Jumatano, 31 Januari 2024

MAHAKAMA MBEYA YATOA ELIMU YA SHERIA KWA IDARA YA AFYA, MAGEREZA

Mwinga Mpoli – Mahakama Mbeya 

Jaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Mbeya Mhe. Emmanuel Kawishe akiambatana na Maafisa Mahakama, mawakili wa serikali, wakili wa kujitegemea, na afisa kutoka Tume ya Usuluhishi jana tarehe 30 Januari, 2024 walitembelea hospitali ya Rufaa Mkoa wa Mbeya kutoa elimu katika masuala mbalimbali yahusuyo sheria.


Akiongea na watumishi hospitalini hapo Mhe. kawishe aliwaeleza kuwa kwa sasa masuala ya ndoa, talaka na Mirathi imekuwa ni jambo linalosumbua katika jamii, vifungu vingi vya sheria mbalimbali vinavyohusu ndoa, unyanyasaji na haki za msingi katika masuala mazima ya ndoa vinalinda ustawi wa mambo hayo.


“Tumeona umuhimu wa kuwapa elimu hii madaktari na watumishi wengine wa hospitali ya rufaa ili muweze kupata uelewa wa haki zenu katika ndoa, na kuepuka yanayokatazwa na sharia ili kufanya kazi kwa amani na utulivu…..

…Ni vigumu sana kufanya kazi kama hauna utulivu na kwa msingi huo mkiwa na amani na utulivu mtaweza kuwahudumia watanzania vizuri na kuwafanya wawe na afya njema na kuchangia katika kuleta maendeleo ya taifa kwa ujumla” alisema Jaji Kawishe


Naye Jaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Mbeya Mhe. Mussa Kassim Pomo akiongozana na Jaji wa Mahakama kuu katika kanda hiyo Mhe. Aisha Sinda, Naibu Msajili Mhe. Judith Lyimo, Waheshimiwa Mahakimu na wadau wa Mahakama wao wametembelea na kutoa elimu kwa wafungwa na Mahabusu wa Gereza la Ruanda mkoani Mbeya.


Kwa upande wao Mahabusu na wafungwa wakike na kiume wameishukuru Mahakama na wadau kwa kuwakumbuka na kuona umuhimu wa kuwatembelea na kuwasikiliza kama kuna changamoto yoyote na kupewa elimu katika masuala mbalimbali yahusuyo sharia.


Zoezi la utoaji elimu katika maadhimisho ya wiki ya sheria Mkoani Mbeya limehitimishwa jana na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Mbeya Mhe. Danstan Nduguru katika viwanja vya Kabwe jijini Mbeya kuelekea kilele cha siku ya sheria nchini hapo tarehe Mosi Februari, 2024.


Jaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Mbeya Mhe. Emmanuel Kawishe (wapili kutoka kushoto) na Mhe Naibu Msajili Mfawidhi Mahakama Kuu Kanda ya Mbeya Mhe. Aziza Temu (wapili kulia), katikati ni Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Rufaa ya Kanda Mbeya Dkt. Godlove Mbwanji wakiwa kwenye picha ya pamoja na watumishi wa Mahakama, wadau na Watumishi wa Hospitali ya Rufaa.

Sehemu ya watumishi wa hospitali ya Rufaa Kanda ya Mbeya wakisikiliza elimu inayotolewa.

Sehemu ya watumishi wa hospitali ya Rufaa Kanda ya Mbeya wakisikiliza elimu inayotolewa.

Jaji wa Mahakama Kuu, Kanda ya Mbeya Mhe. Emmanuel Kawishe akiwaeleza jambo watumishi wa hospitali ya Rufaa kanda ya Mbeya.

Jaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Mbeya Mhe. Mussa Kassim Pomo wa (sita kulia) wakiwa kwenye picha ya pamoja na watumishi wa Mahakama na wadau walipotembelea la Gereza la Ruanda mkoani Mbeya, wengine ni Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Mbeya Mhe. Aisha Sinda wa sita kulia kushoto kwake ni Naibu Msajili Mhe. Judith Lyimo wa tano kulia.

Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Mbeya Mhe. Dunstan Ndunguru (wa nne kushoto) na Naibu Msajili Mahakama Kuu Kanda ya Mbeya Mhe. Aziza Temu (wa nne kulia) akiwa kwenye picha ya pamoja na watumishi wa Mahakama na wadau mbalimbali walioshiriki kutoa elimu katika wiki ya sheria mara baada ya kuhitimisha rasmi zoezi la utoaji elimu jana tarehe 30 Januari, 2024 katika viwanja vya kabwe.

 

Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Mbeya Mhe. Dunstan Ndunguru (wa tatu kushoto) na Naibu Msajili Mahakama Kuu Kanda ya Mbeya Mhe. Aziza Temu (katikati) akiwa kwenye picha ya pamoja na watumishi wa Mahakama na wadau mbalimbali walioshiriki kutoa elimu katika wiki ya sheria mara baada ya kuhitimisha rasmi zoezi la utoaji elimu jana tarehe 30 Januari, 2024 katika viwanja vya kabwe.

 


Hakuna maoni:

Chapisha Maoni