Ijumaa, 15 Desemba 2023

LENGO LA UTEKELEZAJI WA AMRI YA TUZO SIYO KUMKOMOA MDAIWA; JAJI MKEHA

Na. Innocent Kansha - Mahakama

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Divisheni ya Biashara Mhe. Cyprian Mkeha amewambia Manaibu Wasajili na Mahakimu Wakazi Wafawidhi kwamba utekelezaji wa amri ya tuzo ya hukumu hauna lengo la kukomoa au kumnyanyasa mdaiwa bali una lengo la kuhakikisha haki ya mshindi wa tuzo inapatikana kama Mahakama ilivyoamuru katika shauri la madai husika.

Ameyasema hayo wakati akitoa mada ya Utekelezaji wa amri ya tuzo na maamuzi ya Mahakama mara baada ya shauri la madai kutamatika katika mafunzo elekezi kwa Manaibu Wasajili na Mahakimu Wakazi Wafawidhi yanayoendelea katika ukumbi wa Mahakama Kuu Kituo Jumuishi cha Masuala ya Familia Temeke leo tarehe 15 Desemba, 2023.

Mhe. Mkeha amesema, kwa mujibu wa amri ya 21 kanuni ya kwanza (1) na ya pili (2) ya sheria ya mwenendo wa kesi za madai Sura ya 33 na Kanuni za uendeshaji kesi za madai Mahakama ya Mwanzo kanuni ya 56 kanuni ndogo ya kwanza (1) zinaeleza kwamba si lazima kila shauri la madai lipitie hatua za utekelezaji wa tuzo bali ni busara ya mdaiwa aliyeamriwa na Mahakama kutekeleza amri ya tuzo bila shuruti ya hatua ya utekelezaji wa amri ya tuzo hiyo.

Mhe. Mkeha amesema utekelezaji wa amri ya tuzo au maamuzi mengine kisheria ni jia maalumu ya kisheria ya kumlazimisha mdaiwa (Judgement debtor) kulipa ama kutekeleza amri ya tuzo ya Mahakama kama ilivyoamriwa kwenye maamuzi ya Mahakama. Lengo siyo kumdhalilisha mdaiwa bali zoezi la utekelezaji wa amri ya tuzo linapaswa kuzingatia sheria, kanuni na miongozo mingine kwa mujibu wa sheria zilizowekwa.

“Ifahamike kuwa utekelezaji ni lazima uzingatie sheria na pia utawaliwe na busara kubwa ya Mahakama wakati wote wa utoaji wa maamuzi ama amri zinazoendesha zoezi la utekelezaji wa amri ya tuzo ili kutenda haki iliyoamriwa na Mahakama”, amesema Mhe. Mkeha

Mhe. Mkeha anasema hakuna tafsiri ya moja kwa moja ya utekelezaji wa amri ya tuzo lakini rejea za kesi mbalimbali za mashauri ya madai zimetafsiri nini maana halisi ya uekelezaji wa amri ya tuzo kuwa ni namna au njia ya kisheria itakayotumika na Mahakama kutekeleza amri ya tuzo iliyotolewa inayoagiza mshindi wa tuzo (Judgement creditor) apate staki zake zote alizopewa na Mahakama husika katika shuri la madai.

“Ni muhimu muhusika kutambua silaha na vifaa kwa maana ya sheria zinazotumika katika kutekeleza utekelezaji wa amri ya tuzo mosi ni sheria ya mwenendo wa mashauri ya madai Sura ya 33 (amri ya 21, kanuni 1 hadi 101), Tangazo la Serikali namba 314 la mwaka 1964 ya kanuni za uendeshaji wa mashauri ya madai Mahakama za Mwanzo na Sheria ya Ukomo wa Muda namba 10 ya mwaka 1971 pamoja na kesi rejea za Mahakama ya juu zinazotoa miongozo mbalimbali ya kisheria katika eneo la utekelezaji wa amri ya tuzo”, amesema Jaji Mkeha.

Maombi ya kuomba amri ya utekelezaji wa tuzo mara zote yanatakiwa kufanywa na mshinda wa tuzo au wakili wake kwa njia ya maandishi na pengine mara chache hufanywa kwa njia ya mdomo katika mazingira maalum. Siyo kazi ya Mahakama yenyewe kuanzisha maombi ya utekelezaji wa tuzo au ukamataji wa mali (Suo moto), isipokuwa kwa kanuni ya 54 ya kanuni za uendeshaji mashauri ya madai kwa Mahakama za Mwanzo ndiyo yenye mamlaka ya kuanzisha mchakato huo.

“Mleta maombi katika maombi yake anatakiwa kuiomba Mahakama kumlazimisha mdaiwa kulipa stahiki zake zote na kueleza njia rahisi ya kufanikisha utekelezaji wa tuzo iliyotolewa na Mahakama dhidi ya mdaiwa na maombi hayo ni lazima yaende sambamba na kilichoamriwa katika tuzo ya Mahakama”, amesisitiza Jaji Mkeha.

Mhe. Mkeha amewasisitiza Manaibu Wasajili na Mahakimu Wakazi Wafawidhi kwamba, utekelezaji wa amri ya tuzo ni mchakato unaochukua hatua mbalimbali za kisheri unaowahusisha wadau mbalimbali Madalali na Wasambaza Nyaraka za Mahakama, Watathimini wa Serikali, Mawakili, Wadaawa na Mahakama yenyewe na wala siyo tukio la mara moja utekelezaji wa amri ya tuzo unatakiwa utekelezwe kwa kuzingatia sheria na umakini mkubwa ili haki ionekane imetendeka.  

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Divisheni ya Biashara Mhe. Cyprian Mkeha akitoa mada ya Utekelezaji wa amri ya tuzo na maamuzi ya Mahakama mara baada ya shauri la madai kutamatika kwa Manaibu Wasajili na Mahakimu Wakazi Wafawidhi (hawapo pichani) leo tarehe 15 Desemba, 2023 katika ukumbi wa mikutano wa Mahakama Kuu Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki cha Masuala ya Familia Temeke.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Divisheni ya Biashara Mhe. Cyprian Mkeha akitoa mada ya Utekelezaji wa amri ya tuzo na maamuzi ya Mahakama mara baada ya shauri la madai kutamatika kwa Manaibu Wasajili na Mahakimu Wakazi Wafawidhi

Sehemu ya Manaibu Wasajili na Mahakimu Wakazi Wafawidhi wakiwa wanafuatilia mada kwenye mafunzo elekezi katika ukumbi wa mikutano wa Mahakama Kuu Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki cha Masuala ya Familia Temeke.

(Picha na Innocent Kansha - Mahakama)

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni