Na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Dar es Salaam
Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel amesema Chama cha Ushirika cha Akiba na Mikopo (SACCOS) siyo mradi au kisima cha kufuja fedha bali ni sehemu ya kupata ahueni pale mwanachama anapokuwa na uhitaji.
Akizungumza wakati anafungua Mkutano wa Mkuu wa Mahakama Saccos uliofanyika katika Ukumbi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dar es Salaam jana tarehe 16 Desemba, 2023, Prof. Ole Gabriel alitaja sababu tano zinazofanya Saccos nyingi kufirisika.
Sababu hizo ni wanachama kukosa uaminifu na majungu, ukosefu wa ubunifu kwa Viongozi, mikopo kutorejeshwa kwa wakati, uelewa mdogo kuhusu mikopo na fedha na uwepo wa malumbano kwa Viongozi.
"Saccos lazima iwe na nguvu na wakati mwingine iwe kama benki, ningefurahi kama Saccos ya Mahakama itakuwa ya mfano," Mtendaji Mkuu aliwaambia wanachama hao.
Aliwataka wanachama hao kufuata sheria, ikiwemo Katiba ya Chama na miongozo iliyopo nakurudisha mikopo kwa wakati ili wengine waweze kukopeshwa.
Mtendaji Mkuu pia aliwahimza kutumia mikopo wanayoomba katika malengo yaliyokusudiwa na kufanya mambo yenye tija.
Awali, Mwenyekiti wa Bodi ya Mahakama Saccos, Bw. Mkufya Matope aliwasilisha ombi la kuongezewa mtaji uwe toshelevu, kuweza kuwakopesha wanachama wao.
Alisema kuwa mwajiri ni nguzo muhimu kufanya vyama viwe na uwezo mkubwa wa kiuchumi kuweza kutafuta mahitaji ya kifedha na kuboresha hali za maisha ya watumishi wake.
"Uongozi wa Mahakama Saccos unakuomba kuangalia namna unavyoona inafaa kuweza kukiongezea mtaji chama hiki kiweze kuimarisha uwezo wake wa kutoa huduma kwa wanachama wake, jambo hili ni jema kwa mwajiri kwenda kwa watumishi wake," alisema.
Aliomba Viongozi kupatiwa nafasi ya kuzunguka mikoani na kufanya uhamasishaji ili kuongeza wanachama na kuwapatia mafunzo watumishi wa Mahakama na wanachama wa Saccos hiyo katika kutekeleza mojawapo ya misingi ya ushirika duniani ambayo ni elimu.
Mwenyekiti huyo pia aliomba wapatiwe fursa ya kutumia makongamano, maadhimisho, sherehe, mikutano na maonyesho kuhamisha watumishi ili kuongeza idadi ya wanachama.
Kadhalika, Bw. Matope aliomba Mahakama Saccos kupatiwa vyumba viwili kwa matumizi mbalimbali ya ofisi na uendeshaji wa shughuli za chama hicho.
Alieleza kuwa Chama hicho kinatarajia kuandaa mkataba wa mahusiano kati ya mwajiri na Mahakama Saccos kama sheria ya ushirika inavyohitaji.
Mwenyekiti wa Bodi ya Mahakama Saccos, Bw. Mkufya Matope (kushoto) akiwasilisha taarifa ya utendaji ya chama hiyo. Viongozi wengine meza kuu ni Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel (wa pili kushoto) akifuatiwa na Menejà wa Saccos Geoffrey Lulenga na Mkaguzi wa Nje wa Saccos Brighton Mwangonda.
Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel(katikati) akiwa katika picha ya pamoja na sehemu ya Viongozi wa Mahakama Saccos.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni