Na. Mwandishi Wetu
Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma anatarajia kuzindua kitabu cha wasifu wa aliyekuwa Jaji wa Mahakama ya Rufani, Marehemu Mhe. Robert Kisanga ambaye alikuwa miongoni Majaji wa kwanza watano walioanzisha Mahakama ya Rufani hapa nchini mwaka 1979.
Hafla ya uzinduzi huo itafanyika Januari 23, 2024 katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Mwalimu Julius Nyerere (JNICC) jijini Dar es Salaam na imeandaliwa na Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA).
Viongozi mbalimbali wakiwemo wahe. Majaji Wakuu wastaafu, Majaji wa Rufani, Majaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Manaibu Wasajili, Mahakimu wa ngazi mbalimbali, Majaji wastaafu wa Rufani na Mahakama Kuu watahudhuria uzinduzi huo.
Wengine watakaohudhuria uzinduzi huo ni familia ya marehemu Jaji Kisanga, wanataaluma, wanahabari, wanasheria wa Serikali na wakujitegemea pamoja na wadau wengine wa sekta ya sheria.
Kitabu hicho kiitwacho "DREAM COMING TO FRUITION, A biography of JUSTICE ROBERT HABESH KISANGA," kwa maana ya Ndoto iliyotimia, Wasifu wa Jaji wa Rufani, Robert Kisanga, kimeandikwa na Chuo cha IJA.
Pia Kitabu hicho chenye kurasa 378 na sura... kinaelezea maisha ya marehemu Jaji Kisanga tangu kuzaliwa kwake, maisha yake ya shule, kazi zake za Uanasheria wa Serikali, kazi za Ujaji, na mchango wake katika Tasnia nzima ya Sheria na maendeleo ya nchi kwa ujumla.
Jaji Kisanga alizaliwa katika kijiji cha Fukeni katika Halmashauri ya Moshi vijijini Mkoani Kilimanjaro Juni 20, mwaka 1933, alifariki dunia Januari 23, mwaka 2018 katika Hospitali ya Regency jijini Dar es Salaam.
Aidha, Uzinduzi huo unaenda sambamba na kumbukizi ya miaka mitano ya kifo chake na unafanyika pia sambamba na siku hiyo aliyofariki dunia.
Marehemu Jaji Kisanga ambaye alihudumu katika Mahakama kwa miaka 32, enzi za uhai wake alishika nafasi mbalimbali ikiwemo ya kuwa Mwenyekiti mwanzilishi wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora kati ya mwaka 2002 hadi 2008.
Pia alikuwa Mwenyekiti wa Tume ya kukusanya maoni kuhusu mabadiliko ya Katiba ya mwaka 1998 ambayo iliundwa na Rais wa wakati huo marehemu Benjamin William Mkapa.
Marehemu Jaji
Kisanga anaendelea kukumbukwa kwa maamuzi yake thabiti na mashuhuri aliyowahi
kuyatoa enzi akiwa Jaji na Mwenyekiti wa Tume alizowahi kuziongoza.
Picha na Maktaba - Mahakama ya Tanzania
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni