na kulianzisha katika kituo chetu. Nimekuwepo Mahakamani kama mtumishi kwa miaka 15 sasa lakini hakukuwahi kuwa na tukio kama hili. Zaidi ya kuwa na usiku wa siku ya sheria nchini “law day night” kama kiashiria cha  ufunguzi wa mwaka wa Mahakama basi na hii ya kwetu imekuwa kama zawadi kwa kufunga mwaka wa Mahakama kila ifikapo Desemba 15”, alisema Bi. Sekela Mwijibe.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Mwanza Mhe. Dkt. Ntemi Kilekamajenga akitoa neno wakati wa hafla hiyo ya kula kalamu kwa watumishi (hawapo pichani) wa Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki jijini Mwanza.

Sehemu ya watumishi wa Mahakama ya Tanzania wa Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki jijini Mwanza walioshiriki kalamu hiyo.

Sehemu ya watumishi wa Mahakama ya Tanzania wa Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki jijini Mwanza walioshiriki kalamu hiyo wakiongea na Mtendaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Mwanza, Bw. Tutubi Mangazine (aliyesimama katikati)

Sehemu ya watumishi wa Mahakama ya Tanzania wa Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki jijini Mwanza walioshiriki kalamu hiyo wakiteta jambo na Mtendaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Mwanza Bw. Tutubi Mangazine.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Mwanza Mhe. Dkt. Ntemi Kilekamajenga (katikati) akiiongoza meza kuu wakati wa hafla ya kula kalamu na watumishi wa mahakama kuu mwanza.

(Habari Hii Imehaririwa na Innocent Kansha - Mahakama)

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni