Na Mary Gwera, Mahakama-Morogoro
Maafisa Bajeti wa Mahakama nchini wametakiwa kushiriki kikamilifu katika mchakato wa maandalizi ya bajeti ya mwaka ujao wa fedha 2024/2025 ili kurahisisha utekelezaji wa kazi za Mhimili huo.
Akizungumza hivi karibuni mkoani Morogoro wakati akifungua mafunzo ya siku tatu kwa Maafisa hao, Mtendaji wa Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki Kanda ya Morogoro, Bw. Ahmed Ng’eni aliwaambia washiriki wa mafunzo kufuatilia kwa umakini mada zinazotolewa.
“Ninawasihi pia kuzingatia maeneo ya vipaumbele kwa kuyajumuisha katika bajeti mtakazoandaa ili kutokwamisha utekelezaji wa shughuli za Mahakama hususani za kimaboresho,” alisema Bw. Ng’eni.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Msaidizi wa Mipango na Ufuatiliaji Mahakama ya Tanzania, Bi. Gladys Qambaita alisema kuwa lengo mahsusi la mafunzo hayo ni kuwajengea uwezo Maafisa Bajeti katika eneo la maandalizi ya bajeti Pamoja na utekelezaji wake.
“Mafunzo haya yataangazia sehemu tatu (3) ambazo ni, Maandalizi ya bajeti, Mifumo inayotumika katika maandalizi na utekelezaji wa bajeti pamoja na Utekelezaji wa bajeti,” alisema Bi. Gladys.
Aliwaeleza washiriki wa mafunzo hayo kuandaa bajeti kulingana na vipaumbele lakini pia kuendana na ukomo wa vifungu vyao.
Aliongeza kuwa, bajeti ya Serikali ni chombo muhimu cha kiutawala na kiuwajibikaji ambacho kinahakikisha kuwa utekelezaji wa Mipango na Sera, matumizi bora ya rasilimali, usimamizi mzuri wa kazi na majukumu ya Serikali yanazingatiwa ipasavyo.
Katika eneo la utekelezaji, Bi. Gladys alisema mafunzo hayo yameangazia katika kufanya Maandalizi ya Taarifa za Utekelezaji, Maandalizi ya Daftari la Vihatarishi na katika eneo la Uhamisho wa fedha (reallocation).
Aidha, alisema kwamba kila hatua katika Mzuko wa Bajeti ni muhimu katika kuiwezesha Taasisi kufikia malengo yake, na kusisitiza kuwa, hatua ya maandalizi ni ya muhimu zaidi kwa sababu ubora nyumba huanza na msingi.
“Maandalizi mazuri ya bajeti hupelekea utekelezaji mzuri wa bajeti na vilevile maandalizi mabovu ya bajeti huleta changamoto katika utekelezaji wa bajeti ikiwemo Uhamisho wa fedha usio wa lazima, hivyo ni matumaini yangu mafunzo haya yatawajengea uwezo ili muweze kufanya maandalizi bora ya bajeti pamoja na utekelezaji wake,” alisisitiza.
Jumla ya Washiriki 46 walishiriki katika mafunzo hayo ambapo walifundishwa mada mbalimbali ikiwa ni pamoja na jinsi ya kuepuka vihatarishi (risk) wakati wa uaandaji wa bajeti ili kuepuka matatizo wakati wa utekelezaji.
Mtendaji wa Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki (IJC) Morogoro, Bw. Ahmed Ng'eni akizungumza wakati alipokuwa akifungua Mafunzo ya Maafisa Bajeti wa Mahakama ya Tanzania yaliyofanyika hivi karibuni. Mafunzo hayo ya siku tatu yalifanyika katika ukumbi wa mikutano wa Kituo hicho.
Mchumi kutoka Kurugenzi ya Mipango na Ufuatiliaji-Mahakama ya Tanzania, Bw. John Magere (aliyesimama) akizungumza jambo wakati wa hafla ya ufunguzi wa mafunzo kwa Maafisa Bajeti. Walioketi ni sehemu ya Maafisa kutoka Kurugenzi hiyo.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni