Jumatano, 31 Januari 2024

JAJI MKUU AFUNGUA KONGAMANO LA KUJADILI MAKOSA YA UHALIFU WA KIFEDHA

  • Mahakama, Wadau wakutana kujadiliana kwa undani

Na Mary Gwera, Mahakama-Dodoma

Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma leo tarehe 31 Januari, 2024 amefungua Kongamano la Majaji na Wadau ambalo limelenga kujadili makosa ya uhalifu wa kifedha.

Akizungumza wakati akifungua Kongamano hilo leo katika ukumbi wa PSSSF jijini Dodoma, Mhe. Prof. Juma amesema kwamba, kongamano hilo ni sehemu ya maadhimisho ya Wiki ya Sheria na ni sehemu ya Mpango Mkakati wa miaka mitano wa Mahakama ya Tanzania (2020/21-2024/25) ambapo nguzo namba tatu ya Mpango Mkakati huo inatoa nafasi kwa Mahakama kushirikisha wadau katika kutatua changamoto zinazoikumba Sekta ya Sheria na utoaji haki.   

"Huu ni wakati mzuri kwa Majaji wetu ambao muda mwingi wanatumia kusikiliza mashauri mahakamani, kupata maoni mbalimbali na kubadilishana uzoefu kuhusu makosa ya uhalifu wa kifedha na namna ya kukabiliana nayo," amesema Jaji Mkuu.

Ametoa rai kwa Washiriki wa Kongamano hilo, kusikiliza kwa makini yote yatakayojadiliwa na mada zitakazotolewa na wawezeshaji ili kuwa na uelewa zaidi kuhusu makosa ya uhalifu wa kifedha.

“Uhalifu wa kifedha huyumbisha uchumi wa nchi, siasa, utulivu wa kifedha, maisha na riziki. Uhalifu wa kifedha unakiuka na kupuuza mipaka ya kitaifa, na kudhoofisha uchumi wa kimataifa uliounganishwa,” amesema Mhe. Prof. Juma.

Aidha, Jaji Mkuu amewashukuru Washiriki wote waliohudhuria katika kongamano hilo ambapo amesema, “ninyi nyote mnaowakilisha Mashirika yenu hapa mna jukumu la kuzuia na kupambana na uhalifu wa kifedha. Katika kushughulika na uhalifu wa kifedha, mipaka ya ufafanuzi ya uhalifu wa kifedha haipaswi kutufunga.”

Ameongeza kuwa, Uhuru wa Mahakama sio kujitenga na changamoto zinazoikabili Dunia, bali Maafisa Mahakama nchini lazima wafuate ahadi ya Tanzania ya kushughulikia uhalifu wa kifedha. 

Amesema jitihada za Tanzania zinaonekana wazi katika hatua ambayo imechukua tangu mwaka 1999, wakati ikiwa miongoni mwa wanachama waanzilishi wa Kundi la Kupambana na Utakatishaji Fedha Haramu wa Mashariki na Kusini mwa Afrika (ESAAMLG), lililoanzishwa mwaka 1999 jijini Arusha, Tanzania. 

Ameeleza kuwa Tanzania kama mwanachama wa Kikundi cha Kupambana na Utakatishaji wa Pesa katika Nchi za Mashariki na Kusini mwa Afrika, inakubali Kikosi Kazi cha Kifedha kutathmini ufanisi wa hatua za Nchi dhidi ya utakatishaji fedha mara kwa mara, na hatua ambazo inachukua ili kudhibiti mianya inayoweza kuwezesha ufadhili wa ugaidi. 

“Mahakama haiwezi kukwepa tathmini hiyo. Mahakama ya Tanzania ina jukumu muhimu katika kuimarisha ufanisi wa Mapambano ya Kupambana na Utakatishaji wa Fedha na Kukabiliana na Ufadhili wa tawala za Ugaidi,” amesisitiza Jaji Mkuu.

Katika kongamano hili, pamoja na mambo mengine, washiriki wamejadiliana na kubadilishana uzoefu katika masuala mbalimbali yanayohusiana na vyanzo na athari za makosa ya uhalifu wa kifedha pamoja na njia za jinsi ya kukabili na uhalifu huo ambao unazikumba nchi nyingi barani Afrika na Dunia kwa ujumla.

Kongamano hilo limeandaliwa na Mahakama ya Tanzania kupitia Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA) kwa ufadhili wa Programu ya Kitaifa ya Kuzijengea Uwezo Taasisi za Umma Tanzania zinazohusika na kuzuia na kupambana na Rushwa (BSAAT).

Washiriki wa kongamano hilo ni baadhi ya Majaji wa Mahakama ya Rufani, Mahakama Kuu ya Tanzania, Mahakimu Wakazi wa ngazi mbalimbali pamoja na wadau wengine wa sekta ya sheria na mnyororo wa utoaji haki kutoka ndani na nje ya Tanzania. Aidha, Ufunguzi wa Kongamano hilo umehudhuriwa na Balozi wa Uingereza pamoja na Balozi wa Jumuiya ya Ulaya nchini. 


Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma akifungua Kongamano la Majaji na Wadau  unaojadili makosa ya uhalifu wa kifedha. Kongamano hilo limefanyika leo 31 Januari, 2024 katika ukumbi wa PSSSF jijini Dodoma.     
      Sehemu ya Majaji wa Mahakama ya Rufani wakiwa kwenye Kongamano linalojadili makosa ya uhalifu wa kifedha. Katikati ni Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Mhe. Jacobs Mwambegele.
Jaji Kiongozi Mahakama Kuu ya Tanzania (wa tatu kushoto), Mhe. Mustapher Siyani pamoja na Majaji wengine wa Mahakama hiyo wakiwa katika Kongamano la Majaji na Wadau linalojadili makosa ya uhalifu wa kifedha.
Sehemu ya Wadau wakiwa katika Kongamano la kujadili makosa ya uhalifu wa kifedha.
Mtendaji Mkuu Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel (kushoto) pamoja na Kaimu Msajili Mkuu Mahakama ya Tanzania, Mhe. Sylvester Kainda wakiwa katika Kongamano la kujadili makosa ya uhalifu wa kifedha.
Majaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania pamoja na Wadau wengine wakifuatilia kinachojiri.
Mkuu wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama na Jaji wa Mahakama ya Rufani (T), Mhe. Dkt. Paul Kihwelo akizungumza jambo wakati ya hafla ya ufunguzi wa Kongamano la 
kujadili makosa ya uhalifu wa kifedha.
Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma (kushoto) akimkabidhi zawadi ya picha Balozi wa Uingereza nchini Tanzania, Balozi David Concar.
Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma na meza kuu wakiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya Majaji wa Mahakama ya Rufani. 
Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma na meza kuu wakiwa katika picha ya pamoja na sehemu ya Majaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania walioshiriki katika Kongamano la kujadili makosa ya uhalifu wa kifedha.

                            

                                                                    


Hakuna maoni:

Chapisha Maoni