Jumanne, 23 Januari 2024

JAJI MKUU AWATAKA WATUMISHI WA MAHAKAMA KUACHA ALAMA WAKATI WA UTUMISHI WAO

 

Na Tiganya Vincent-Mahakama -Dar es Salaam.

 

Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma amewataka Maafisa wa Mahakama ,Viongozi na Watumishi wa Mahakama kuhakikisha wanapotekeleza majukumu yao wanaacha alama katika utumishi wao ambao haitasahaulika kwa wananchi.

 

Ametoa kauli hiyo leo tarehe 23 Januari 2024 wakati wa sherehe katika hafla ya uzinduzi wa Kitabu cha Wasifu na Maisha ya Marehemu Jaji wa Rufani Robert Habesh Kisanga iliyofanyika jijini Dar es Salaam.

Marehemu Jaji Robert Habesh Kisanga aliacha alama isiyofutika zaidi ykwenye mchango whaki.


 Wanadamu wa Kale huko Ngorongoro, waliotembea kwenye tope na majivu ya volcano yaliyokuwa hayajakauka zimetupa viashiria vya namna walivyoishi. Wanadamu wa leo wanaacha historia ya kesho, kupitia maandishi,”alisema Jaji Mkuu.


Mhe. Prof. Juma alisema Marehemu Jaji Robert Habesh Kisanga aliacha alama yenye wino usiofutika katika Katiba ya Tanzania hususan mchango wake katika mabadiliko ya Kumi na Tatu na Kumi na Nne Katika Katiba ya Jamhuri ya Muungano ya Tanzania Wa Mwaka 2004.


Msingi wa mapendekezo ya mabadiliko haya ya 14 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ilikuwa ni kuendelea kutekeleza maoni ya wananchi yaliyoratibiwa na Kamati ya Jaji Robert Kisanga, iliyokusanya maoni kuhusu hoja 19 kupitia Waraka wa Serikali namba 1 wa mwaka 1998 yaani White Paper,” aliongeza Jaji Mkuu


Alisema moja ya alama kubwa zilizoletwa na na Jaji Kisanga kupitia Mabadiliko ya Kumi na Tatu ya Katiba ni kuanzishwa kwa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (The Commission of Human Rights and Good Governance), ambayo ilianzishwa chini ya Ibara ya 129. 


Mhe. Prof. Juma aliongeza kuwa Jaji Kisanga aliacha alama nyingine mara baada Mhe. Rais  wa Awamu ya Tatu Marehemu Benjamin William Mkapa kumteua, Mwaka 2002 kuanzisha Taasisi mpya nchini , kama Mwenyekiti wa kwanza wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora. 


Katika hatua nyingine Jaji Mkuu amekishukuru Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto(IJA) kwa kushirikiana na familia ya Marehemu Jaji Kisanga kwa kukusanya na kuandika wasifu na historia yake ambao itatoa mchango mkubwa katika maendeloeo ya sekta ya sheria nchini.


Aidha Mhe. Prof. Juma amekitaka Chuo hicho kuendeleza utamaduni wa kuandika katika vitabu, alama za historia, zisizofutika ambazo Majaji na Watumishi wengine wa Mhimili wa Mahakama wameacha. 

Kwa upandewa Mkuu wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto(IJA) Mhe. Dkt. Paul Kihwelo alisema Kitabu hicho ni muhimu kwa Wanasheria, Wanachuo wanaosomea fani ya Sheria na watu ambao wanaopendwa kujua masuala mbalimbali ya kisheria.


Alisema katika kuhakikisha kinawanufaisha watu wengi wanatarajia kutoa nakala kwa kila Taasisi ya Elimu inayotoa fani ya Sheria na kuongeza kuwa kwa mdau yoyote ambaye angependa mawazo ya Marehemu Jaji Kisanga yawafikie watu wengi wanaweza kuchangia kwa kununua nakala moja kwa kiwango cha shilingi 52,500.00 kwa fedha za Kitanzania.


Marehemu Jaji Robert Habesh Kisanga alifariki dunia tarehe 23 Januari 2018 na kuzikwa mkoani Kilimanjaro.


Jaji Mkuu wa Tanzania,Mhe.Prof. Ibrahim Hamis Juma (kulia) akizindua Kitabu cha Maisha Ndoto ya Marehemu Mhe. Jaji Robert Habesh Kisanga.


Jaji Mkuu wa Tanzania,Mhe.Prof. Ibrahim Hamis Juma (kushoto) akimkabidhi kitabu hicho Waziri Mkuu Mstaafu,Mhe.Joseph  Warioba.


Jaji Mkuu wa Tanzania,Mhe.Prof. Ibrahim Hamis Juma (kushoto) akimkabidhi Jaji Mkuu wa Zanzibar, Khamis Ramadhan Abdallah.


Jaji Mkuu wa Tanzania,Mhe.Prof. Ibrahim Hamis Juma (kushoto) akimkabidhi kitabu hicho Jaji Mkuu Mstaafu Mhe.Barnabas Samatta kitabu hicho.



Jaji Mkuu wa Tanzania,Prof. Ibrahim Hamis Juma (kushoto) akimkabidhi Mwanazuoni Prof. Issa Shivji.


Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania,Mhe. Mustapher Mohamed  Siyani (wa kwanza kushoto) akiwa na baadhi ya Majaji wa Mahakama ya Rufani na Mahakama Kuu ya Tanzania, wakiwemo wageni waalikwa wakifuatilia tukio hilo.


Jaji Mstaafu wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Fauz Twaib akitoa maelezo ya uandishi wa kitabu hicho.


Mkuu wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto(IJA), Mhe.Dkt. Paul Kihwelo,ambaye pia ni Jaji wa Mahakama ya Rufani Tanzania akitoa neno la utangulizi kuhusu kitabu hicho.




 


 



 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni