Na. Mwandishi Wetu- Dar es Salaam
Jaji Mfawidhi wa Mahakama
Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dar es Salaam Mhe. Salma Maghimbi amebainisha kuwa, chimbuko
la Kauli Mbiu ya wiki na siku ya sheria nchini kwa mwaka 2024 inatokana na Tume
ya Haki Jinai iliyoundwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia
Suluhu Hassan na kupewa jukumu la kupitia mfumo mzima wa mnyororo wa utoaji
haki.
Akizungumza wakati wa
uzinduzi wa wiki ya sheria kwa Mahakama Kuu Kanda ya Dar es salaam iliyoambatana
na matembezi leo tarehe 27 Januari, 2024 katika Viwanja vya Mnazi Mmoja jijini
hapo Mhe. Maghimbi amebainisha kuwa Tume hiyo iliibua mambo 18 yanayogusa
Mahakama ya Tanzania, kutokana na taarifa hiyo ndiyo kauli mbiu ya mwaka huu
ilizaliwa ili kuakisi utekelezaji wa mapendekezo ya taarifa ya Tume hiyo.
Mhe. Maghimbi ameongeza
kuwa, katika
kutoa uamuzi wa mashauri ya madai na jinai, Mahakama itaongozwa na sheria na
Kanuni mbalimbali ambazo zimewekwa. Kwa muktadha huo, Mahakama inatumika kama
chombo cha utoaji haki kwa ajili ya kuboresha ustawi wa Taifa.
Mahakama
inatakiwa kushirikiana na wadau kuboresha mfumo jumuishi wa haki jinai. Mfumo
huo unatakiwa ufanye kazi kwa kushirikiana na kwa kusomana kwenye mifumo ya
Kielekitroniki kwa lengo la kuhakikisha kuwa wananchi wanaohitaji kupata haki
Mahakamani, basi wanatakiwa wapate haki zao kwa wakati bila kucheleweshwa kwa
haki hiyo kwa sababu tu ya mdau mmoja wa haki jinai aidha kwa makusudi au kwa
uzembe kushindwa kutekeleza majukumu yake kwa wakati, amesisitiza Jaji Maghimbi.
“Kwa
hivyo basi, lengo la kauli mbiu tajwa ni kutoa elimu na hamasa kwa umma juu ya
umuhimu wa dhana ya haki kwa ustawi wa Taifa, nafasi ya Mahakama na wadau
katika kuboresha Mfumo Jumuishi wa Haki Jinai,” ameongeza Mhe. Maghimbi
Aidha,
Mhe. Maghimbi amesema katika kutoa elimu kwa umma juu ya kauli mbiu hiyo, ni
vema katika wiki ya sheria na siku ya kilele chake, mada za utoaji elimu
zijikite katika kuelezea na kufafanua kwa uchache mambo ya msingi yayohusiana
na maboresho yanayoendelea Mahakamani na vile vile ushirikishwaji wa wadau
katika maboresho hayo kwa ajili ya kuboresha mfumo wa Haki Jinai kwa ujumla.
Mhe.
Maghimbi amewahakikishia wananchi watakaofika kwenye viwanja vya kutolea elimu
kuwa, mbali na elimu watakayoipata kuhusu maudhui ya wiki ya sheria ya mwaka
huu, pamoja na elimu ya mambo mengine ya kisheria, watapata pia nafasi ya kutoa
malalamiko, maoni na mapendekezo ya uboreshaji wa huduma za Mahakama.
“Nimatumaini
yangu na ya Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam kuwa, Taasisi zote
zinazosimamia sheria na zinazohusika kwenye Haki Jinai, zitatumia fursa hii kuhakikisha
kuwa wananchi wanaelewa vyema dhana nzima ya mfumo wa Haki Jinai inavyofanya
kazi zake na pia kuhakikisha kuwa haki inatendeka kwa wakati bila
kucheleweshwa,” amesisitiza Jaji Mfawidhi huyo.
Mhe.
Maghimbi akawakumbusha wananchi huduma watakazo kutana nazo katika kipindi
chote cha wiki ya sheria ikilenga elimu kuhusu taratibu za ufunguaji wa
mashauri hasa kwa njia ya mtandao, uendeshaji wa mashauri kimtandao, sheria na
taratibu zinazotumika katika kuendesha mashauri mbalimbali kama mashauri ya
ndoa na talaka, ardhi, migogoro ya kazi pamoja na utekelezaji wa hukumu, sheria
za watoto, taratibu za mashauri ya mirathi na sheria na taratibu zinazotumika
katika kuendesha mashauri ya jinai.
Aidha,
katika maonesho hayo elimu itatolewa na Waheshimiwa Majaji, Naibu Wasajili,
Watendaji, Mahakimu pamoja na wadau wa Mahakama wakiwemo Ofisi ya Mwanasheria
Mkuu wa Serikali, Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali, Ofisi ya Taifa ya Mashtaka,
Ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali, Ofisi ya Uhamiaji, Ofisi ya Mfuko wa Taifa wa
Bima ya Afya (NHIF),Afisa Mfawidhi Tume ya Usuluhishi na Uamuzi (CMA), Afisa
Mtendaji Mkuu wa Chama cha Wanasheria Wanawake (TAWLA), Chama cha Majaji na
Mahakimu Wanawake (TAWJA), Ofisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU),
Ofisi ya Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dar es Salaam, Ofisi ya Mkuu wa Magereza
Mkoa wa Dar es Salaam, Ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji Kituo cha Sheria na Haki za
Binadamu (LHRC), Ofisi ya Huduma kwa Jamii Mkoa wa Dar es Salaam, Mkurugenzi
Mtendaji Kituo cha Msaada wa Sheria kwa Wanawake na Watoto (WLAC), Chama cha
Wanasheria Tanganyika (TLS), na wadau wengine.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni