Jumatano, 17 Januari 2024

JAJI MKUU AWAALIKA WATANZANIA KUSHIRIKI WIKI YA SHERIA

Na Mary Gwera, Mahakama

Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma amewaalika wananchi wote nchini kutembelea maonesho ya Wiki ya Sheria yanayotarajiwa kuanza tarehe 24 Januari, 2024 ili kujifunza mambo mbalimbali katika muktadha mzima wa utoaji haki.

Mhe. Prof. Juma ametoa wito huo leo tarehe 17 Januari, 2024 katika Ukumbi wa Kituo Jumuishi cha Masuala ya Familia Temeke jijini Dar es Salaam wakati akizungumza na Waandishi wa Habari kuhusu maadhimisho ya Wiki na Siku ya Sheria kwa mwaka huu.

“Napenda kutoa rai kwa wananchi na wadau wote wa Sheria kutembelea sehemu zote zilizoandaliwa kwa ajili maadhimisho ya Wiki ya Sheria kuanzia wilayani, mikoani na Jijini Dodoma ambapo Maonesho yatafanyika kitaifa katika viwanja vya Nyerere ‘Square’ kwa ajili ya kujifunza na kupata huduma mbalimbali za kisheria,” amesema Mhe. Prof. Juma. 

Amesema kwamba, kwa wale waliopo katika Mikoa mbalimbali watembelee mabanda ambayo yataandaliwa na Kanda za Mahakama Kuu, Mahakama za Hakimu Mkazi na zile za Wilaya kwa ajili ya kupata elimu na msaada wa kisheria. 

Jaji Mkuu amesema kwamba, wananchi wana haki ya kupata taarifa za nchi ikiwemo za kimahakama huku akirejea Ibara ya 18 (2) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (1977) ambayo inataja haki ya wananchi kupewa taarifa wakati wote kuhusu matukio mbalimbali nchini na duniani kote ambayo ni muhimu kwa Maisha na shughuli zao, na pia kupata taarifa juu ya masuala muhimu kwa jamii. 

Amebainisha wadau watakaoshiriki katika Maonesho hayo yatakayofanyika hadi tarehe 30 Januari, 2024 ni pamoja na Wizara ya Katiba na Sheria, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali, Ofisi ya Taifa ya Mashtaka, Jeshi la Polisi, Jeshi la Magereza, Mamlaka ya Udhibiti wa Madawa ya Kulevya, Ofisi ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali na wengine. 

Amesema kuwa ni muhimu wananchi na wadau mbalimbali kutembelea maonesho hayo kwa kuwa yatawawezesha kufahamu masuala mbalimbali ya kimahakama ikiwa ni pamoja na Uandishi wa Wosia, Usimamizi wa Mirathi na huduma nyingine. 

“Wananchi watapata fursa ya kuzungumza, kuuliza maswali na kujadiliana na Maafisa wa Mahakama na wadau wake kwa lengo la kujifunza kuhusu huduma mbalimbali zinazotolewa na Mahakama na pia zile zinazotolewa na wadau wake,” ameeleza Jaji Mkuu. 

Mhe. Prof. Juma amebainisha kuwa Kaulimbiu ya Wiki na Siku ya Sheria ya mwaka huu ni “Umuhimu wa Dhana ya Haki kwa Ustawi wa Taifa: Nafasi ya Mahakama na Wadau Katika Kuboresha Mfumo Jumuishi wa Haki Jinai.”

Kwa mujibu wa Jaji Mkuu, Maonesho hayo yatazinduliwa rasmi tarehe 27 Januari, 2024 kwa matembezi maalum ambayo yataongozwa na Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambaye pia ni Rais wa Umoja wa Mabunge Duniani (IPU), Mhe. Dkt. Tulia Ackson.

“Maonesho haya yatazinduliwa kwa matembezi maalum yatakayofanyika tarehe 27 Januari, 2024 kuanzia Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki-Dodoma hadi Viwanja vya Nyerere ‘Square’ jijini humo, matembezi haya yataongozwa na Spika wa Bunge la Tanzania, Mhe. Dkt. Tulia Ackson,” amesema.

Kadhalika, Jaji Mkuu amesema kwamba, kilele cha Maonesho ya Wiki ya Sheria kitafanyika tarehe Mosi, Februari 2024 katika Viwanja vya Chinangali jijini Dodoma ambapo Mgeni Rasmi anatarajiwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.

 Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma akizungumza na Waandishi wa Habari (hawapo katika picha) leo tarehe 17 Januari, 2024 kuhusu Maadhimisho ya Wiki na Siku ya Sheria, 2024.
 Sehemu ya Waandishi wa Habari pamoja na Maafisa wa Mahakama wakimsikiliza Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma (hayupo katika picha) alipokuwa akizungumza na Wanahabari leo tarehe 17 Januari, 2024 katika Ukumbi wa Mikutano wa Kituo Jumuishi cha Masuala ya Familia-Temeke.
Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma (katikati) akizungumza na Wanahabari. Kushoto ni Jaji Mfawishi Mahakama Kuu Kituo Jumuishi cha Masuala ya Familia-Temeke, Mhe. Mwanabaraka Mnyukwa na kulia ni Mtendaji Mkuu Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel.
Sehemu ya Viongozi na Maafisa wa Mahakama walioshiriki katika Mkutano kati ya Jaji Mkuu na Waandishi wa Habari. Kutoka kulia ni Kaimu Msajili Mkuu, Mahakama ya Tanzania ambaye pia ni Msajili Mahakama ya Rufani, Mhe. Sylivester Kainda, Naibu Msajili Mwandamizi Mahakama ya Rufani, Mhe. Emmanuel Mrangu, Naibu Msajili Mahakama ya Rufani, Mhe. Charles Magesa na Naibu Msajili Mahakama ya Rufani, Mhe. Joseph Fovo.


Hakuna maoni:

Chapisha Maoni