Na. Innocent Kansha – Mahakama.
Jaji
Mfawidhi Mahakama Kuu Kituo cha Usuluhishi, Mhe. Zahra Maruma amekutana na
Ujumbe kutoka Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS) pamoja na Kituo cha Kimataifa cha usuluhishi Tanzania (TIAC) na kufanya nao mazungumzo
juu ya muelekeo wa kituo hicho katika utekelezaji wa kauli mbiu ya wiki ya
sheria ya mwaka 2023 kwa vitendo.
Akizungumza
na ujumbe huo Ofisini kwake jijini Dar es Salaam alipotembelewa na ujumbe kutoka
TLS leo tarehe 28 Desemba, 2023 Mhe. Maruma amesema, Kituo kilianza zoezi la
kuwatembelea na kuzungumza na wadau kama taasisi za fedha (Mabenki), na pia
Kituo kilifanya utafiti mdogo kwenye mabaraza ya usuluhishi ya kata katika Wilaya zote za Mkoa wa Dar es salaam yanayofanya usuluhishi ili kutambua changamoto zinazokwamisha zoezi la usuluhishi
wa migogoro kwa njia mbadala.
“Lengo
kubwa ni kujitathimini katika utekelezaji wa maudhui ya kaulimbiu ya wiki
na siku ya sheria ya mwaka huu 2023 ambayo inasisitiza umuhimu wa utatuzi wa
migogoro kwa njia ya usuluhishi katika kukuza uchumi endelevu: wajibu wa
Mahakama na Wadau”, amesema Jaji Maruma.
Mhe.
Maruma amesema, Kituo cha Usuluhishi kinaowajibu wa kusimamia na kutekeleza kauli mbiu hiyo, kwa kuangalia ni namna gani kituo kinaweza kuboresha matumizi ya
utatuzi wa migogoro kwa njia mbadala.
Mhe.
Maruma akanukuu hotuba ya Jaji Mkuu Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma aliyoitoa
wakati wa kilele cha siku ya sheria nchini “Watu wenye migogoro, kama walivyo
watu wenye maumivu au ugonjwa, wanapofika mahakamani lengo lao kamwe siyo
kuwaona Majaji waliovaa majoho nadhifu au kuona nyumba ya Mahakama ilivyotiwa
nakshi nzuri. Wanachofuata ni nafuu, na wanaitaka hiyo nafuu kwa haraka na kwa
gharama ndogo”.
Mhe.
Maruma akaongeza kuwa japo usuluhishi ndiyo jukumu la msingi la kituo la
kuhakikisha kituo kinasuluhisha migogoro kwa njia ya usuluhishi kwa mashauri ya
Mahakama Kuu lakini pia Kituo kinaangalia kwa ujumla namna ya kuendelea kuiishi kaulimbiu hiyo ili iweze kuwasaidia wadau kutatua mogogoro.
“Tumeona
si vyema tukaacha kauli mbiu hii iende hivi hivi tumepaga kuendelea
kujitathimini kwa mwaka huu tuone tumefanya nini lakini pia kupata uzoefu
kutoka kwenu, kutathimini kwa kuona kama sheria hizi zinaturuhusu kufanya
vizuri kwenye maeneo hayo kwa kutambua changamoto, uelewa na kutambua mchango
wenu kama wadau muhimu”, ameongeza Jaji Maruma.
Aidha,
Mhe. Maruma amesema siyo kwamba Mahakama inafanya Usuluhishi peke yake bali kuna
njia nyingine kama Upatanishi, wapatanishi binafsi hivyo Kituo kimeona kifanye juhudi za pamoja ili kiweze kuibua
maeneo ambayo kituo kimefanya vizuri na kuangalia sehemu zenye changamoto ili
zifanyiwe kazi kwa pamoja.
Mhe.
Maruma amesema kuwa Kituo kimepanga kuandaa tukio
maalumu la kuwatambua rasmi wadau wale wote waliokisaidia kufanikisha utatuzi
wa migogoro kwa njia mbadala litakalo fanyika tarehe 16 Januari, 2024 kwa hiyo TLS na TIAC ni miongoni mwao. Kupitia hafla hiyo
kituo kitapenda kupata uzoefu kutoka kwa wadau hao namna wanavyotekeleza
utatuzi wa mogogoro kwa njia mbadala ili kupata maoni ya maeneo ya kuboresha
kwa upande wa Mahakama.
“Kuna
usemi kuwa mawakili wamekuwa wakikwamisha ile hatua ya usuluhishi au
upatanishi sasa usemi huu unaweza kuwa na ukweli ama usiwe na ukweli kwani
changamoto zipo pande zote mbili”, ameeleza Mhe. Maruma.
Mathalani,
Mhe. Maruma amesema Kituo kimefanikiwa kupokea mashauri ya usuluhishi 372,
mashauri yaliyotatuliwa kwa njia za usuluhishi ni 84 na mashauri 253 hayakufanikiwa
kusuluhishwa, hivyo kuendelea mahakamani kusikilizwa kwa njia ya kawaida. Bado
hali hiyo unaonyesha muamko ni mdogo wa watu kumaliza mashauri yao kwa njia
mbadala ya utatuzi wa migogoro.
Kwa upande wake mwakilishi wa ujumbe
kutoka TLS, wakili msomi Dkt. Rugemeleza Nshalla ambaye ni Mwenyekiti wa Bodi ya Kituo cha Kimataifa cha usuluhishi Tanzania (TIAC) amesema mabadiliko ya sheria ya mwaka 2019 yana lengo la kuhimiza hatua ya
usuluhishi katika mashauri ya madai na kufanya wadaawa wasichukulie kama kitu cha mchezo mchezo
hatua hiyo muhimu ya usuluhishi katika mashauri.
“Labda
wadaawa wengi katika mashauri haya hawaelewi nini maana ya usuluhishi mfano mimi
nina kesi moja iliyokaa mahakamani toka mwaka 2001 tokea nina miaka mitano na
nusu kwenye uwakili hadi sasa nina miaka 28, kesi kama hii inakupotezea muda na
hata mteja hawezi kukulipa tena, lakini kama tungetumia njia ya utatuzi wa
mgogoro kwa njia mbadala tusingekuwa mahakamani kwa muda wote huo hadi sasa”,
amesema Dkt. Nshalla
Dkt. Nshalla amesema, falsafa ambayo mawakili wengi na hata wateja
hawajazingatia ni thamani ya muda, wakili angekuwa amejiwekea lengo la kumaliza
idadi ya kesi fulani kwa mwaka, kama ilivyo kwa Majaji walivyojiwekea malengo
ya kumaliza kesi 220 kwa mwaka nadhani faida ya usuluhishi ingeonekana kwa
mawakili na wateja na kufanya uwakilishi wa tija.
“Kwa
kuzingatia haya mabadiliko ya sheria ya mwaka 2019 wadau wote wa Mahakama,
mawakili na Chama cha chetu cha TLS ni vema tukapanga mikakati madhubuti ya
kuangalia ni namna gani tujipange kuwaelimisha watu kuhusiana na masuala ya
upatanishi na usuluhishi ili kuokoa muda wa kuendesha kesi na kwa gharama nafuu”,
ameongeza Mhe. Dkt. Nshalla.
Aidha, Dkt. Nshalla akashauri njia nyingine ya kutoa elimu ya utatuzi wa migogoro kwa
njia mbadala ni kutumia majukwaa ya mawakili na Baraza la shule ya sheria kutoa
mada za kusaidia wadaawa kuzifahamu faida za usuluhishi kwa njia mbadala.
Naye, Mratibu wa Kituo cha Kimataifa cha usuluhishi Tanzania (TIAC) Bi. Magreth Magoma akataja changamoto katika usuluhishi ikiwemo ya watu kutotambua shughuli za chao. Hivyo inahitajika utoaji wa elimu kwa mawakili na wadau wa usuluhishi.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni