Jumatatu, 11 Desemba 2023

MAHAKAMA KUDIJITI NYARAKA ZOTE KATIKA MASJALA

Na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Dar es Salaam

Mahakama ya Tanzania imepitisha uamuzi unaowataka Wasajili na Mahakimu Wafawidhi katika Mahakama zote kusimamia mpango wa kudijiti nyaraka zote katika Masjala nchini.

Hatua hiyo imetangazwa leo tarehe 11 Desemba, 2023 na Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma katika hafla ya kuwaapisha Naibu Wasajili 30 na Makimu Wafawidhi 10 wapya iliyofanyika katika Ukumbi wa Kimataifa wa Mwalimu Nyerere jijini Dar es Salaam.

“Uamuzi umeshafanyika kwa Wasajili na Mahakimu Wafawidhi kusimamia mpango wa kudijiti nyaraka zote katika Masjala kuzitoa katika mfumo wa analojia, makaratasi na kuzihamisha kwenda katika mfumo wa kidijitali,” amesema.

Jaji Mkuu amebainisha kuwa timu ya wataalam ndani ya Mahakama kwa kushirikiana na wataalamu kutoka Mamlaka ya Serikali Mtandao (eGA) tayari wametayarisha mpango kazi wa kudigiti nyaraka zote za Mahakama katika Masjala zote.

Amesema wanaoweza kufanikisha azma hiyo ni Naibu Wasajili na Mahakimu Wafawidhi, hivyo akawaomba kusoma mpango kazi huo kwenye mafunzo elekezi watakayopewa ili kuelewa majukumu yao katika kudijiti nyaraka.

 “Mahakama hatuwezi kurudi nyuma tena. Mmesikia Serikali ipo katika safari ya kufikia utoaji wa huduma za umma kwa njia za kidijitali na kuna program inaendelea, hivyo sisi Mahakama tukibaki nyuma tutaonekana tumeshindwa kwenda na kasi ya mabadiliko,” Mhe. Prof. Juma amesema.

Jaji Mkuu pia amewakumbusha Viongozi hao kuhusu uwepo wa mfumo mpya wa kielektroniki wa kuratibu mashauri ambao umefungwa kwenye Masjala za Mahakama zote. 

Amesema kuwa mafanikio ya mfumo huo yatategemea Naibu Wasajili na Mahakimu Wafawidhi kwa sababu wao ndiyo wanaweza kutoa majibu kama unafanya kazi.

“Siku zote tuwe tunaangalia faida kubwa ambayo inatokana na huu mfumo, ikiwemo kusajili mashauri kwa njia ya mtandao kwa kasi, wepesi na uwazi zaidi, kupanga mashauri kwa Majaji na Mahakimu…

“Mfumo huu utatuwezesha kuandika hukumu na mienendo ya mashauri kadri shauri linavyoendelea na mwisho wa siku mwananchi atapata kumbukumbu ya mambo yote yanayotokea mahakamani,” amesema.

Jaji Mkuu amebainisha kuwa mfumo huo ambao unasomana na mifumo mingine kutoka NIDA, RITA na Ofisi ya Taifa ya Mashtaka utaongezea uwazi, kuaminika na kuifanya Mahakama kuwa imara zaidi. 

Amesema kama Naibu Wasajili na Mahakimu Wafawidhi watashindwa kutumia mfumo huo kikamilifu, ule uwekezaji mkubwa wa fedha za umma zilizotumika kuujenga hautakuwa na maana yoyote.

Jaji Mkuu amewaambia Viongozi hao pia kuwa nafasi za Naibu Wasajili na Hakimu Wafawidhi ni muhimu katika uendeshaji na usimamizi wa shughuli za kimahakama za kila siku.

Amesema kuwa injini ya Mahakama ni Masjala ambazo zipo chini yao, hivyo baada ya kuapishwa na kupewa nyenzo Mahakama inategemea watasaidia kusukuma utoaji wa haki.

“Mtu wa kwanza ambaye mwananchi atakutana naye ni mtumishi ambaye yupo chini ya masjala zenu. Uwezo wa injini zenu unatakiwa usiwe tu wa kujifungia ofisini, lazima uelewe kila kitu kinachotendeka nje na ndani ya ofisi,” amesema.

Mhe. Prof. Juma amesema kuna baadhi ya Masjala kama injini hazifanyi kazi, hivyo akaonya kuwa mwananchi anapofika Masjala yoyote anatakiwa kupatiwa huduma inayohusu Masjala nyingine yoyote hapa nchini.

“Hatutaki tena tumwambie mwananchi nenda kwenye Masjala fulani utapata hiyo huduma, ndiyo maana tunafunga mitambo ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) kuhakikisha kuwa kila kituo kitakuwa kinatoa majibu kwa kila mtu ambaye atakuwa anatafuta huduma.

“Tukumbuke kuwa Masjala ni injini ambayo ufanisi wa Mahakama nzima unategemea ni namna gani tunafanya kazi kwa sababu ni barabara inayotiririsha taarifa zote za kimahakama, kutoa wito na kuwasiliana na wadaawa wote,” amesema.

Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma akisisitiza jambo alipokuwa anazungumza kwenye hafla ya kuwuapisha Naibu Wasajili na kuwapa nyenzo za kazi Mahakimu Wafawidhi wapya.

Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma aklimkabidhi nyaraka za kufanyia kazi Naibu Msajili na Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Mhe. Franco Kiswaga.


Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya  Tanzania, Mhe. Mustapher Mohamed Siyasi akimwapisha Mhe. Roda Ngimilanga kuwa Naibu Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania.


Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya  Tanzania, Mhe. Mustapher Mohamed Siyasi akimwapisha Mhe. Moses Ndelwa kuwa Naibu Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania.


Meza Kuu ikiongozwa na Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma (katikakati waliokaa) ikiwa katika picha ya patoja na sehemu ya Naibu Wasajili wapya. Wengine kwenye meza kuu ni Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Mustapher Mohamed Siyani (kushoto) na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dar es Salaam, Mhe. Salma Maghimbi (kula).

 

Naibu Wasajili wapya wakifuatilia matukio mbalimbali kwenye hafla hiyo. Picha chini ni sehemu ya Majaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania wakiwa katika hafla ya kuwaapisha Naibu Wasajili na kuwakabidhi nyenzo Mahakimu Wafawidhi wapya.


Picha na Innocent Kansha-Mahakama, Dar es Salaam.





Hakuna maoni:

Chapisha Maoni