Na. Innocent Kansha - Mahakama
Msajili
wa Mahakama ya Rufani na Kaimu Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe.
Sylvester Kainda amewataka Manaibu Wasajili na Mahakimu wakazi Wafawidhi
kuzingatia maagizo yaliyotolewa na Jaji Mkuu na Jaji Kiongozi siku ya kuapishwa
na kufungua mafunzo elekezi hayo kwani hotuba hizo mbili ndiyo ufunguo wa
majukumu yao mapya na kuwataka kuzisoma na kuzielewa ili kuwarahisisha
kutekeleza wa majukumu yao mapya ya kiuongozi wanayokwenda kuyatimiza, ikiwa
pamoja na utoaji haki kwa wananchi wanaoenda kuwahudumia.
Akizungumza
katika hafla fupi ya kufunga mafunzo elekezi kwa Manaibu Wasajili na Mahakimu
Wakazi Wafawidhi yaliyofanyika kwa muda wa siku tano kuanzia tarehe 12 hadi 16
Mahakama Kuu Kituo Jumuishi cha Masuala ya Familia Temeke jana tarehe 16
Desemba 2023, Mhe Kainda alisema, niwakumbushe kuzingatia maelekezo yote
yaliyotolewa na Viongozi wa ngazi ya juu wa Muhimili ili yawajengee msingi
imara wa kutekeleza majukumu yao ya kila siku ya kiuongozi na utoaji haki kwa
wananchi.
“Nendeni
mkachape kazi acheni kufanya kazi kwa mazoea chungeni kauli zenu zingatieni
viapo vyenu mtekelezapo majukumu yenu, msizime simu zenu muda wote wa kazi,
muwe wakweli achene kufanya kazi kiujanja ujanja, mnapotoka hapa ondokaneni na
tabia za usanii na muhakikishe mnashirikiana na watumishi wengine katika vituo
vyenu na pia mtapimwa kila siku kwa matendo yenu”, alisisitiza Mhe. Kainda.
Mhe.
Kainda amewaonya Manaibu Wasajili na Mahakimu Wakazi Wafawidhi kuwa watakapo
kuwa vituoni kuachana mazoea yasiyokuwa na tija hata kama Naibu Msajili
unafahamia na Jaji Mfawidhi au na mtu mwingine yeyote. Akawataka kutotengeneza mazingira
yanayoleta tashwishwi na akawaomba wakati wa kazi kuhakikisha wanatenganisha
kazi na mazoea ili kuongeza ufanisi na kuleta weledi katika kazi kwa kuzingatia
salamu ya Mahakama ya uadilifu, weledi na uwajibikaji.
“Achani
tabia za kujipendekeza kwa viongozi wenu jengeni utamaduni unaimarisha utendaji
kazi mahusiano mengine yasiyo rasmi yataharibu kazi na kuigharimu taasisi,
hakuna kiongozi atavumilia tabia hizo, wakati wa kazi tufanye kazi hata kama ni
rafiki yako mkutane muda husiyo wa kazi”, alisisitiza Mhe. Kainda.
Mhe.
Kainda amekumbusha Manaibu Wasajili kuwa, watafanya kazi kwa karibu sana na Majaji
Wafawidhi katika vituo vyao, wanapaswa kwenda kuwasaidia kutimiza jukumu la
kutenda haki kwa kuzingatia miiko ya kiuongozi, mashauriano, ushirikiano na
uwazi bila kumuonea mtumishi ama mtu yeyote.
“Katika
ofisi zenu mtamkuta na Watendaji wa Mahakama katika Kanda zenu ni lazima
mshirikiane nao katika kufanya kazi bila kubaguana, ofisi ya Mtendaji ni ofisi
pacha ya Naibu `Msajili, hivyo basi katika kupanga, kuratibu na kutekeleza majukumu
yenu ni lazima mshirikiane, hakuna gharama zozote za mashauriano katika
kuhakikisha shughuli za kitaasisi zinafanikiwa kama inavyokusudiwa hii
itasaidia kupunguza malalamiko ya wananchi dhidi ya utendaji kazi wa taasisi”,
alieleza Mhe. Kainda.
Naye,
Naibu Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania na Naibu Mkurugenzi wa Kurugenzi ya
Usimamizi wa Mashauri Mahakama ya Tanzania, Mhe. Hawa Mguruta akitoa neno la
shukurani kwa niaba ya washiriki wa mafunzo hayo, alisema mafunzo hayo yatakuwa
chachu ya kuongeza uhodari wa utendaji kazi kwao.
“Napenda
kuushukuru Uongozi wa Mahakama ya Tanzania kwa kufanikisha mafunzo haya kwa
kweli tumeelimika vya kutosha mada zilizotolewa na wawezeshaji waliowasilisha
walikuwa wabobevu kiasi kwamba tumepata elimu na maarifa kupita kiasi na sasa
tupo tayari na tumeiva kwa ajili ya kwenda kuanza kutekeleza majukumu yetu
mapya kwa ufanisi na weledi mkubwa”, alisema Mhe. Mguruta.
Mhe.
Mguruta alinukuu baadhi ya maneno ya washiriki wa mafunzo hayo waliokiri kuwa
kama watumishi wa Mahakama walishashiriki mafunzo mbalimbali ya kitaasisi
lakini mafunzo hayo yaliyohitimisha jana tarehe 16 Desemba 2023 yalikuwa mazuri
kupita kiasi na kubeba maono ya taasisi, hivyo kama washiriki wanajivuna kupata
mafunzo bora kabisa yatayowasaidia kutimiza ndoto za Mahakama ya Tanzania
kupitia utendaji kazi wao.
Msajili wa Mahakama ya Rufani na Kaimu Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Sylvester Kainda akitoa hotuba ya kufunga mafunzo elekezi kwa Manaibu Wasajili na Mahakimu Wakazi Wafawidhi jana tarehe 16 Desemba 2023, katika ukumbi wa Mahakama Kuu Kituo Jumuishi cha Masuala ya Familia Temeke.
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Divisheni ya Biashara Mhe. Cyprian Mkeha akitoa mada ya namna bora ya kushughulikia mashauri ya madai ya gharama za uendeshaji wa shauri kwa mshindi wa amri ya tuzo.
Naibu Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Mary Moyo akiwakumbusha Manaibu Wasajili na Mahakimu Wakazi Wafawidhi mambo yanayohusu utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku wawapo vituo vya kazi. (Does and Don'ts)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni