Na Magreth Kinabo -Mahakama
Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) ina nafasi kubwa katika kuboresha na kufanikisha upatikanaji wa haki kwa wakati.
Hayo yamebainishwa na Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe.Prof, Ibrahim Hamis Juma alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari katika Kituo Jumuishi cha Masuala ya Familia Temeke jijini Dar es Salaam kuhusu maonesho ya Wiki ya Sheria na maadhimisho ya Siku ya Sheria ya mwaka 2024.
“Katika Wiki ya Sheria mwaka huu 2024, Mahakama ya Tanzania itatumia kauli mbiu kuonyesha namna Mahakama inavyoendelea kuboresha huduma zake kupitia mifumo ya TEHAMA. Mifumo ya TEHAMA ya Mahakama inalenga kuzifunganisha Taasisi za Haki Jinai kwenye mwavuli mmoja wa mawasiliano ili kuratibu na taarifa sahihi tangu mtuhumiwa anapokamatwa hadi pale kesi inapokamilika mahakamani,”alisema Jaji Mkuu Prof Juma.
Aidha aliongeza kwamba Mahakama inategemea kwamba wananchi na wadau watakaofika kwenye viwanja vya maonesho ya Kitaifa Jijini Dododma watapata maelezo kutoka Kurugenzi ya TEHAMAna Kurugenzi ya Usimamizi wa Mashauri ya namna mifumo mipya ya TEHAMA inavyofanya kazi na wataoneshwa kwa vitendo namna mifumo hiyo inavyofanya kazi.
Mhe. Prof. Juma aliitaja mifumo itakayooneshwa wakati wa maonesho hayo kuwa ni mfumo mpya wa ki-elektroniki wa Kuratibu Uendeshaji na Usimamizi wa Mashauri (Electronic Case Management System—e-CMS), ambao umelenga kutoa huduma zifuatazo ambazo ni usajili wa mashauri (nyaraka za mashauri za pande zilizo na mgogoro) kwa njia ya mtandao na kuyafuatilia mashauri yanavyotiririka katika hatua mbalimbali kwa njia za ki-elektroniki hadi hatua ya uamuzi (Hukumu);
Huduma nyingine itolewayo na mfumo huo ni upangaji wa mashauri kwa Majaji na Mahakimu na Majaji na Mahakimu waliopangiwa mashauri watakuwa na uwezo wa kusoma nyaraka zote za shauri zilizo katika nyaraka laini zinazopatikana kwa njia ya ki-elektroniki. Na watazisoma wakiwa pahali popote.
“Mfumo huu ulianza kazi Novemba mwaka huu, na tayari Jaji Mkuu wa Zimbabwe na Jaji Mkuu wa Uganda wameshatuma watu kujifunza mfumo huu, na kuna majaji wengine wanaotaka kutuma watu ili wajifunze,”alisisitiza Jaji Mkuu.
Aliwaomba wananchi wajitokeze kwa wingi ili kuweza kujifunza kuhusu mfumo huo unavyofanya kazi, ikiwemo kuuliza maswali magumu na kutoa changamoto ambazo zitasaidia kuendelea kuuboresha.
Mfumo huo, hadi sasa umeshafungwa katika Mahakama 11 kikiwemo kituo hicho.
Maadhimisho ya Wiki ya Sheria mwaka yataanza tarehe 24 hadi 30 Januari 2024 kwenye Viwanja vya Mwalimiu Nyerere katikati ya Jiji la Dodoma. Uzinduzi rasmi wa Maonesho ya Wiki ya Sheria utafanyika tarehe 27 Januari 2024 kwa matembezi yatakayoanza saa 12.00 asubuhi kwenye Jengo la Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki Dodoma na kuhitimishwa kwenye Viwanja vya Mwalimu Nyerere na mgeni rasmi atakuwa ni Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Tulia Ackson (Mb), na pia Rais wa Umoja wa Mabunge Duniani – Inter-Parliamentary Union.
Kilele cha Siku ya Sheria itakuwa ni tarehe 01 Februari, 2024 kwenye viwanja vya Chinangali Jijini Dodoma, ambapo mgeni rasmi anatarajiwa kuwa, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe.Prof, Ibrahim Hamis Juma akizungumza na waandishi wa habari katika Kituo Jumuishi cha Masuala ya Familia Temeke jijini Dar es Salaam kuhusu maonesho ya Wiki ya Sheria na maadhimisho ya Siku ya Sheria ya mwaka 2024.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni