Jumatano, 31 Januari 2024

‘TUSIWAFUNGIE NDANI WATOTO WENYE UHITAJI MAALUM’

Na Hasani Haufi- Mahakama Kuu Songea

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Songea, Mhe. James Karayemaha ametoa wito kwa wazazi na walezi kuacha kuwafungia majumbani watoto wenye uhitaji maalum.

Amesema vitenxdio hivyo siyo vya kiungwana kwa kuwa watoto hao kwani wana haki kama watoto wengine.

Jaji Karayemaha aliyazungumza hayo alipotembelea Shule ya Msingi Jumuishi ya Luhira iliyopo Manispaa ya Songea, ikiwa ni moja ya utekelezaji wa maadhimisho ya Wiki ya Sheria nchini.

Katika ziara hiyo, Jaji Mfawidhi aliambatana na wadau kutoka Ofisi ya TAKUKURU, Jeshi la Polisi, Jeshi la Zimamoto, Uhamiaji, Jeshi la Magereza, Ofisi ya Ustawi wa Jamii, Jeshi la Wananchi Tanzania, Ofisi ya Taifa ya Mashtaka Mkoa wa Ruvuma.

Wengine ni Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali Songea, Ofisi ya Usimamizi wa Wanyama Pori Tanzania, Ofisi ya Uhifadhi wa Misitu (Tfs-Ruvuma), Ofisi ya Uangalizi, pamoja na wadau wengine ambao Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Songea wanashirikiana nao kwa ukaribu.

Wadau hao walikabidhi mahitaji muhimu ya kijamii ikiwemo, unga wa ngano, unga wa mahindi, sukari, sabuni, vyandarua vyenye dawa, mchele, mafuta ya kupikia, mafuta ya kupaka, vifaa vya usafi, kandambili, madaftari madogo na makubwa, karamu za wino pamoja na karamu za risasi.

 Mhe. Karayemaha alisema watoto hao wanahitaji malezi bora tena ya ukaribu. “Kupitia ziara hii nimejifunza na kugundua kuwa kazi ninayofanya ya kusikiliza mashauri na utoaji wa hukumu ni kazi rahisi sana kuliko mnayoifanya Walimu wa watoto hawa, mnastahili pongezi kubwa, msichoke na muendelee na moyo huo,” alisema.

Walimu na wanafunzi hao walitoa shukrani kwa kuwatembelea na kugusa maeneo ambayo yalikuwa yanauhitaji mkubwa, hivyo ujio wao umerejeshea faraja kwani wamekuwa wakipata msaada kila mwaka katika kipindi cha maadhimisho ya Wiki ya Sheria nchini.

“Mmekuwa mkitukumbuka kila mwaka katika kipindi hiki na kutuokoa katika sehemu ambazo tumekuwa tunakosa msaada, hivyo ujio wenu umeleta faraja sana kwetu, ingawa mnaona mahitaji mliyoleta ni madogo, lakini kwetu ni makubwa sana,” mmoja wa walimu hao alisema. 



Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Songea, Mhe. James Karayemaha (wa kwanza kushoto waliosimama) akikabidhi mahitaji kwa wanafunzi wenye mahitaji maaluum wa Shule ya Msingi Luhira.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Songea, Mhe. James Karayemaha (aliyevaa tai waliokaa chini) akiwa kwenye picha ya pamoja na Walimu na wadau wa Mahakama.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Songea, Mhe. James Karayemaha (wa tatu kutoka kushoto na kulia waliokaa kwenye viti) akiwa kwenye picha ya pamoja na Walimu wa Shule Jumuishi Luhila.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Songea, Mhe. James Karayemaha akiwa kwenye picha ya pamoja na watoto wa Shule wenye mahitaji maalum pamoja na Walimu na wadau.

(Habari hii imehaririwa na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Dodoma)

 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni