Na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Dar es Salaam
Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma ameshauri sheria zinazohusika katika mchakato wa utoaji haki nchini kufanyiwa marekebisho makubwa ili kuondoa konakona zinazochangia ucheleweshaji wa kumaliza mashauri.
Mhe. Prof. Juma ametoa ushauri huo katika hafla ya kukabidhi tuzo kwa wadau mbalimbali wa usuluhishi iliyokuwa imeandaliwa na Mahakama Kuu ya Tanzania Kituo cha Usuluhishi katika Ukumbi wa Kimataifa wa Mwalimu Nyerere jijini Dar es Salaam.
“Kuna tatizo kubwa sana katika mfumo wetu wa sheria, kuna michakato mingi, kuna konakona nyingi na kwa bahati mbaya, taaluma yetu ya sheria imejengwa kwa kutegemea hizo konakona,” amesema.
Ameeleza kuwa moja ya maboresho ambayo ni muhimu katika karne ya 21 ni usuluhishi na maboresho hayo yanatokana na ukweli kwamba taratibu za kimahakama pamoja na sheria, zikiwemo zile za mienendo ya madai na jinai, zilitungwa katika maudhui ya karne ya 18 au 19.
“Ndiyo maana kuna wakati mmoja, Profesa kutoka Marekani alikuja nchini na aliposoma sheria yetu ya mienendo ya madai, aliposoma sheria ya mienendo ya jinai, aliposoma sheria ya ushahidi aliandika andiko na kusema zote ni za kizamani,” Jaji Mkuu ameeleza.
Katika andiko lake, Profesa huyo alibaisha sheria alizopitia zina konakona nyingi ambazo zinaweka fursa za mapingamizi na kuruhusu mdaawa kurudi mahakamani hata baada ya shauri kukamilika na kazi kuanza upya.
“Wenzetu Wizara ya Elimu wameangalia upya mfumo wa elimu, mfumo wa elimu ya sheria hatujauangalia na hata marekebisho ya sheria tunayofanya ni vipande vipande, hatuangalii marekebisho kwa ujumla na ndiyo maana kunakuwa na changamoto nyingi sana,” Mhe. Prof. Juma amesema.
Hivyo, Jaji Mkuu akasema kuwa pamoja na kuhimiza wananchi kutatua migogoro kwa njia ya usuluhishi kuna haja pia ya kuangalia upya sheria zote kwani taratibu zilizopo zinaweka nafasi ya mashauri kuchukua zaidi ya miaka mitano au sita.
“Je, kuna haja ya mgogoro wa ardhi uanzie kata, uende baraza la ardhi, uende Mahakama Kuu na Mahakama Kuu kuna mapingamizi mengi, kuna maombi mengi, uende Mahakama ya Rufani, halafu hapo hapo uwe na Nchi ambayo ni shindani katika biashara na uwekezaji.
“Ndiyo maana Mawakili watakwambia hapo ndiyo tunapata chakula chetu, bila hizo konakona hatuwezi kupata kitu. Kwa hiyo, ule ucheleweshaji kwa wengine ni faida inayowapatia kipato, hivyo kuna haja kabisa ya kuangalia upya sheria zetu,” amesema.
Mhe. Prof. Juma alitolea mfano wa Mahakama ya Rufani ambayo imejitahidi kwa kiasi kikubwa kupunguza muda wa shauri kukaa mahakamani na utaratibu uliopo unaonyesha halitakiwi kuzidi miaka miwili tangu liliposajiliwa.
“Kuna baadhi ya wateja wanalalamika kwamba tunaenda kwa kasi sana kwa sababu wanajua wakishakata rufaa Mahakama ya Rufani kila kitu kitasimama na wataendelea kunufaika. Wale ambao kipato chao kinatokana na huo ucheleweshaji hawatapenda haya mageuzi. Kwa hiyo, kuna maeneo mengi sana ambayo tunatakiwa kuyafanyia kazi,” amesema.
Jaji Mkuu ameeleza kuwa kuna watu wengine wanadiriki kusema hata elimu ya sheria kuanzia Vyuo Vikuu, Shule ya Sheria imejengwa katika maudhui ya karne ya 18 au 19 na ndiyo maana wanapata shida katika teknolojia na utandawazi kwa vile mapinduzi ya teknolojia yameleta mageuzi ambayo sheria haziwezi kumudu.
“Ukienda Nchi zingine hawasomi masomo ya shahada ambayo tunasoma sasa, wameshaongeza masomo ya teknolojia, masomo ya biashara kwa sababu Dunia imebadilika,” Mhe. Prof. Juma amesema.
Ameeleza kuwa katika Mikutano ya Jukwaa la Dunia la Kiuchumi wanasema kati ya taaluma ambazo zipo hatarini kupotea kutokana na mapinduzi ni sheria na inaweza kupotea kwa sababu bado wanakanyaga katika maeneo yale yale ambayo mababu zao walikanyaga wakati Dunia imebadilika.
Kabla ya kuzungumza katika hafla hiyo, Jaji Mkuu alizindua taarifa iliyoandaliwa na Mahakama Kuu Kituo cha Usuluhishi kuhusu utafiti wa matumizi ya utatuzi mbadala wa migogoro na baadaye kutoa tuzo 23 kwa wadau mbalimbali kutoka na mchango wao kwenye suala la usuluhishi.
Akizungumza kabla ya kumkaribisha Jaji Mkuu, Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kituo cha Usuluhishi, Mhe. Zahra Maruma alieleza kuwa dhana ya utoaji wa tuzo za kutambua mchango wa Wapatanishi na Wasuluhishi ni moja ya mkakati katika kuhamasisha matumizi ya njia za usuluhishi katika utatuzi wa migogoro.
Alisema tukio hilo linafungua ukurasa mpya wa ushirikiano wenye tija katika kutambua michango ya wadau waliofanya vizuri kwani utatuzi wa migogoro kwa suluhu unaweka alama chanya na kuokoa gharama na muda ili kutoa fursa kwa wananchi kushiriki katika shughuli za kukuza uchumi endelevu kama Dira ya Taifa inavyoeleza.
Hivyo, Mhe. Maruma aliwapongeza Wapatanishi wote waliofanikisha upatanishi wa migogoro katika ngazi na nafasi zao ambazo, kwa namna moja au nyingine, umesaidia wepesi na upatikanaji wa haki na kuchangia katika utekelezaji wa nguzo ya tatu ya mpango mkakati wa Mahakama.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni