Na Evelina Odemba-Mahakama, Morogoro
Mahakama ya Tanzania, Kanda ya Morogoro, imepokea jumla ya Taasisi 34 ambazo ni wadau wa Mahakama juu ya ushiriki wao katika kutoa elimu wakati wa maadhimisho ya wiki ya sheria yanayotarajia kuanza tarehe 24 Januari, 2024 na kuhitimishwa tarehe 30 Januari, 2024 mkoani hapa.
Hayo yemebainishwa na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Morogoro, Mhe. Latifa Mansoor katika mkutano na Waandishi wa Habari uliofanyika katika Jengo la Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki Morogoro.
Alizitaja baadhi ya Taasisi hizo kuwa ni Ofisi ya Taifa ya Mashtaka, Mawakili wa Kujitegemea, Mawakili wa Serikali, Jeshi la Polisi, Magereza, Uhamiaji na taasisi nyingine.
Jaji Mansoor pia aliwashukuru Waandishi wa Habari hao ambao wamekuwa mstari wa mbele kuuhabarisha Umma kuhusu shughuli zinazofanywa na Mahakama. Awasihi wawe bega kwa bega katika kipindi hicho ili kutoa habari za shughuli za Wki ya Sheria ili wananchi waweze kujua kinachoendelea.
Alibainisha kuwa wakati wa maadhimisho hayo watatumia Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) kurahisisha shughuli za utoaji haki na uelimishaji jamii kuhusiana na haki jinai.
Jaji Mfawidhi alieleza kuwa mwananchi atapata fulsa ya kujifunza namna mashauri yanavyofunguliwa kupitia mtandao na jinsi mteja anavyoweza kufuatilia taarifa za shauri kupitia mfumo wa Mahakama.
“Mahakama imejikita katika kuboresha miundombinu, mifumo na vifaa vya kisasa vya TEHAMA katika mfumo mzima wa utoaji haki kwa wananchi kwa uwazi na kwa wakati na ili kufanikisha yote hayo, Mahakama haiwezi kufanya kazi peke yake bali inahitaji ushiriki wa wadau,” alisisitiza.
Aliongeza kuwa Mahakama inapojitahidi kupeleka huduma zake kwa wananchi ni muhimu pia kwa Taasisi zingine za haki kufanya hivyo ili wananchi wapate uelewa sahihi wa matumizi ya elektroniki yanayotumiwa na Mahakama na wajue namna watakavyonufaika na mifumo hiyo ya Mahakama.
Mhe. Mansoor alieleza pia kuwa ili kufikia namna bora ya kufikisha elimu kwa wananchi, Mahakama imejipanga kupeleka elimu sehemu mbalimbali ndani ya Kanda ya Morogororo ambapo kwa mjini elimu itatolewa katika kituo mama ambacho kitakuwa standi ya zamani ya mabasi iliyoko Morogoro mjini.
Kadhalika, elimu itatolewa kupitia vyombo mbalimbali vya habari vilivyoko mkoani hapa, baadhi ya shule za sekondari na msingi, vyuo vikuu, kwenye magereza, maeneo ya masoko na kupitia kazi za sanaa kama maandiko, nyimbo na vipeperushi
Maonesho ya Wiki ya Sheria yatazinduliwa rasmi tarehe 27 Januari, 2024 kabla ya kuhitimishwa tarehe 30 January, 2024 kuelekea kilele cha Siku ya Sheria tarehe 1 Februari, 2024.
Kwa Mkoa wa Morogoro, uzinduzi utaanza kwa maandamano ambayo yataanzia katika Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki kuelekea uwanja wa stendi ya zamani ya mabasi mjini.
Maandamano hayo yataongozwa na Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Mhe. Adam Malima akiwa na mwenyeji wake, Jaji Mfawidhi. Mhe. Mansoor.
Kauli mbiu kwa mwaka 2024 inasema, “Umuhimu wa Dhana ya Haki kwa Ustawi wa Taifa: Nafasi ya Mahakama na Wadau katika Kuboresha Mfumo Jumuishi wa Haki Jinai.”
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya , Mhe. Latifa Mansoor akizungumza na Waandishi wa Habari (hawapo katika picha) katika mkutano wake maadhimisho ya Siku na Wiki ya sheria kwa Mahakama Kanda ya Morogoro.
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Morogoro, Mhe. Latifa Mansoor akisisitiza jambo kwa Waandishi wa Habari. kulia kwake ni Kaimu Mtendaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Morogoro, Bi. Elinuru Maleko.
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Morogoro, Mhe. Latifa Mansoor (katikati) akiwa na Naibu Msajili, Mhe. Susan Kihawa (kushoto) na Kaimu Mtendaji, Bi. Elinuru Maleko (kulia) wakati wa mkutano huo.
Mkutano ukiendelea.
(Habari hii imehaririwa na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Dar es Salaam)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni