Jumatano, 24 Januari 2024

JAJI MFAWIDHI TABORA AWAITA WANANCHI KWENYE MAADHIMISHO YA WIKI, SIKU YA SHERIA

Na Amani Mtinangi- Mahakama Kuu Kanda, Tabora.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Tabora, Mhe.  Dkt. Adam Mambi amefanya kikao na Waandishi wa Habari kuelezea maandalizi ya Wiki na Siku ya Sheria. 

Kikao hicho kilichofanyika katika Ofisi yake iliyopo Mahakama Kuu Tabora kilihudhuriwa na Waandishi wa Habari kutoka vyombo mbalimbali, ikiwemo Televisheni, Redio na vinavyotumia mitandao ya kijamii (social media platforms).

Aliwaasa kutumia vyombo vyao kuhabarisha Umma kuhusu wiki hiyo. Mhe. Dkt. Mambi aliwaeleza kuwa maadhimisho ya Wiki na Siku ya Sheria mwaka huu yatakuwa ni ya aina yake kwani mipango kabambe inayotekelezeka imewekwa na Mahakama, wadau na Taasisi mbalimbali za Umma.

Jaji Mfawidhi alisema maandalizi yote muhimu yamekamiliika ikiwemo uwekaji wa mabanda ya maonesho, matembezi, Bonanza la Michezo, utoaji wa huduma na misaada ya kijamii na elimu kwa Umma imeanza kutolewa ili kuhakikisha kuwa Umma unakuwa na taarifa za kutosha kuhusu uwepo wa maadhimisho hayo.

“Maadhimisho ya mwaka huu katika Mahakama Kuu Kanda ya Tabora yatakuwa ya aina yake, tutafungua maonesho tarehe 24 Januari na tarehe 27 Januari, 2024 tutakuwa na matembezi ya Wiki ya Sheria yatakayofuatiwa na bonanza la michezo litakalofanyika tarehe 28 Januari, 2024 na tarehe 30 Januari, 2024 tutafunga maonesho yetu.

Amesema kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Sheria yatakayofanyika katika Viwanja vya Mahakama Kuu Kanda ya Tabora ambapo Taasisi na Wadau wa Mahakama watashiki, hivyo akawaalika wananchi na Umma wote wa Tabora kushiriki matukio hayo muhimu bila kukosa. 

Maadhimisho ya Wiki na siku ya Sheria Nchini ni sehemu ya utamaduni wa Mahakama ya Tanzania ya kufanya maadhimisho hayo ambapo shughuli mbalimbali hufanyika katika Mahakama zote kuashiria mwanzo wa mwaka wa shughuli za kimahakama.

Kaulimbiu ya maadhimisho kwa mwaka huu 2024 inahusu “UMUHIMU WA DHANA YA HAKI KWA USTAWI WA TAIFA: NAFASI YA MAHAKAMA NA WADAU KATIKA KUBORESHA MFUMO JUMUISHI WA HAKI JINAI.”

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Tabora, Mhe. Dkt. Adam Mambi akizungunza na Waandishi wa Habari.


Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Tabora, Mhe. Dkt. Adam Mambi (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na Naibu Msajili wa Mahakama Kuu Kanda ya Tabora Mhe. Rhoda Ngimilanga (kushoto) na Mtendaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Tabora, Bw. Emmanuel Munda baada ya kikao cha Waandishi wa Habari.
(Habari hii imehaririwa na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Dodoma)

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni