Jumatatu, 15 Januari 2024

JAJI KIHWELO AFUNGUA MAFUNZO YA ‘E-LEARNING’ KWA WATUMISHI WA MAHAKAMA

Na. YUSUFU AHMADI, IJA

Jaji wa Mahakama ya Rufani na Mkuu wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA), Mhe. Dkt. Paul F. Kihwelo amefungua mafunzo ya maandalizi na matumizi ya jukwaa la kufundishia kwa njia ya mtandao ‘e-learning’ ambalo limeandaliwa na Mahakama ya Tanzania kwa ajili ya kutoa mafunzo kwa watumishi wake kwa njia ya mtandao.

Mafunzo hayo yatakayochukua siku tano yamefunguliwa leo tarehe 15/01/2024 hapa Chuoni Lushoto na yameandaliwa na Mahakama ya Tanzania kwa kushirikiana na Chuo ambapo washiriki ni Majaji, Manaibu Wasajili, Mahakimu Wakazi, Maafisa Utumishi/Tawala, Maafisa TEHAMA pamoja na Afisa habari.

Katika hotuba yake ya ufunguzi, Mhe. Dkt. Kihwelo amesema kuwa jukwaa hilo la mafunzo ya mtandao litarahisisha utoaji wa mafunzo kwa washiriki wengi tofauti na kikwazo cha sasa cha gharama na umbali.

Sisi kama Chuo tunajivunia jukwaa hili na kuona fahari kwani litarahisisha utoaji wa mafunzo kwa washiriki wengi, kwa wakati na kwa gharama nafuu huku tukiendelea kutekeleza wajibu wetu kama Chuo wa kutoa mafunzo pamoja na kufanya tafiti,” amesema Mhe. Jaji Kihwelo.

Pia Mhe. Jaji Kihwelo ameongeza kuwa ujenzi wa jukwaa hilo ni utekelezaji wa dhamira ya Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma ambaye amekuwa akisisitiza Mahakama kujikita katika TEHAMA ili kuendesha shughuli zake ikiwemo kutoa mafunzo kwa njia ya mtandao.

Kuhusu mafunzo haya, Hakimu Mkazi Mkuu na Mkurugenzi wa Mafunzo ya Kimahakama, Mhe. Dkt. Patricia Kisinda amesema kuwa ndani ya siku hizo tano, washiriki watajifunza jinsi ya kutengeneza na kutumia  maudhui ya jukwaa hilo, na miongoni mwa maeneo yatakayokuwa yakifundishwa kupitia mfumo huo ni kama vile uandishi wa hukumu, jinsi ya kuendesha kesi, masuala ya kimaadili, na kujali mteja na mengineyo.

Naye Mkurugenzi Msaidizi wa Mafunzo ya Mahakama, Bi. Patricia Ngungulu amebainisha kuwa ujenzi wa jukwaa hilo umefadhiliwa na Benki ya Dunia kupitia mradi wa maboresho ya Mahakama ya Tanzania na kwamba upo katika Mpango Mkakati wa Mahakama wa mwaka 2020/21-2024/25.

Nao baadhi ya washiriki akiwemo Hakimu Mkazi Mkuu kutoka Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam Mhe. Richard Kabate pamoja na Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Mwanzo Kawe Dar es Salaam, Mhe. Nabwike Mbaba wamebainisha kuwa mafunzo hayo ni muhimu kwao kwani yatawasaidia kulifahamu vema jukwaa hilo kwa manufaa ya Mahakama na taifa kwa ujumla.

Jukwaa hilo la kujifunzia mtandaoni limetengenezwa na wataalamu wa hapahapa nchini kutoka Mahakama ya Tanzania, IJA, Chuo Kikuu Huria cha Tanzania na Chuo cha Serikali za Mitaa (Hombolo), na ni utekelezaji wa Mkakati wa Kitaifa wa Kuelekea Tanzania ya Kidigiti (Digital Economy Strategic Framework (2023-2033) pamoja na National ICT Policy 2023 ambavyo kwa pamoja vinachagizwa na Mradi wa Kidigiti wa Taifa (Digital Tanzania Project-DTP).

Jaji wa Mahakama ya Rufani na Mkuu wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA) Mhe. Dkt. Paul F. Kihwelo akihutubia wakati wa mafunzo ya maandalizi na matumizi ya jukwaa la kufundishia kwa njia ya mtandao ‘e-learning’ ambalo limeandaliwa na Mahakama ya Tanzania kwa ajili ya kutoa mafunzo  kwa watumishi wake kwa njia ya mtandao leo tarehe 15 Januari, 2023.

Jaji wa Mahakama ya Rufani na Mkuu wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA) Mhe. Dkt. Paul F. Kihwelo (aliyokaa katikati) akiwa pamoja na Jaji wa Mahakama Kuu, divisheni ya biashara kanda ya Dar es Salaam, Mhe. Prof. John Ubena pamoja na Hakimu Mfawidhi wilaya ya Lushoto Mhe. Rose Ngoka wakati wa mafunzo ya maandalizi na matumizi ya jukwaa la kufundishia kwa njia ya mtandao ‘e-learning’ ambalo limeandaliwa na Mahakama ya Tanzania kwa ajili ya kutoa mafunzo  kwa watumishi wake kwa njia ya mtandao. Waliyosimama ni Majaji, Manaibu Wasajili, Mahakimu Wakazi, Maafisa Utumishi/Tawala, Maafisa TEHAMA pamoja na Afisa habari.

Mkurugenzi Msaidizi wa Mafunzo ya Mahakama Bi. Patricia Ngungulu akizungumza wakati wa mafunzo ya maandalizi na matumizi ya jukwaa la kufundishia kwa njia ya mtandao ‘e-learning’ ambalo limeandaliwa na Mahakama ya Tanzania kwa ajili ya kutoa mafunzo  kwa watumishi wake kwa njia ya mtandao.

Sehemu ya Washiriki wa Mafunzo ya ya maandalizi na matumizi ya jukwaa la kufundishia kwa njia ya mtandao ‘e-learning’ ambalo limeandaliwa na Mahakama ya Tanzania kwa ajili ya kutoa mafunzo kwa watumishi wake kwa njia ya mtandao.

Hakimu Mkazi Mkuu na Mkurugenzi wa Mafunzo ya Kimahakama, Mhe. Dkt. Patricia akizungumza na vyombo vya habari wakati wa mafunzo ya maandalizi na matumizi ya jukwaa la kufundishia kwa njia ya mtandao ‘e-learning’ ambalo limeandaliwa na Mahakama ya Tanzania kwa ajili ya kutoa mafunzo  kwa watumishi wake kwa njia ya mtandao.







 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni