Na Eunice Lugiana, Mahakama Kuu-Dar es Salaam
Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dar es Salaam, Mhe. Salma Maghimbi amewapongeza watumishi wa Kanda hiyo kwa kuchapa kazi na kuonyesha moyo wa kujituma na kuwezesha Kanda hiyo kupunguza mlundikano wa mashauri 300 ya muda mrefu yakiwemo ya ugaidi yaliyofanyiwa kazi na kuisha wakati wa vikao maalum vya kusikiliza mashauri hayo vilivyofanyika kati ya Oktoba na Desemba 2023.
Jaji Maghimbi aliyasema hayo jana tarehe 22 Desemba, 2023 katika ukumbi wa Mahakama Kuu Dar es Salaam alipokuwa akitoa salamu za mwaka mpya kwa watumishi wa Kanda hiyo.
“Nafahamu Viongozi wengi tulikuwa wageni lakini tumepata ushirikiano mkubwa kutoka kwa watumishi na kuwezesha kwa kasi kubwa kufanya kazi kwa pamoja na kuweza kuitoa Kanda katika mzigo mkubwa wa mashauri hadi kufikia mashauri 50, hii ni hatua nzuri,” alisema Mhe. Maghimbi.
Jaji Maghimbi aliwapongeza watumishi wote bila kujali kada kwakuwa wote wameshiriki katika mafanikio hayo. Kwa sasa mashauri mlundikano ni chini ya 50 tofauti na ilivyokuwa awali.
Aidha, watumishi wamesisitizwa kuendeleza umoja, mshikamano na utendaji kazi mzuri kwa lengo la kuondoa mashauri ya mlundikano. Aliongeza pia kwa kusisitiza matumizi ya mifumo mbalimbali iliyopo katika usikilizwaji wa mashauri ukiwemo mfumo wa e-CMS na Mfumo wa Kunukuu na Kutafsiri (T.T.S).
Alieleza kuwa kwa sasa hakuna njia mbadala ya kuepuka Mifumo hiyo zaidi ya kujifunza na kutatua changamoto chache zinazojitokeza ili kazi za kimahakama ziendelee kidijitali.
Amewaahidi watumishi kuandaa mafunzo ya kujikumbusha kuhusu Mpango Mkakati wa Mhimili huo na Mifumo mingine ili kuwezesha kila mtumishi kushiriki kikamilifu katika kuutekeleza kwa mwaka 2024.
Mhe. Maghimbi alitumia kikao hicho kuwatakia heri watumishi wote katika sherehe za mwisho wa mwaka na mwaka mpya 2024.
Kwa mwaka huu 2023 Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam ilielekeza nguvu kubwa katika kuleta mabadiliko ya kifikra na kimtazamo. Nguvu hizo ambazo pia zimetokana na watumishi zimesaidia kuboresha utendaji kazi uliofanikisha kupunguza mashauri ya mlundikano.
Mahakama hiyo pia imejiwekea malengo ya kuwa Kituo bora cha mfano katika usimamizi wa shughuli za mashauri na kiutawala katika Mahakama ya Tanzania.
Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dar es Salaam, Mhe. Salma Maghimbi akizungumza na Watumishi wa Kanda hiyo (hawapo katika picha) jana tarehe 22 Desemba, 2023.
Watumishi wa Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam wakimsikiliza Jaji Mfawidhi wa Kanda hiyo, Mhe. Salma Maghimbi (hayupo katika picha) wakati akitoa salamu za pongezi kwa Watumishi hao.
(Habari hii imehaririwa na Mary Gwera, Mahakama)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni