MAJAJI, MAHAKIMU WAKAZI ARUSHA WANOLEWA KUHUSU MIFUMO MIPYA YA TEHAMA MAHAKAMANI
Na Seth Kazimoto – Mahakama Kuu Arusha.
Kurugenzi ya Usimamizi wa Mashauri ya Mahakama ya Tanzania imetoa mafunzo kwa Majaji na Mahakimu Wakazi wa Mahakama katika Kanda ya Arusha kuhusu mifumo mipya ya kitekinolojia inayotumika mahakamani.
Mafunzo hayo yalifanyika hivi karibuni katika ukumbi wa wazi wa Mahakama ya Biashara mkoani hapa. Akifungua mafunzo hayo, Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Arusha, Mhe. Joachim Tiganga alisema kuwa mafunzo hayo yanalenga kuwapitisha Majaji na Mahakimu kwenye mifumo mipya ili kuwawezesha kuijua na kuitumia, hivyo kuboresha utendaji wa kazi za kimahakama.
Aliitaja mifumo hiyo ya kitehama, ikiwemo ule wa ki-elektroniki wa kuratibu uendeshaji na usimamizi wa mashauri (Electronic Case Management System—e-CMS) na mfumo wa Unukuzi na Tafsiri wa Mienendo ya Mashauri (TTS).
Mhe. Tiganga aliwataka wajumbe kujifunza kwa umakini na hatimaye kufikia malengo ya mafunzo hayo. ‘‘Ni matarajio yangu kuwa kila mmoja wenu atanufaika na mafunzo haya na kupelekea ufanyaji kazi mzuri zaidi bila vikwazo,’’ alisema Mhe. Tiganga.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Usimamizi wa Mashauri wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Desdery Kamugisha aliwaeleza wajumbe kuwa maboresho ya mifumo ya kimahakama ni endelevu kadri mahitaji yatakavyojitokeza. “
“Pamoja na changamoto zilizopo, elimu itazidi kutolewa ili mifumo ieleweke na kuwa rafiki zaidi kwa watumiaji,” alisisitiza.
Alifafanua kuwa mfumo wa ki-elektroniki wa kuratibu uendeshaji na usimamizi wa mashauri umelenga kutoa huduma za usajili wa mashauri kwa njia ya mtandao na kuyafuatilia yanavyotiririka katika hatua mbalimbali kwa njia za ki-elektroniki hadi hatua ya uamuzi.
Mhe. Kamugisha alisema pia kuwa mfumo huo huwezesha upangaji wa mashauri kwa Majaji na Mahakimu utakao wawezesha kusoma nyaraka zote za shauri kwa njia ya ki-elektroniki bila kulazimika kwenda ofisini na kuandika mienendo na hukumu kwenye mfumo moja kwa moja.
Akizungumzia mfumo wa Unukuzi na Tafsiri wa Mienendo ya Mashauri (TTS), alisema kuwa vifaa vitakapofungwa katika Mahakama zote, Majaji na Mahakimu wataachana na utaratibu wa kuandika mienendo ya mashauri kwa mkono na kumbukumbu zitakazotolewa na mfumo wa TTS zitakuwa ni maneno halisi yaliyotamkwa mahakamani.
Aidha, Mhe. Kamugisha alisema Mahakama ya Tanzania inaangalia uwezekano wa kuwa na vifaa vya akili bandia vinavyohamishika (mobile gadgets) katika Mahakama zake ili kuwezesha na kurahisisha usikilizaji wa mashauri eneo lolote.
Mafunzo hayo yalihudhuriwa na wajumbe mbalimbali, wakiwemo wawezeshaji ambao ni Afisa Tehama na Mjenzi wa Mifumo ya Mahakama wa Mahakama ya Tanzania, Bw. Said Tamimu na Mkurugenzi Msaidizi wa Kurugenzi ya Usimamizi wa Mashauri, Bi. Agnes Lawrence. Pia Msaidizi wa Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Mhe. Kassian Mshomba alihudhuria mafunzo hayo.
Wajumbe katika mafunzo hayo wakifuatilia kwa makini wanachoelekezwa.
(Habari hii imehaririwa na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Dar es Salaam)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni