Jumatano, 17 Januari 2024

HAKI MSINGI KATIKA USTAWI WA TAIFA: JAJI MKUU

Na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Dar es Salaam

Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma amezitaka Taasisi zote na wadau katika mfumo wa haki jinai nchini kutafakari na kuendeleza suala la haki ambalo ni la msingi katika ustawi wa Taifa.

Mhe. Prof. Juma ametoa wito huo leo tarehe 17 Januari, 2024 alipokuwa anaongea na Waandishi wa Habari katika Kituo Jumuishi cha Masuala ya Familia Temeka jijini Dar es Salaam kuhusu maadhimisho ya Wiki na Siku ya Sheria kwa mwaka 2024.

Amesema kuwa kauli mbiu itakayoongoza maadhimisho hayo inasema, ““Umuhimu wa Dhana ya Haki kwa Ustawi wa Taifa: Nafasi ya Mahakama na Wadau Katika Kuboresha Mfumo Jumuishi wa Haki Jinai.”

“Kauli mbiu hii, inatoa nafasi nyingine kwa taasisi za Haki Jinai kutafakari maoni ya Mapendekezo ya Tume ya Rais, kuangalia Jinsi ya Kuboresha Taasisi za Haki Jinai. Kauli mbiu inajenga hoja kuwa, hatua, taasisi na ngazi mbalimbali ambazo hupitiwa na mashauri ya jinai lazima zitahmini haki,” amesema.

Akifafanua zaidi kuhusu kauli mbiu hiyo, Jaji Mkuu amebainisha kuwa mchakato wa haki jinai hupitia hatua muhimu mbalimbali ambazo zinahusisha Mahakama na wadau, ikiwemo uchunguzi, upelelezi na kukamatwa kwa washukiwa.

Ametaja hatua zingine kama uendeshaji wa mashtaka unaofanywa na Ofisi ya Taifa ya Mashtaka, Mahakama katika ngazi mbalimbali kusikiliza mashauri na kutoa uamuzi, huku Jeshi la Magereza likihusika na kuhifadhi wafungwa au mahabusu.

Mhe. Prof. Juma amewaambia Waadishi wa Habari kuwa taarifa ya Tume ya Rais, kuangalia jinsi ya kuboresha taasisi za haki jinai ipo katika hatua za utekelezaji wa mapendekezo kwa ujumla na mapendekezo yanayotakiwa katika kila Taasisi ya Haki Jinai.

“Wiki ya Sheria itatumiwa na Taasisi mbalimbali kujieleza kwa wananchi. Moja ya changamoto zilizoanishwa na Tume ya Rais, ni mifumo ya utekelezaji wa majukumu ya Taasisi zinazohusika na Haki Jinai kutosomana, haziwasiliani na kila taasisi inahifadhi taarifa muhimu bila kutoa kwa taasisi zingine. 

“Hali hiyo ya kutosomana, kutogawana taarifa muhimu inaathiri upatikanaji wa haki kwa wakati kwa vile inachelewesha upelelezi, inachelewesha usikilizwaji wa mashauri, bila kusahau kuwa kutogawana na kutosomana huko kunaathiri uendeshaji na usimamizi wa vyombo vingine vya utoaji haki,” amesema.

Jaji Mkuu amesema kuwa kwa mwaka huu 2024, Mahakama ya Tanzania itaadhimisha Wiki na Siku ya Sheria katika ngazi ya Kitaifa jijini Dodoma, katika Kanda za Mahakama Kuu, katika Mikoa na Wilaya zote nchini.

Amesema maadhimisho ya Wiki ya Sheria yataanza tarehe 24 hadi 30 Januari, 2024 kwenye Viwanja vya Mwalimu Nyerere Square katikati ya Jiji la Dodoma. 

Mhe. Prof. Juma amebainisha kuwa uzinduzi rasmi wa maonesho ya Wiki ya Sheria utafanyika tarehe 27 Januari, 2024 kwa matembezi yatakayoanza saa 12.00 asubuhi kwenye Jengo la Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki Dodoma na kuhitimishwa kwenye Viwanja vya Mwalimu Nyerere.

“Mgeni Rasmi atakuwa ni Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na pia Rais wa Umoja wa Mabunge Duniani – Inter-Parliamentary Union, Mhe. Dkt. Tulia Ackson,” amesema. 

Jaji Mkuu ameeleza pia kuwa kilele cha Siku ya Sheria itakuwa ni tarehe 01 Februari, 2024 kwenye viwanja vya Chinangali Jijini Dodoma na Mgeni Rasmi anatarajiwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Mahakama ya Tanzania ina jukumu la kikatiba la kutoa haki ikiongozwa na dira yake ya utoaji haki kwa wakati na kwa watu wote (Timely and Accessible Justice for all). Watu wote hapa ni watanzania zaidi ya milioni 60, waliopo katika Mikoa 26, Wilaya 139, na Kata takriban 4000. 

Katika kutimiza wajibu wake wa kutoa haki katika nchi kubwa, yenye mahitaji makubwa, ni lazima iwepo dira, nguzo, mikakati, malengo na tathmini za mara kwa mara. 

Mahakama imekuwa ikifanya maboresho kwenye huduma zake ili kutoa huduma bora inayomlenga mwananchi kupitia Mpango Mkakati wa Miaka Mitano Awamu ya Pili (2020/21 - 2024/25) ambao umesimikwa katika Nguzo ya Tatu zinazoongoza utekelezaji wa Mpango Mkakati na Programu za Kimaboresho.

Katika Nguzo ya kwanza, Mahakama inatekeleza utawala bora, uwajibikaji na usimamizi wa rasilimali; Nguzo ya Pili ni upatikanaji na utoaji wa haki kwa wakati na Nguzo ya Tatu ni kuthamini mani kutoka kwa wananchi, watumiaji wa huduma za Mahakama, wadau wa na jamii kwa ujumla. 

Nguzo ya tatu ina umuhimu wa kipekee kwa vile inahusu Mahakama ya Tanzania kuwashirikisha wananchi, watumiaji wa huduma za Mahakama, wadau na jamii kwa ujumla, katika shughuli za kimahakama. 

Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma (juu na chiniakisisitiza jambo alipokuwa anaongea na Waandishi wa Habari kuhusu maadhimisho ya Wiki na Siku ya Sheria mwaka 2024.


Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel akitoa maelezo ya utangulizi kabla ya kumkaribisha Jaji Mkuu kuongea na Waandishi wa Habari.

Sehemu ya Viongozi wa  Mahakama ya Tanzania wakiwa katika mkutano huo.

Sehemu ya Viongozi wa Mahakama ya Tanzania na Waandishi wa Habari wakiwa katika mkutano huo.






Hakuna maoni:

Chapisha Maoni