Na. Yusufu Ahmadi - IJA
Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA) kwa kushirikiana na Taasisi ya Kimataifa ya nchini Ireland (Irish Rule of Law International-IRLI) kwa ufadhili wa Ubalozi wa Ireland nchini Tanzania kinaendesha mafunzo maalumu ya wakufunzi juu ya uendeshaji wa mashauri yanayohusu waathirika wa ukatili wa kingono.
Mafunzo hayo yaliyoanza tarehe 09 Januari, 2024 Chuoni Lushoto na kuendeshwa kwa siku tatu hadi tarehe 11Januari, 2024, yanaendeshwa na Majaji waliyobobea kwenye mashauri ya ukatili wa kingono kutoka Ireland ya Kaskazini pamoja na Jamhuri ya Ireland.
Majaji hao wanajumuisha Majaji wa Mahakama ya Upeo, Mahakama ya Rufani na Mahakama Kuu huku washiriki wa mafunzo hayo wakiwa ni 17 ambao ni Majaji wa Mahakama Kuu, Manaibu wasajili wa Mahakama Kuu na Mahakimu Wakazi wa ngazi mbalimbali wa hapa nchini.
Akizungumzia mafunzo hayo, Jaji wa Mahakama Kuu kutoka Ireland ambaye pia ni mwezeshaji, Mhe. Mary Rose Gearty amesema: “Mafunzo haya tunayoyafanya ni kujaribu kuwafanya Majaji wavae viatu vya waathirika, wafahamu jinsi ilivyo vigumu kwa muathirika kuongea waziwazi na kusema kwamba suala hili lilinitokea. Kama Majaji wakifahamu hilo, wanaweza kushughulikia masuala hayo kwa ubora na wanaweza kuwasaidia waathirika kutoa ushahidi mzuri Mahakamani.”
Kwa upande wake, Jaji wa Mahakama ya Rufani na Mkuu wa Chuo, Mhe. Dkt. Paul Kihwelo amebainisha kuwa hatua itakayofuata baada ya mafunzo haya ni washiriki kwenda kuendesha mafunzo kwa maafisa wengine wa Mahakama wakiwemo Majaji na mahakimu katika kanda saba za Mahakama Kuu ya Tanzania.
Naye Naibu Mkuu wa Maendeleo na Ushirikiano kutoka Ubalozi wa Ireland hapa nchini, Bi. Mary McCarthy amesema kuwa mafunzo hayo ni hatua muhimu ya ushirikiano baina ya Tanzania na Ireland hasa katika kubadilishana uzoefu wa jinsi ya kuwalinda watoto dhidi ya ukatili wa kingono, akibainisha kuwa hiyo ni changamoto inayozikumba nchi zote hizo mbili.
Aidha, mmoja wa washiriki, Jaji wa Mahakama Kuu ambaye pia ni Jaji Mfawidhi, kituo Jumuishi cha masuala ya familia Temeke na mratibu wa mashirikiano kati ya IJA na IRLI, Mhe. Mwanabaraka Mnyukwa amesema kuwa anatarajia kujifunza kutoka kwa Majaji hao wa Ireland jinsi wao wanavyoendesha mashauri ya ukatili wa kingono katika kumlinda mtoto muathirika na mashahidi wa mashauri ya aina hiyo.
Mafunzo hayo yamehudhuriwa na viongozi mbalimbali wakiwemo maafisa wa Ubalozi wa Ireland hapa nchini.
Mafunzo haya ni moja ya maeneo ya Makubaliano ya Mashirikiano (MoU) baina ya IJA na IRLI yaliyosainiwa Machi 2022, kwa lengo la kuendeleza uhusiano kwenye eneo la kukabiliana na ukatili wa kingono dhidi ya wanawake na watoto.
Mafunzo haya yanaendana na sheria mbalimbali
ikiwemo Sheria ya Mtoto ya mwaka 2009, Sera ya Maendeleo ya Mtoto ya mwaka 2008
pamoja na mikataba mbalimbali ya Kimataifa na kikanda kama Mkataba wa Umoja wa
Mataifa wa Haki za mtoto (CRC) wa mwaka 1989 pamoja na Mkataba wa Afrika wa
Haki na Ustawi wa Mtoto wa Mwaka 1999.
Jaji wa Mahakama Kuu Mhe. Mary Rose Gearty kutoka nchini Ireland akiendesha mafunzo maalumu ya wakufunzi juu ya uendeshaji wa mashauri ya ukatili wa kijinsia yanayofanyika katika Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA). Washiriki wa mafunzo haya ni Majaji wa Mahakama Kuu, Manaibu wasajili wa Mahakama Kuu na Mahakimu Wakazi wa ngazi mbalimbali nchini.
Jaji wa Mahakama ya upeo, Mhe. Aileen Donnely (kulia) akiwa pamoja na Jaji wa Mahakama Kuu Mhe. Mary Rose Gearty kutoka nchini Ireland wakiendesha mafunzo maalumu ya wakufunzi juu ya uendeshaji wa mashauri ya ukatili wa kijinsia yanayofanyika katika Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA).
Sehemu ya Washiriki wa mafunzo maalumu ya wakufunzi juu ya
uendeshaji wa mashauri ya ukatili wa kijinsia yanayofanyika katika Chuo cha
Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA). Washiriki hao ni Majaji wa Mahakama Kuu, Manaibu wasajili wa
Mahakama Kuu na Mahakimu Wakazi wa ngazi mbalimbali wa hapa nchini.
Jaji wa Mahakama Kuu Mhe. Mary Rose
Gearty (aliyesimama mbele) kutoka nchini Ireland akiendesha mafunzo maalumu ya wakufunzi juu ya
uendeshaji wa mashauri ya ukatili wa kijinsia yanayofanyika katika Chuo cha
Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA). Washiriki wa mafunzo haya ni Majaji wa Mahakama
Kuu, Manaibu wasajili wa Mahakama Kuu na Mahakimu Wakazi wa ngazi mbalimbali wa
hapa nchini.
Jaji
wa Mahakama ya Rufani na Mkuu wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA)
Mhe. Dkt. Paul Kihwelo (kushoto) akimkabidhi machapisho ya Chuo Naibu Mkuu wa
Maendeleo na Ushirikiano kutoka Ubalozi wa Ireland hapa nchini, Bi. Mary
McCarthy wakati wa mafunzo maalumu ya wakufunzi juu
ya uendeshaji wa mashauri ya ukatili wa kijinsia yanayofanyika katika Chuo cha
Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA).
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni