Jumanne, 30 Januari 2024

KAIMU MSAJILI MKUU AWAALIKA WANANCHI SIKU YA SHERIA

Na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Dodoma

Maadhimisho ya Wiki ya Sheria yaliyokuwa yanafanyika Kitaifa katika Viwanja vya Nyerere Square jijini hapa yakihusisha mabanda ya maonesho yaliyokuwa yemeandaliwa na Mahakama na Wadau mbalimbali yemehitimshwa leo tarehe 30 Januari, 2024.

Mgeni Rasmi katika hafla ya kuhitimisha maadhimisho hayo alikuwa Kaimu Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Silvester Kainda, ambaye amewaalika wananchi kushiriki kwa wingi kwenye kilele cha maadhimisho hayo, ambayo ni Siku ya Sheria yatakayofanyika terehe 1 Februari, 2024.

“Nichukue fursa hii kuwaomba wananchi kujitokeza kwa wingi kwenye kilele cha maadhimisho haya ambayo ni Siku ya Sheria itakayofanyika tarehe 1 Februari, 2024 ambapo Kitaifa itakuwa katika Viwanja vya Chinangali. Mgeni Rasmi atakuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan,” amesema.

Kaimu Msajili Mkuu ametumia fursa hiyo kuwashukuru washiriki zaidi ya 35 walioshiriki katika maonesho hayo katika Viwanja vya Nyerere Square yaliyoanza tangu tarehe 24 Januari, 2024.

Kadhalika, Mhe. Kainda amewashukuru Viongozi na Wadau wote kutoka Taasisi mbalimbali waliojitolea kwa hali na mali na kuacha shughuli zao ili kuwezesha maadhimisho hayo yanafanyika kwa ufanisi mkubwa.

“Kipekee nimshukuru Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Rais wa Umoja wa Mabunge Duniani, Mhe. Dkt. Tulia Ackson kwa kutufungulia rasmi Wiki ya Sheria,” amesema.

Kaimu Msajili Mkuu pia amemshukuru Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma, Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Mustapher Mohamed Siyani, Mtendaji Mkuu wa Mahakama na Viongozi wengine kwa kufanikisha maadhimisho hayo.

Kabla ya kuhitimisha maadhimisho hayo, Mgeni Rasmi alikabidhi vyeti kwa washiriki wote wa maonesho hayo, hii ikiwa ni mara ya kwanza kwa Mahakama ya Tanzania kufanya hivyo.

Wakati wa maadhimisho hayo, mbali na Mahakama, wengine walioshiriki walikuwa Wadau wa Haki Jinai, Magereza, Uhamiaji, Polisi, Ofisi ya Taifa ya Mashtaka, Mkemia Mkuu wa Serikali, Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa.

Kaimu Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Silvester Kainda akizungumza katika hafla ya kuhitimisha maadhimisho ya Wiki ya Sheria jijini Dodoma.


Sehemu ya Watumishi wa Mahakama na wadau wakiwa katika hafla hiyo.

Sehemu ya Wadau walioshiriki kwenye Wiki ya Sheria (juu na chini) wakifuatilia kile kilichokuwa kinaendelea wakati wa kuhitimisha maadhimisho hayo.


Kaimu Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Silvester Kainda (kulia) akimkabidhi cheti Mwakilishi wa Tume ya Utumishi wa Mahakama. Picha chini akisalimiana na Mwakilishi kutoka Ofisi ya Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora baada ya kumkabishi cheti chake.


Kaimu Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Silvester Kainda (kulia) akimkabidhi cheti Mwakilishi wa Ofisi ya Taifa ya Mashtaka. Picha chini akikabidhi cheti kwa Mwakilishi wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto.



Kaimu Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Silvester Kainda (kulia) akikabidhi cheti kwa Mwakilishi wa Jeshi la Polisi. Picha chini akikabidhi cheti kwa Mwakilishi wa Wizara ya Katiba na Sheria.




Hakuna maoni:

Chapisha Maoni