Ijumaa, 19 Januari 2024

MJADALA ‘KWA NINI SIYO UPATANISHI’ WAPAMBA UTOAJI TUZO KWA WADAU WA USULUHISHI

Na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Dar es Salaam

Hivi karibuni Mahakama Kuu ya Tanzania Kituo cha Usuluhishi kiliandaa hafla ya kutoa tuzo kwa wadau mbalimbali baada ya kutambua mchango wao katika utatuzi wa migogoro kwa njia ya usuluhishi.

Wakati wa hafla hiyo ambayo Mgeni Rasmi alikuwa Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma, kulikuwepo na mjadala kabambe uliowakutanisha watalaam mbalimbali wa masuala ya usuluhishi kujadili mada inayosema, ‘Kwa nini Sio Upatanishi?”

Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Fatma Khalifan aliendesha mjadala huo kwa umahiri mkubwa, huku wachangiaji wakiwasilisha hoja namna ya kuimarisha na kuendeleza matumizi ya usuluhishi ili kutatua migogoro ambazo zilizowafanya wageni mbalimbali waliohudhuria hafla hiyo kuendelea kufuatilia kwa makini muda wote.

Akichangia mada hiyo, Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dar es Salaam, Mhe. Salma Maghimbi aliimiminia Mahakama ya Tanzania kupitia Kituo cha Usuluhishi, kwa hatua kubwa waliyoifikia katika kuweka mazingira bora ya kumaliza mashauri kwa njia ya usuluhishi yenye faida lukuki.

Mhe. Maghimbi aliwasihi Mawakili kuwa wa kwanza kuwajenga wateja wao na kuwashauri kutumia njia ya usuluhishi ili mashauri yaweze kumalizika kwa haraka, hivyo kuwezesha haki kutendeka kwa pande zote mbili zinazohusika.

Akasisitiza uwepo wa elimu endelevu kuhusu njia hiyo ili kupata mwitikio chanya wa wananchi. Baadhi ya wadau waliojadili mada hiyo walibainisha changamoto za kisheria kuhusu usuluhishi na kutoa mapendekezo ya kuziondoa.

\

Mkufunzi Mkuu wa Shule ya Sheria kwa Vitendo, ‘Law School of Tanzania,’ Prof. Clement Mashamba alisema kuwa kuna aina 10 za Sheria zinazoanzisha usuluhishi na Kanuni mbalimbali, lakini tatizo hazina umoja.

Kadhalika, alisema kuna Taasisi nyingine zinazofanya usuluhishi huo huo, lakini kwa namna tofauti na kwamba hiyo ni changamoto kubwa, hivyo kuna haja ya kuirekebisha.

Prof. Mashamba alisema ingawa usuluhishi ni suala la kisheria na ni njia rahisi ya kutatua migogoro, bado Mawakili wengi hawaitumii kwa sababu hawana elimu ya kutosha kwa kuwa hawafundishwi vyuoni na kwamba wana hofu ya kukosa mapato.

Hivyo akashauri vyuo vianzishe somo hilo katika mitalaa yake, huku Wizara ya Katiba na Sheria, Ofisi ya Jaji Mkuu na Chama cha Mawakili Tanganyika (TLS) wakiangalia namna ya kujengea uwezo ili kutatua changamoto ya uhaba wa wataalamu wa usuluhishi.

"Ofisi ya Mwanaheria Mkuu wa Serikali na Wakili Mkuu wa Serikali mna jukumu la kuisaidia Serikali kumaliza migogoro kwa njia mbadala maana hawa tunaogombana nao bado tunahitajiana", alisisitiza.

Naye Katibu Mtendaji wa Tume ya Kurekebisha Sheria, Bw. George Mandepo alisema kuwa licha ya kuwa na vyombo vingi vya usuluhishi kama Tume ya Usuluhishi na Uamuzi (CMA) na Baraza la Ardhi na Nyumba, bado kuna changamoto katika utekelezaji kutokana na ukosefu wa elimu.

“Kuna baadhi ya Taasisi ambazo zinatajwa kwenye Sheria ya Usuluhishi na vyombo ambavyo vimeanzishwa lakini havina wataalamu. Wakati mwingine usuluhishi unachelewa kwa sababu wahusika na wadau wamelifanya jambo hilo kama ni sehemu ya kupata posho, kwani kuna kanuni ambazo zimeanziaha posho, kwa kadri ya muda unaotumika,” alisema.

Akabainisha pia kuna tatizo la mitizamo ya watu na hata Mawakili kupenda kufika mahakamani ili kuwa na hukumu za kuwaonesha watu kuwa ameshinda kesi, hivyo eneo la mafunzo kwa wataalamu, Mawakili na Wasuluhishi binafsi ni muhimu kutiliwa maanani.

Rais wa Taasisi ya Usuluhishi Tanzania, Bi. Madeline Kimei alisema vikwazo vinavyokwamisha usuluhishi ni pamoja na mtizamo wa watu kuona kwamba akienda mahakamani ndiyo atapata haki yake na kibaya zaidi kinatokana na aina ya mafunzo wanayopewa Wanasheria kwamba kazi yao ni kuwawakilishi wateja wao mahakamani pekee.

"Hivyo Sheria inapaswa irekebishwe ili, pamoja na mambo mengine, iweze kujibu swali la kwa nini siyo upatanishi," Bi. Kimei alisema na kuongeza kuwa kuwa licha ya kuwepo kwa Sheria, pengo la kutokuwepo kwa sera ya usuluhishi linarudisha nyuma juhudi zinazofanywa na Mahakama katika suala hilo.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Mashauri ya Katiba, Haki za Binadamu na Uchaguzi kutoka Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali, Bw. Hangi Chang'a alisema kuwa kabla ya marekebisho ya Sheria ya Mwenendo wa Mashauri ya Madai (CPC) mwaka 2019, suala la usuluhishi lilikuwa kama hiyari.

"Lakini baada ya marekebisho hayo limekuwa ni takwa la lazima kuwa mashauri ya madai lazima kwanza yapitie katika hatua ya usuluhishi. Sheria kwa sasa imeweka nidhamu kwani inabainisha madhara kama mtu asipohudhiria katika usuluhishi,"alisema.

Mwakilishi wa Kamati ya Sheria, Taasisi za Benki, Bw. Wala Nittu alisema kuwa kuna vikwazo vingine vya kimamlaka ambavyo vinakwamisha usuluhishi. Alisema kuwa upatanishi unaofanywa na Mahakama ni mzuri, lakini haujapewa mamlaka dhidi ya watu ambao wanaonekana kukwamiaha bila sababu za msingi.

Alibainisha kuwa kwenye Taasisi binafsi ndio kuna tatizo kubwa kwani hawana mamlaka ya kutekeleza makubaliano yanayofikiwa mpaka yapelekwe tena mahakamani ambako pia inabidi mtu afuate taratibu za usajiili, jambo ambalo linaweza kumfanya mtu aone haina haja.

Bw. Nittu akataja kikwazo kingine kuwa usimamizi na uwajibikaji, kwa kuwa hakuna mfumo unaobainisha kuwa hizo Taasisi binafsi zinawajibika kwa nani na zinasimamiwa na nani. "Benki ndio mwathirika mkubwa kuchelewa kwa usuluhishi kwani kuna pesa nyingi zinazokuwa zimeshikiliwa na zaidi unaathiri uchumi,"alisema.

Makamu wa Rais wa Chama cha Wanasheria wa Serikali kutoka Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Bw. Lukas Makumde alisema kuwa hata wale waliopewa jukumu la kusaidia kupatikana kwa suluhu, wakiwemo Mawakili wa Kujitegemea na hata Wasuluhishi, huchangia usuluhishi, wakati mwingine, kutokupatikana.

Hivyo akasihi kazi kubwa ifanyike kuwarejeshea imani wananchi waliokuwa wamekata tamaa kuhusiana na usuluhishi. "Wananchi wamekuwa na dhana ya ugomvi kwa miaka mingi, hivyo wanahitaji kubadilishwa dhana hiyo kwanza," Bw. Malumde alisema.

Naye Rais wa Chama cha Mawakili Tanganyika (TLS), Msomi Harold Sungusia albainisha kuwa licha ya Mawakili kusimamia haki kama maafisa wa Mahakama lakini pia wanafanyabiashara.

Alisema alisema kuwa kwa jinsi walivyofundishwa utalaamu wa kutumia Sheria Mawakili hupambana kwa hoja za kisheria mahakamani na ndipo huonyesha umahiri na umwamba waona hivyo kuaminika kwa mteja.

"Hivyo kuna dhana kwamba kama Wakili akijifungia tu katika chumba kupata usuluhishi, umaarufu wake utapotea na hata kipato kitashuka," Msomi Sungusia alisema.

Akabainisha pia kuwa kuna wateja wengine hawataki kabisa kusikia habari ya usuluhishi wakisema kwani wanaamini wakikomaa mahakamani na kuwa na uhakika wa kushinda hawataona sababu ya kwenda kwenye usuluhishi.

Hivyo Rais wa TLS akashauri uwepo wa haja ya kutoa elimu ya kutosha ili kubadili msimamo huo kwani usuluhishi una faida nyingi. 

Vilevile, Msomi Sungusia alisema usuluhishi ni suala ambalo linahitaji hekima na busara ya kijamii katika kufikia upatanishi na kwamba hilo siyo la wanasheria pekee, bali kuna watu wengine ambao ni Wapatanishi wazuri kuliko hata wale wenye uelewa wa Sheria.

Mtaalam kutoka Shirika la Miliki Bunifu Dunia, Bi Joyce Tan (picha ndogo katikati kwa juu) akichokoza mada kuhusu "Kwa nini Sido Upatanishi" kwa nia ya mtandao kutoka Uswizi.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dar es Salaam, Mhe. Salma Maghimbi akichangia hoja baada ya Mtalaam kutoka Shirika la Miliki Ubunifu Dunia, 'WIPO' kuhusu usuluhishi.

Wachangiaji wakichukua 'nondo' wakati Mtaalam wa masuala ya usuluhishi kutoa WIPO alipokuwa anachokoza mada. 


Wageni mbalimbali wakiongozwa na Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma wakifuatilia kwa karibu kile kilichokuwa kinaendelea wakati wa kujadili mada ya "Kwa nini Sio Upatanishi" katika hafla ya kuwakabidhi tuzo wadau mbalimbali wa usuluhishi.



Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Ibrahim Hamis Juma (katikati) pamoja na Majaji wa Mahakama Kuu, Mhe. Salma Maghimbi (kulia) na Mhe. Zahra Maruma (kushoto) pamoja na Majaji wengine (picha kwa nyuma) wakifuatilia kwa karibu mjadala huo. Picha chini, Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kituo cha Usuluhishi akitoa maelekezo kwa timu ya Wataalam wa Mitambo kabla ya hafla ya utoaji tuzo kuanza.


 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni