Na. Innocent Kansha - Mahakama
Mkurungenzi
wa Usimamizi wa Mashauri Mahakama ya Tanzania, Naibu Msajili Mhe. Desdery
Kamugisha amewaambia Manaibu Wasajili na Mahakimu Wakazi Wafawidhi kuwa,
wanapaswa kutambua kuwa Masjala za Mahakama ndiyo moyo wa shughuli zote za
Mahakama za utoaji haki kwa wananchi, hivyo wanapaswa kuzilinda na kuzisimamia
kwa mujibu wa Sheria, Miongozo, Waraka na Kanuni mahususi zilizotungwa kwa
ajili ya kuziendesha masjala hizo.
Akitoa
mada ya namna bora ya kusimamia masjala za Mahakama za mashauri katika mafunzo elekezi kwa
Manaibu Wasajili na Mahakimu Wakazi Wafawidhi, Mhe. Kamugisha amesema majukumu
ya karani katika masjala ya Mahakama yapo kimuundo wa kiutumishi kama ilivyo
kwa taasisi nyingine za umma ila sheria ya mwenendo wa kesi za madai na waraka
namba nne (4) wa mwaka 2018 wa Jaji Mkuu wa Tanzania unamtaja Naibu Msajili na
Hakimu Mfawidhi, hivyo basi kwa mujibu wa sheria masjala ya Mahakama Kuu inamilikiwa
na kusimamiwa Naibu Msajili katika uendeshaji wa shughuli zake zote za kila
siku za utoaji haki.
“Iko
miongozo, waraka na sheria mbalimbali zinazotumika kuelezea namna bora ya
kusimamia na kuendesha Masjala za Mahakama na jukumu kubwa la msingi la Naibu
Msajili, Hakimu Mkazi Mfawidhi ni mlezi na msimamia mkuu wa shughuli za
utendaji kazi wa masjala”, amesema Mhe. Kamugisha
Mhe.
Kamugisha amesema masjala ni moyo wa taasisi yoyote si kwa mahakama pekee kwani
ndiyo kitovu cha kutunza nyaraka zote na kumbukumbu zote mahususi za kitaasisi,
hivyo taasisi isiyokuwa na nyaraka ama kumbukumbu basi taasisi hiyo itakuwa
iliyokufa.
Waraka
namba nne (4) wa mwaka 2018 Jaji Mkuu wa Tanzania, sheria ya kumbukumbu na
nyaraka za Taifa, sheria ya mwenendo wa kesi za madai na miongozo mingine mingi iliyoandaliwa na viongozi wa Mahakama inaeleza kuwa majukumu yote ya usimamizi na utunzaji wa nyaraka zote za Masjala ya Mahakama ni jukumu la Naibu Msajili na Hakimu Mfawidhi.
“Waraka
namba nne (4) wa 2018 wa Jaji Mkuu wa Tanzania umetoa chaguo-msingi (by
default) na kanuni ya 10 ya kanuni ndogo za uendeshaji masjala za Mahakama Kuu zinatoa mwongozo wa kuhusu nani ana jukumu msingi la kupokea na kusajili mashauri katika masjala ya
Mahakama Kuu jukumu hilo lipo chini ya mamlaka sawa (concurrent Jurisdiction) kwa Jaji Mfawidhi na Naibu Msajili wa kituo husika”, amesisitiza Mkurugenzi wa
Mashauri.
Mhe.
Kamugisha amesema uzoefu unaonyesha kuwa Manaibu Wasajili na Mahakimu Wakazi
Wafawidhi wa ngazi zote za Mahakama wamekuwa wakiwaachia Wasaidizi wa
Kumbukumbu kumiliki na kusimamia masjala bila kufanya ufuatiliaji wa karibu wa uendeshaji
wa masjala za Mahakama. Hii imekuwa ikisabisha ucheleweshaji wa haki bila
sababu za msingi.
Mhe.
Kamugisha amesema, Masjala za Mahakama zinajitanabaisha kwa kubeba majukumu
mengi mazito na mbalimbali yanayoratibu mchakato mzima wa utoaji haki kama vile
kupokea kumbukumbu, kurekodi kumbukumbu na kuziratibu, kupokea na kufungua
mashauri na kuyapa namba, kusimamia mienendo ya majalada kutoka hatua moja hadi
nyingine, kupanga majalada ya mashauri yanayoendela na yaliyomalizika, kutoa nakala za hukumu na maamuzi mengine ya Mahakama.
Kazi
zingine za masjala ni kuandaa nyaraka za wito, kuandaa na kusambaza nyaraka
zote za amri zilizotolewa mahakamani na kuzisambaza kwa wahusika kuchambua na
kuchukua idadi halisi ya mashauri yaliyopo masjala (stock taking), kupokea,
kusoma na kuchunguza kama nyaraka zilizowasilishwa zina kidhi vigezo kwa ajili
ya kusajiliwa Mahakamani, kutunza nyaraka na vielelezo vilivyopokelewa
mahakamani na kujaza na kutunza rejista zote za Mahakama vilevile kuandaa na
kujaza rejista za kiutawala ili kuboresha utendaji kazi wa kila siku.
Mkurungenzi wa Usimamizi wa Mashauri Mahakama ya Tanzania, Naibu Msajili Mhe. Desdery Kamugisha akitoa mada ya namna bora ya kusimamia masjala za Mahakama za mashauri katika mafunzo elekezi kwa Manaibu Wasajili na Mahakimu Wakazi Wafawidhi katika ukumbi wa Mahakama Kuu Kituo Jumuishi cha Masuala ya Familia Temeke.
Sehemu ya Manaibu Wasajili na Mahakimu Wakazi Wafawidhi wakifuatilia mada katika mafunzo hayo
Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Mwanza Mhe. Wilbert Chuma akitoa mada ya namna ya kuchunguza malalamiko ya kimaadili ya Maafisa Mahakama kwa kuzingatia sheria na miongozo iliyopo kwa Manaibu Wasajili na Mahakimu Wakazi Wafawidhi wakifuatilia mada hayo.
Sehemu ya Manaibu Wasajili na Mahakimu Wakazi Wafawidhi wakifuatilia mada katika mafunzo hayo
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni