· Maandalizi Wiki ya Sheria yakamilika
· Wananchi waalikwa kushiriki
Na Mwandishi wetu-Mahakama Dodoma
Maandalizi kuelekea maadhimisho ya Wiki ya Sheria kwa mwaka 2024 ambayo yatahusisha maonesho na utoaji wa elimu ya kisheria bure kutoka kwa wadau mbalimbali wa Mahakama ya Tanzania yemekamilika.
Kutoka Makao Makuu Dodoma, FAUSTINE KAPAMA anaripoti kuwa uandaaji wa mabanda katika Viwanja vya Nyerere Square kutakapofanyikia kitaifa maadhimisho hayo umekamilika na watumishi wapo tayari kuanza kuwahudumia wananchi kuanzia kesho tarehe 24 Januari, 2024.
Katibu wa Kamati maalumu iliyoundwa na Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel kuratibu shughuli hizo, Mhe. Charles Magesa amesema wameshakamilisha maandalizi yote.
“Kazi imekamilika. Tupo tayari kwa maonesho, tupo tayari kutoa elimu ya kisheria kwa wananchi wetu. Wadau wote wanaoshiriki kwenye maonesho kama unavyoona mabanda yao wameshafika kwa ajili ya shughuli hii,” amesema.
Mhe. Magesa amewaalika wananchi wote kufika katika Viwanja vya Nyerere Square na kutembelea mabanda ambayo yameandaliwa na wadau wa Mahakama ili kujionea shughuli wanazofanya na kupata elimu kwenye maeneo mbalimbali ya kisheria.
Elimu itakayotolewa inahusu taratibu za ufunguaji wa mashauri hasa kwa njia ya mtandao, sheria na taratibu zinazotumika katika kuendesha mashauri mbalimbali kama yale ya Ndoa na Talaka, Ardhi, migogoro ya Kazi pamoja na utekelezaji wa hukumu, Sheria za Watoto na taratibu za mashauri ya mirathi.
Vilevile wanananchi watapata fursa ya kujifunza huduma zitolewazo na Mahakama inayotembea “Mobile Court” na Mahakama za Vituo Jumuishi, watajifunza jinsi Mahakama ya Tanzania imejipanga kutoa haki katika Karne ya 21 kwa kutumia matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA).
Sambamba na Elimu ya Sheria na maonesho yatakayofanyika Kitaifa katika Mji Mkuu wa Tanzania, Dodoma, utoaji wa elimu ya sheria kwa umma na maonesho utaendelea pia katika Kanda za Mahakama Kuu, Mikoa na Wilaya nchi nzima kama ilivyofanyika kwa miaka mingine.
Kwa mwaka huu, katika maadhimisho haya ya Wiki ya Sheria na Siku ya Sheria, kauli mbiu inasema, "Umuhimu wa Dhana ya Haki kwa Ustawi wa Taifa: Nafasi ya Mahakama na Wadau katika Kuboresha Mfumo Jumuishi wa Haki Jinai."
Kutoka Mwanza, Stephen Kapiga anaripoti kuwa kuelekea Wiki na Siku ya Sheria Nchini, Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Mwanza, Dkt. Ntemi Kilekamajenga amefanya kikao cha pamoja na watumishi wote wa Mahakama zilizopo Mjini Mwanza kwa lengo la kuona namna bora itakayowawezesha kushiriki katika maadhimisho hayo.
Mhe Dkt. Kilekamajenga aliwahimiza Mahakimu wa Mahakama za Mwanzo zilizopo Mwanza Mjini kushiriki kikamilifu na kuhakikisha ratiba yao ya mashauri kutokuwa kikwazo kwao au wasaidizi wao wa kumbukumbu.
Wakati huo huo, mipango imefanywa kwa ajili ya kuwafikia waendesha bodaboda wote waliopo Mwanza Mjini kwa kushirikiana na Viongozi wa vyama vyao ili waweze kupewa elimu ya sheria inayohusu mikataba ya kazi, usalama barabarani, usafirishaji wa abiria na bima ya vyombo vya moto ili kuwasaidia ambao wengi wao wamekuwa wakikumbana na changamoto wakati wa ufanyaji kazi zao.
Taarifa kutoka kwa Eunice Lugiana wa Mahakama Pwani zinaeleza kuwa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kibaha Pwani imekamilisha maandalizi kuelekea Wiki ya Sheria nchini. Katika maandalizi hayo watumishi wameonekana kuwa katika pilika pilika za hapa na pale ili kuweka mambo sawa sawia.
Akiongea wakati wa maandalizi hayo, Afisa Tawala wa Mahakama ya Hakimu Mkazi, Bi. Stumai Hozza amesema “maandalizi yote ya msingi yako tayari na watumishi wamejiandaa vyema kuwahudumia wananchi kwa kutoa elimu.”
Baadhi ya watumishi walioongea na Mwandishi wa Habari hizi wamesema wako tayari kuwahudumia wananchi kuelekea Wiki ya Sheria.
“Maandalizi ni mazuri tuko tayari kuwasikiliza wananchi na kutoa huduma bora, tunawakaribisha wananchi wote waje kupata huduma,”alisema Msaidizi wa Ofisi, Bi Nuru Moto wakati akifanya usafi katika mazingira ya Mahakama hiyo.
Maandalizi ya Wiki na Siku ya Sheria katika Mahakama ya Hakimu Mkazi yameanza mapema huku wadau na wananchi, Viongozi wa Dini, Viongozi wa Vyama vya Siasa na Ofisi za Serikali tayari wameshapatowa mialiko.
Katika Mkoa wa Pwani, zoezi la utoaji elimu litafanyika pia mashuleni, ofisi za watendaji wa kata na vijiji, hasa Soga, Ruvu na Magindu ambapo wananchi wa maeneo hayo wanatamani siku hii ifike maana wamepata utatuzi wa masuala yao kupitia Wiki ya Sheria iliyofanyika mwaka jana 2023.
Naye Na Hasani Haufi wa Mahakama Kuu Songea anaripoti kuwa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Songea imejiandaa kikamilifu katika kipindi chote cha Wiki ya Sheria nchini katika utoaji wa elimu mbalimbali kwa wananchi wa Mkoa wa Ruvuma ikiwa ni sehemu ya kuongeza uelewa wa sheria kwa wananchi wa kawaida.
Aidha Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Songea imearika Taasisi mbalimbali za kiserikali kama wadau wa Mahakama katika kuhakikisha elimu kwa wanachi inawafikia.
Zoezi la utoaji elimu litafanyika katika mabanda mbayo yamendaliwa kwenye Viwanja vya Soko Kuu Songea, Shule ya Sekondari ya Wavulana, Shule ya Sekondari Ruvuma, Shule ya Msingi Mfaranyaki na Jeshini Chandamali.
Kutoka Shinyanga, Mwandishi wetu Emmanuel Oguda anaripoti kuwa Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Shinyanga, Mhe. Frank Mahimbali amewahimiza wananchi kujitokeza kwa wingi katika maeneo yaliyoandaliwa kwa ajili ya elimu ya sheria katika kipindi hiki cha maadhimisho ya Wiki ya Sheria.
Mhe. Mahimbali ametoa rai hiyo wakati akiongea na Waandishi wa Habari kutoka vyombo mbalimbali ofisini kwake na kusisitiza wadau na wananchi wote kujitokeza kwa wingi katika maadhimisho hayo.
Amesema kutakuwepo pia na wadau watakaoungana nao katika zoezi hilo kwenye maeneo mbalimbali yenye mikusanyiko ya watu, mfano minadani, sokoni, shuleni na vyuoni, lengo ni kuhakikisha elimu ya sheria inawafikia wananchi wote hasa maeneo ya Shinyanga na Simiyu ambapo mashauri ya migogoro ya ardhi na mauaji yamekithiri.
Aidha, Mhe. Mahimbali amesema kuwa, katika maadhimisho ya Wiki ya Sheria, malalamiko, maoni na mapendekezo ya namna ya kuboresha huduma za Mahakama yatapokelewa katika maeneo mbalimbali yaliyoainishwa.
Mwandishi wetu kutoka Mahakama Mbeya, Mwinga Mpoli anaripoti kuwa katika kuelekea maadhimisho ya Wiki ya Sheria na kilele cha Siku ya Sheria nchini, Mahakama Kuu Kanda ya Mbeya imeungana na Mahakama ya Tanzania kwa ujumla katika kuhakikisha maadhimisho hayo yanakuwa yenye mafanikio.
Haya yameonekana kutokana na maandilizi ya Wiki ya Sheria ambapo kwa Mahakama Kuu Mbeya, Majaji, Mahakimu, watumishi na wadau mbalimbali wameonekana kuwa na mwamko mkubwa wa kushiriki kikamilifu katika maadhimisho hayo.
Akiongea wakati wa maandalizi hayo, Naibu Msajili Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Mbeya, Mhe. Aziza Temu ameeleza kuwa hakika utakuwa mwaka wa kukumbukwa kwa maandalizi mazuri ambayo tayari yameshafanyika na watumishi na wadau wapo tayari kuwahudumia wananchi.
“Maandalizi yote ya msingi yako tayari, watumishi pamoja na wadau wote wa Mahakama tumejiandaa na tupo tayari kuwahudumia wananchi,” alisema Mhe. Temu
Aidha, watumishi wa Mahakama nao hawakuwa nyuma kuelezea jinsi walivyojipanga kuwasikiliza wananchi na kuahidi kutoa huduma iliyo bora.
Kwa Mkoa wa Mbeya, utoaji wa elimu wakati wa Wiki ya Sheria utafanyika katika Viwanja vya Kabwe, mashuleni, katika taasisi kadhaa, Magereza na stesheni za radio mbalimbali.
Hakimu Mkazi Mfawidhi Mahakama ya Hakimu Mkazi Singida, Mhe.Allu Nzowa, Mtendaji wa Mahakama, Bw. Yusuph Kasuka na Afisa Utumishi. Bi Eva Leshange walifanya ziara katika Wilaya za Iramba, Singida na Manyoni kujionea maandalizi yanavyoendelea na kutoa mapendekezo.
Aidha Mkoa umejipanga vyema kuhakikisha elimu inatolewa ipasavyo ambapo maeneo yaliyolengwa na wadau kutoa elimu ni katika viwanja vya Mahakama, Shule za Sekondari na Shule za Msingi, vyuoni , sokoni na redioni.
Sambamba na hilo, kamati ya elimu imeaandaa ratiba elekezi ya utoaji elimu, wahusika na mahali pakutoa elimu. Vile vile wadau na watumishi wamejipanga kushiriki kikamilifu katika maadhimisho hayo.
Wakati huo huo, Mwandishi Wetu James Kapele- Mahakama ya Hakimu Mkazi Katavi anaeleza kuwa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Sumbawanga imefanya ziara ya kikazi mwisho wa wiki mkoani Katavi kujionea namna maandalizi ya Wiki ya Sheria yanavyofanyika.
Ziara hiyo iliongozwa na Kaimu Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Sumbawanga Mhe, Abubakar Mrisha.
Akiongea na Viongozi wa Mahakama Mkoa wa Katavi katika Ofisi ya Hakimu Mkazi Mfawidhi, Mhe. Mrisha alielezea kuridhishwa na maandalizi yanavyokwenda na kushauri wadau wa haki kushirikishwa ili kuwafikia wananchi wengi katika elimu ya masuala mbalimbali ya kisheria na huduma mbalimbali zinazotolewa na Mahakama
“Nimefurahishwa sana na maandalizi yenu kuelekekea maadhimisho haya, naomba sana mjitahidi kuwashirikisha kwa wingi wadau wengine hata kwenye vikao vyenu ili maadhimisho haya yawafikie wananchi wengi zaidi,” alisema Jaji Mrisha.
Mhe. Mtulya ametoa rai hiyo kupitia kikao cha watumishi pamoja na wadau wa Mahakama watakaoshiriki katika zoezi la utoaji wa elimu.
Kupitia kikao hicho, Jaji Mfawidhi aliwaasa watumishi wa Mahakama na wadau watakaoshiriki katika zoezi zima la utoaji wa elimu kujitoa kikamilifu ili mwananchi atakayefika kutafuta elimu mbalimbali za kisheria au msaada wa kisheria, apate huduma anayohitaji bure na kusaidiwa kwa haki kama ilivyokusudiwa.
Kikao hicho kimebainisha mpango wa utoaji elimu ambapo maonesho ya Wiki ya Sheria katika Kanda ya Musoma yatafanyika kupitia viwanja vya Shule ya Msingi Mukendo, stendi ya zamani Bunda, viwanja vya Mahakama ya Wilaya Tarime, viwanja vya Mahakama ya Wilaya Serengeti, viwanja vya Mahakama ya Wilaya Rorya, Butiama, taasisi za elimu, magereza, redio mbalimbali na maeneo mbalimbali ya masoko.
Maandalizi kwa ajili ya maonesho ya Wiki ya Sheria yakiendelea katika viwanja vya Shule ya Msingi Mukendo Musoma Mjini ambako elimu ya masuala mbalimbali ya kisheria itatolewa.
Katika maonesho hayo, elimu hiyo itatolewa na Majaji, Wasajili, Naibu Wasajili, Mahakimu pamoja na wadau wa Mahakama, wakiwemo Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali, Ofisi ya Taifa ya Mashtaka, Ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali, Tume ya Haki za Binadamu, Chama cha Majaji na Mahakimu Wanawake (TAWJA), Polisi, Magereza na Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS).
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni