Jumanne, 23 Januari 2024

BONANZA LA MAHAKAMA LAFANA MKOANI IRINGA

Na LUSAKO MWANG’ONDA-Mahakama Kuu, Iringa

Bonanza la michezo mbalimbali lililoandaliwa na Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Iringa,limefanyika kwa mafanikio makubwa huku mamia ya wananchi wa Manispaa ya Iringa na vitongoji vyake wakiwa wamehudhuria. 

Katika Bonanza hilo, kulikuwepo na michezo mbalimbali iliyofanyika kama mpira wa miguu, mpira wa pete, mpira wa wavu, kuvuta Kamba, kukimbiza kuku, kukimbia kwenye magunia, mashindano ya kula na michezo mingine ambayo iliandaliwa kwa ajili ya ukaribisho wa Wiki ya Sheria kwa mwaka 2024 itakayofunguliwa tarehe 24 Januari, 2024.

Bonanza hilo lililopewa jina la “Bonanza la Mahakama” lilishirikisha watumishi wa Taasisi mbalimbali za Umma, ikiwemo Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Manispaa ya Iringa, Mamlaka ya Mapato Tanzania, pamoja na wadau mbalimbali wa haki, ikiwa ni pamoja na Polisi, Chama cha Wanasheria Iringa, Magereza, Takukuru. 

Kabla ya kufanyika kwa Bonanza, kulikuwa na a Mbio za Ridhaa (Fun Run) ambazo zilianzia katika Viwanja vya Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Iringa kupitia maeneo mbalimbali ya Manispaa ya Iringa na kwenda kutamatika katika Viwanja vya Chuo Kikuu cha Mkwawa ambako michezo mbalimbali ndiko ilikofanyikia.

Akiongea katika Bonanza hilo, Mgeni rasmi ambaye ni Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Iringa, Mhe. Ilvin Mugeta amewapongeza watu wote kwa kuitia mwaliko wa Mahakama kwa kuhudhuria na kwa wingi. 

Jaji Mugeta aliwaomba watu wote waliohudhuria kushiriki pia katika matembezi maalumu ya Ufunguzi wa Wiki ya Sheria ambayo yatafanyika kesho tarehe 24 Januari, 2024.  

Ndugu zangu, nawashukuru sana kwa kutuunga mkono katika Bonanza hili, lakini niwaombe tena kuwa kwa uwingi huu huu mtuunge mkono hapo Jumatano tutakapokuwa na matembezi maalumu ya ufunguzi wa Wiki ya Sheria nchini, alisema.

Naye, Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Mhe. Halima Dendego, ambaye alikuwa ni mgeni maalumu ameushukuru uongozi wa Mahakama Kanda ya Iringa kwa kubuni Bonanza hilo.

Alisisitiza umuhimu wa mabonanza kama hayo kufanyika kwa kuwa yanaiweka Mahakama kuwa karibu na wananchi. Amewataka wananchi wa Iringa kuitumia vyema Wiki ya Sheria kujifunza mambo mbalimbali ya kisheria.


Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Iringa, Mhe. Ilvin Mugeta akizungumza na washiriki wa Bonanza hilo baada ya kushiriki kwenye mbio maalum zilizokuwa zimeandaliwa na Mahakam ana kushirikisha wananchi.

Mgeni maalumu ambaye ni Mkuu wa Mkoa awa Iringa Mhe. Halima Dendego akizungumza na umati wa watu uliojitokeza kushiriki Bonanza hilo.

Watumishi wa Mahakama pamoja na wadau wengine wa haki wakikatiza mitaa mbalimbali ya Manispaa ya Iringa katika mbio za ridhaa (fun run). Anayeonekana pichani upande wa kushoto (mwenye miwani) ni Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Iringa Mhe. Ilvin Mugeta.

 

Watumishi na wadau mbalimbali wakifanya mazoezi ya viungo kwenye Viwanja wa Chuo Kikuu cha Mkwawa baada ya  mbio ndefu za zaidi ya kilomita tano.

 

 


 Timu ya Kamba ya Wanawake wa Mahakama Kanda ya Iringa ikiwa kwenye “shughuli” yao.


 

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Iringa, Mhe. Ilvin Mugeta (wa mbele) akiwa ameongozana na Naibu Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Iringa, Mhe. Maximillian Malewo (wa nyuma) kukagua Timu za Mpira wa Miguu wakati wa ufunguzi wa michezo katika Bonanza hilo.


 

Kikosi cha wachezaji wa Timu ya Mpira wa Miguu ya Mahakama ya Tanzania Kanda ya Iringa kilichocheza kwenye Bonanza hilo.

(Habari hii imehaririwa na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Dodoma)

 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni