Na Mary Gwera, Mahakama-Dodoma
Waziri wa Katiba na Sheria, Balozi Mhe. Dkt. Pindi Chana leo tarehe 30 Januari, 2024 amepata wasaa wa kutembelea mabanda ya Maonesho ya Wiki ya Sheria katika Viwanja vya Nyerere ‘Square’ jijini Dodoma ambapo ametoa wito kwa wananchi kuchangamkia fursa za maonesho kama hayo ili kujua haki zao.
Akiwa katika maonesho hayo, Mhe. Dkt. Chana ametembelea mabanda kadhaa ikiwemo banda la Wadau wa Haki Jinai, Kituo cha Huduma kwa Mteja cha Mahakama na Malalamiko, Tume ya Utumishi wa Mahakama, Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Tume ya Kurekebisha Sheria na Wizara ya Katiba na Sheria.
“Kwanza nipende kusema kuwa, nimefurahi sana kutembelea maonesho haya, hivyo nitoe rai kwa watanzania kujitokeza kwenye maonesho kama haya ambayo yanatolewa bure kabisa bila gharama yoyote na vilevile yanalenga kutoa elimu kuhusu masuala ya kisheria na Mahakama kwa ujumla,” amesema Mhe. Dkt. Chana.
Hata hivyo, Waziri huyo ameipongeza pia Mahakama maandalizi mazuri ya Wiki ya Sheria na pia kwa maboresho makubwa ambayo inaendelea kufanya ikiwemo ya kuondosha mashauri kwa wakati na kuwatoa wasiwasi wananchi kuimbilia Mahakama kwakuwa ndipo haki inapopatikana.
“Kupitia maonesho haya na hata kupitia Vyombo vya Habari, Mahakama imepiga hatua za kimaboresho katika huduma zake na ninayo furaha hata katika maonesho ya mwaka huu kuna banda la Wadau wa Haki Jinai ambao pia wanawaeleza wananchi jinsi utekelezaji wa maboresho ya Kamati ya Rais Samia ya Haki Jinai yanavyotekelezwa,” ameeleza Balozi, Dkt. Chana.
Kadhalika, Waziri huyo amewahakikisha Watanzania kuwa Serikali ya Rais wa Awamu ya Sita ya Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan itaendelea kuhakikisha kuwa inatunza amani ya nchi kwa gharama yoyote.
Leo ndio siku ya mwisho ya Maonesho ya Wiki ya Sheria kwa mwaka huu, kilele cha Siku ya Sheria kitakuwa tarehe 01 Februari, 2024 ambapo Kitaifa sherehe hizo zitafanyika katika Viwanja vya Chinangali jijini Dodoma na Mgeni Rasmi atakuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Waziri wa Katiba na Sheria, Balozi Mhe. Dkt. Pindi Chana (kulia) akizungumza jambo na Mtendaji Mkuu Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante leo tarehe 30 Januari, 2024 wakati Waziri huyo alipowasili katika viwanja vya Nyerere 'Square' jijini Dodoma tayari kwa kutembelea mabanda yaliyoshiriki katika Maonesho ya Wiki ya Sheria.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni