MAHAKAMA KUU KITUO CHA USULUHISHI CHAWEKA HISTORIA
· Chatoa tuzo 23 kwa wadau wa usuluhishi
· Yumo mzee kutoka Mtwara anayesuluhisha migogoro usiku
· Jaji Mkuu awahakikishia wadau ushirikiano wa karibu
Na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Dar es Salaam
Mahakama Kuu Kituo cha Usuluhishi jana tarehe 16 Januari, 2024 kimetoa tuzo kwa wadau mbalimbali baada ya kutambua mchango wao katika utatuzi wa migogoro kwa njia ya usuluhishi.
Wadau hao 23 kutoka Taasisi mbalimbali na watu binafsi wamekabidhiwa tuzo hizo na Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe Prof Ibrahim Hamis Juma katika hafla iliyofanyika kwenye Ukumbi wa Mwalimu Nyerere jijini Dar-es-Salaam.
Katika hafla hiyo, Mzee Issa Mkumba kutoka Mkoa wa Mtwara anayesuluhisha migogoro wakati wa usiku alikuwa kivutio kikubwa kutokana na sifa alizojizolea kwa kufanya kazi hiyo kwa umahiri mkubwa uliosababisha Mahakama ya Mwanzo Msimbati kukosa mashauri.
Wadau wengine waliokabidhiwa tuzo hizo ni pamoja na Majaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Dkt. Cleophase Kasenene, Mhe. Dkt. Deo Nangela na Mhe. Gabriel Malata. Walikuwepo pia Mahakimu, Mawakili wa Serikali, Mawakili wa Kujitegemea, Watu Mashuhuri, Taasisi za Kiserikali na Taasisi binafsi.
Akizungumza kabla ya kukabidhi tuzo hizo, Mhe. Prof. Juma amewahakikishia wananchi kuwa Mahakama ya Tanzania ipo tayari kuendelea kushirikiana na wadau wote katika eneo la usuluhishi na ndiyo maana wameanzisha Kituo hicho maalumu ambao ndiyo “think tank” katika eneo hilo.
“Hawa kila siku wanafikiria usuluhishi na ndiyo wanaotushauri katika maeneo hayo, nyinyi kama mnachochote ambacho mnataka kuwasiliana na Mahakama (fanyeni hivyo kwenye) Kituo cha Usuluhishi ambacho ni muhimu sana,” Jaji Mkuu amewaeleza wadau hao.
Jaji Mkuu amewapongeza wadau mbalimbali kwani Mahakama inawategemea kuwa Waalimu katika eneo la usuluhishi na ndiyo watakaoangalia mapungufu ya sheria na taratibu na mapendekezo yao ndiyo yatazua na kuzalisha sheria nzuri.
“Nawaomba wale mtakaopewa tuzo muwe Mabalozi na wasemaji wa faida kubwa za usuluhishi,” Mhe. Prof. Juma alisema muda mchache kabla ya kuwakabidhi wadau hao tuzo zilizokuwa zimeandaliwa.
Naye Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kituo cha Usuluhishi, Mhe. Zahra Maruma, akizungumza katika hafla hiyo, amewaambia wageni waalikwa kuwa kumekuwepo na mafanikio ya usuluhishi yanaonekana kuongezeka katika kutekelezaji wa kauli mbiu ya Siku ya Sheria ya mwaka 2023 iliyokuwa inasema, “Umuhimu wa Utatuzi wa Migogoro kwa Njia ya Usuluhishi katika Kukuza Uchumi Endelevu: Wajibu wa Mahakama na Wadau.”
Ameeleza kuwa hadi kufikia mwezi Novemba, 2023, jumla ya mashauri 1,532 yakijumuisha Mahakama Kuu, Mahakama Kuu Divisheni ya Biashara, Mahakama za Hakimu Mkazi na Mahakama za Wilaya yalifikia hatua ya upatanishi.
“Jumla ya mashauri 671 yaliyofanikiwa kumalizika katika hatua hii, sawa na asilimia 44 ya mashauri yote yalifikia hatua ya upatanishi. Kiwango hiki ni mara mbili ya kwa asilimia 21 kwa mwaka 2022,” Mhe. Maruma amesema.
Jaji Mfawidhi amebainisha kuwa Mahakama Kuu Kituo cha Usuluhishi kwa mwaka 2023 kimefanikiwa kutatua mashauri 84, sawa na asilimia 21 ya mashauri 397 yaliyofikia hatua ya upatanishi, ikiwa ni ongezeko la idadi ya mashauri 20 ukilinganisha na 64 yaliyofanikiwa kupitia usuluhishi kwa mwaka 2022.
Mhe. Maruma amewaeleza wageni waalikwa kuwa kati ya hayo 397, mashauri 65 yanahusu migogoro ya kibenki yenye thamani ya kiasi cha 626,186,874,571/- ambapo mashauri 11 yalifanikiwa kumalizika kwa njia ya upatanishi kwa makubaliano ya thamani ya kiasi chja 142,563,982,134/-.
Amebainisha pia kuwa mashauri ya ardhi yalikuwa 233 ambapo 54 yalimalizika katika hatua ya upatanishi, huku 30 yaliyosalia yalihusu migogoro ya madai mbalimbali. Jaji Mfawidhi amesema muda uliotumika katika upatanishi wa mashauri hayo ni kati ya siku moja hadi 23.
Mhe. Maruma amewapongeza wadau wote waliofanikisha upatanishi wa migogoro katika ngazi na nafasi zao ambazo kwa namna moja au nyingine kumesaidia wepesi na upatikanaji wa haki na kuchangia katika utekelezaji wa nguzo ya tatu ya Mpango Mkakati wa Mahakama.
Hafla ya utoaji wa tuzo hizo imehudhuriwa na wageni mbalimbali, wakiwemo sehemu ya Majaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Majaji wa Mahakama Kuu wastaafu, Mawakili wa wa Serikali, Mawakili wa Kujitegemea, Viongozi wa Taasisi mbalimbali, Mabaraza ya Kata ya Ardhi, Wanafunzi wa Shule ya Sheria kwa vitendo na watumishi wa Mahakama.
Wakati wa hafla hiyo kulifanyika uzinduzi wa taarifa ya Utafiti wa Matumizi ya Utatuzi Mbadala wa Mogogoro: Usuluhishi, Dar es Salaam uliofanywa na Jaji Mkuu pamoja na mjadala kabambe kuhusu mada inayosema, “Kwa nini Siyo Upatanishi?” ulioongozwa na Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Fatma Khalifan.
Wataalam mbalimbali waliobobea katika masuala ya usuluhishi, wakiongozwa na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dar es Salaam, Mhe. Salma Maghimbi walishiriki katika mjadala huo uliokuwa wa kuvutia kiasi cha kuwafanya wageni kuendelea kufuatilia kilichokuwa kinajiri licha ya kuchukua muda mrefu.
Hoja na majadiliano hayo yalilenga katika kuimarisha suala la usuluhishi na mifumo iliyopo, huku wataalam hao wakiipongeza Mahakama ya Tanzania, hususan Kituo cha Usuluhishi kwa maendeleao makubwa ambayo kimeyafikia kuhusu utatuzi wa migogoro kwa njia mbadala.
Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Dkt. Deo Angela (katikati) akiwa na tuzo yake mara baada ya kukabidhiwa na Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe Prof Ibrahim Hamis Juma (kushoto). Kulia ni Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kituo cha Usuluhishi, Mhe. Zahra Maruma.
Majaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Dkt. Cleophase Kasenene na Mhe. Gabriel Malata wakiwa na tuzo zao.
Mzee Issa Mkumba kutoka Mkoa wa Mtwara ambaye ni bingwa wa kusuluhisha migogoro usiku akiwa na tuzo yake.
Meza Kuu ikiongozwa na Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe Prof Ibrahim Hamis Juma (katikati waliokaa) ikiwa katika picha ya pamoja na wadau mbalimbali waliokabidhiwa tuzo hizo (juu na chini).
Meza Kuu ikiongozwa na Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe Prof Ibrahim Hamis Juma (katikati waliokaa) ikiwa katika picha ya pamoja na Majaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania waliohudhuria hafla hiyo ya utoaji tuzo.
Meza Kuu ikiongozwa na Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe Prof Ibrahim Hamis Juma (katikati waliokaa) ikiwa katika picha ya pamoja na Majaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania wastaafu waliohudhuria hafla hiyo.
Meza Kuu ikiongozwa na Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe Prof Ibrahim Hamis Juma (katikati waliokaa) ikiwa katika picha ya pamoja na sehemu ya wajumbe wa menejimenti wa Mahakama ya Tanzania.
Meza Kuu ikiongozwa na Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe Prof Ibrahim Hamis Juma (katikati waliokaa) ikiwa katika picha ya pamoja na Mawakili wa Serikali na Mawakili wa Kujitegemea.
Meza Kuu ikiongozwa na Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe Prof Ibrahim Hamis Juma (katikati waliokaa) ikiwa katika picha ya pamoja na wadau wengine waliohudhuria hafla hiyo.
Meza Kuu ikiongozwa na Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe Prof Ibrahim Hamis Juma (katikati waliokaa) ikiwa katika picha ya pamoja na Wanafunzi wa Shule ya Sheria kwa vitendo.
Meza Kuu ikiongozwa na Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe Prof Ibrahim Hamis Juma (katikati waliokaa) ikiwa katika picha ya pamoja na watumishi kutoka Kituo cha Usuluhishi.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni