Jumamosi, 27 Januari 2024

MAFURIKO UZINDUZI WIKI YA SHERIA MIKOANI

Ufunguzi rasmi wa Wiki ya Sheria kwa mwaka 2024 umefanyika leo tarehe 27 Januari, 2024 katika Mikoa mbalimbali nchini, huku watumishi wa Mahakama, Wadau na wananchi kwa ujumla wakiwa wamejitokeza kwa wingi.

Mwandishi wetu Lusako Mwang’onda kutoka Mahakama Iringa anariopoti kuwa matembezi maalumu kwa ajili ya ufunguzi huo rasmi yamefanyika kwa mafanikio makubwa.

Mgeni rasmi alikuwa ni Mkuu wa Wilaya ya Kilolo, Mhe. Peres Magiri ambaye alimwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Iringa na alipokea matembezi hayo ambayo yaliongozwa na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Iringa, Mhe. Ilvin Mugeta huku majaji wengine wote wakiwa sehemu ya matembezi hayo. 

Matembezo hayo yameanzia Viwanja vya Mahakama Kuu Iringa na kuzunguka maeneo mbalimbali katikati ya Manispaa ya Iringa na hatimaye kutamatika katika Viwanja vya Garden vilivyopo maeneo ya Posta.

Akizungumza na umati wa watu uliohudhuria ufunguzi huo, Mhe. Migiri ameushukuru Uongozi wa Mahakama ya Tanzania kwa utaratibu wa kuwa na Wiki ya Sheria ambapo elimu kuhusu masuala mbalimbali ya kisheria na kimahakama kwa ujumla hutolewa bure kwa wananchi. 

Mhe. Migiri amewasisistiza wananchi kuhudhuria kwenye maeneo mbalimbali ambako elimu hutolewa. Pia ameuomba Uongozi wa Mahakama kuwa na utaratibu  wa kutoa elimu bure kwa wananchi mara kwa mara.

Naye Jaji Mfawidhi amemshukuru mgeni rasmi huyo kwa kuitikia wito wa kuja kujumuika na watumishi wa Mahakama katika ufinguzi rasmi wa Wiki ya Sheria. 

Mhe. Mugeta pia ameuomba umma wa Wanairinga kujitokeza kwa wingi kupata elimu ya bure kuhusu masuala mbalimbali ya kisheria. Jaji Mugeta amesema ni jambo la fahari kwa Mahakama ya Tanzania kutenga Wiki ya Sheria ili kujisogeza kwa wananchi, maana Mahakama ipo kwa ajili yao.



Watumishi wa Mahakama ya Tanzania, Kanda ya Iringa pamoja na Wadau mbalimbali wa haki (juu na chini) wakiwa kwenye matembezo ya uzinduzi rasmi wa Wiki ya Sheria.


Mkuu wa Wilaya ya Kilolo, Mhe. Peres Magiri akisisitiza jambo wakati akizungumza na umati uliohudhuria ufunguzi wa Wiki ya Sheria mkoani Iringa.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Iringa, Mhe. Ilvin Mugeta akizungumza na umati wa watu (hawapo pichani) uliojitokeza katika ufunguzi rasmi wa Wiki ya Sheria mkoani Iringa.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Iringa, Mhe. Ilvin Mugeta akimpa cheti cha shukrani kMgeni Rasmi, Mhe. Peresi Migiri kwa kukubali mwaliko wa kushiriki ufunguzi rasmi wa Wiki ya Sheria.

Kutoka Mahakama ya Hakimu Mkazi Katavi, James Kapele anaeleza kuwa maadhimisho ya Wiki ya Sheria Mkoani Katavi yamezinduliwa mapema leo asubuhi kwa matembezi yaliyohusisha wadau wa haki, wananchi, watumishi wa Mahakama na wengineo.

Matembezi hayo yameongozwa na Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Katavi, Mhe. Gway Sumaye na kupokelewa na Mkuu wa Wilaya ya Mpanda, Mhe. Jamila Yusuph katika Viwanja vya Mahakama ya Mwanzo Mpanda Mjini.

Akiwasilisha salamu zake katika uzinduzi huo, Mhe. Jamila ameipongeza Mahakama ya Tanzania kwa kuona umuhimu wa kuwa na Wiki ya Sheria kila mwaka kwa kuwa imekuwa ikiwaweka wananchi karibu na Mahakama hasa wanapokuwa wanatafuta haki zao katika vyombo mbalimbali vya sheria.

“Naipongeza sana Mahakama ya Tanzania kwa kuona umuhimu wa kuwa na maadhimisho haya kila mwaka kwa kuwa Wiki ya Sheria imekuwa muhimu sana kwa wananchi wetu kujipatia elimu ya masuala mbalimbali ya kisheria, lakini pia inawaweka wananchi karibu na Mhimili huu muhimu wa utoaji haki,” alisema.

Awali, akisoma hotuba yake ya ufunguzi wa maadhimisho hayo, Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Katavi pamoja na mambo mengine, amewahimiza wananchi kulitumia Wiki hilo kupata elimu ili wazijue haki zao za msingi wanazostahili kuzipata kisheria huku akisisitiza maudhui ya kauli mbiu ya Wiki ya sheria kwa mwaka huu 2024. 

“Kauli mbiu ya mwaka huu imekuja wakati sahihi sana kwani wananchi wengi wamekuwa wahanga wa haki zao wenyewe. Ni vyema mkatumia maadhimisho haya kikamilifu ili mpate kujua misingi mbalimbali ya namna ya kuzipigania na kuzitafuta haki zenu,” alisisitiza Mhe, Sumaye.

Mkuu wa Wilaya ya Mpanda ambaye ndiye aliyekuwa mgeni maalum katika uzinduzi wa maadhimisho hayo alihitimisha uzinduzi huu kwa kutembelea mabanda ya kutolea elimu katika viwanja vya Mahakama ya Mwanzo Mpanda Mjini.



Pichani ni sehemu ya wadau wakiwa katika matembezi ya ufunguzi wa Wiki ya Sheria mkoani Katavi mapema leo asubuhi.

Katika picha ni Mkuu wa Wilaya ya Mpanda, Mhe. Jamila Yusuphu akiwasilisha hotuba yake katika uzinduzi wa Wiki ya Sheria mkoani Katavi.

Pichani ni Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Katavi, Mhe. Gway Sumaye alipokuwa akiwasilisha hotuba yake.

Pichani ni sehemu ya watumishi na wadau walioshiriki katika uzinduzi wa maadhimisho hayo.

Katika picha, ni katika banda la Jeshi la Magereza ambalo nalo lilipata furssa ya kutembelewa na mgeni maalum wa uzinduzi huo.

Naye Abdallah Salum kutoka Mahakama Njombe anaripoti kuwa Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Njombe. Mhe. Liadi Chamshama ameongoza matembezi ya uzinduzi wa Wiki ya Sheria katika Mkoa huo.

Matembezi hayo yalianzia kwenye viunga vya Mahakama ya Mwanzo Njombe Mjini na kuelekea kwenye Viwanja vya Nation Housing Njombe, huku Mgeni Rasmi akiwa Mkuu wa mkoa wa Njombe, Mhe. Anthony Mtaka.

Akizungumza baada ya matembezi hayo, Mhe. Chamshama amemshukluru Mkuu wa Mkoa kwa kukubari kushiriki pamoja na wadau na wananchi waliojitokeza.

“Tukumbuke kuwa   mdau wetu mkubwa ni mwananchi, hivyo tunatakiwa kumpa elimu kuhusiana na haki zake za msingi katika masuala mbalimbali,” alisema.

Alisema kuwa Mahakama imekuwa ikiweka utaratibu wa kuwa na Wiki ya Sheria kwa lengo La kusogeza huduma karibu na mwananchi na asiweze kuiogopa Mahakama, huku akiwaomba wananchi waendelee kujitokeza kwa kutoa malalamiko yao kama yapo na kupata msaada wa kisheria.

Kwa upande wakem Mhe. Mtaka alimshkuru Hakimu Mkazi Mfawidhi, Mahakimu wote na wadau wa Mahakama kiujumla kwa kumkaribisha siku hiyo muhimu na kueleza kuwa wao kama Serikali wataendeleza ushirikiano pale ambapo kutakuwa na jambo ambalo linaitaji ushirikiano.

Aliiomba Mahakama kuwakaribisha vijana ambao wapo mashuleni hili waweze kushiriki na kujifunza hasa masuala ya sheria kwani wakipata elimu hiyo itawasaidia kuwahamasisha na kujitambua kwa siku za baadaye.

Matembezi hayo ya ufunguzi wa Wiki ya Sheria yalihudhuriwa na Wadau mbalimbali wakiwemo Waendesha Mashtaka, Mawakili wa Kujitegemea, Maofisa wa Takukuru, Maofisa wa NSSF, Madalali  wa Mahakama  na Jeshi la Polisi pamoja na wananchi.

Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Njombe, Mhe. Liadi Chamshama akiongea na wadau mbalimbali wa Mahakama (hawapo katika picha).

Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Mhe. Anthony Mtaka akiongea na watumishi na wananchi kwa ujumla.

Watumishi wa Mahakama wakiwa na mabango yaliyobeba kauli mbiu ya Wiki ya Sheria kwa mwaka huu 2024 katika matembezi hayo.

Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Njombe, Mhe. Liadi Chamshama (aliyevalia T-shert nyekundu) pembeni yake ni Mtendaji wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Njombe kwa Pamoja wakiongoza matembezi ya uzinduzi wa Wiki ya Sheria.

Baadhi ya watumishi na wananchi waliohudhuria kwenye uzinduzi wa Wiki ya Sheria wakisikiliza kinachoendelea.

Kutoka Mahakama Kuu Sumbawanga, Mwandishi wetu Mayanga Someke anaripoti kuwa maadhimisho ya Wiki ya Sheria yamezinduliwa kwa matembezi leo hii, lengo ni kuashiria kuanza kwa mwaka mpya wa shughuli za Kimahakama ambapo elimu na huduma mbalimbali zinatolewa kwa jamii kutoka kwenye taasisi mbalimbai.


Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Sumbawanga, Mhe. Dkt. Deo John Nangela amewashukuru wadau wote walioshiriki na amewapongeza wananchi waliojitokeza kupata elimu hiyo adhimu.

 “Ndugu Wananchi na Wadau wa Mahakama, leo tumezindua rasmi maadhimisho ya Wiki ya Sheria ambayo yanapambwa na kauli mbiu ya mwaka huu 2023 inayosema, “Umuhimu wa Dhana ya Haki kwa Ustawi wa Taifa: Nafasi ya Mahakama na Wadau katika Kuboresha Mfumo Jumuishi wa Haki Jinai.’’

Amesema kuwa kauli mbiu hiyo imebeba tafakari kubwa juu ya kuwakumbusha maafisa wa Mahakama na wadau kwamba wanalo jukumu kubwa la kuhakikisha upatikanaji wa haki unachangia ustawi wa Taifa la Tanzania na mfumo wa Haki Jinai ni eneo mojawapo la kuwezesha upatikanaji wa haki kwa wananchi wote wanaostahili kuipata.

“Niwaombe Wananchi kutumia fursa hii kujipatia elimu ya sheria itakayotolewa katika viwanja hivi,” amesema.

Naye Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Rukwa, Mhe. Peter Lijuakali ameishukuru Mahakama ya Tanzania Kanda ya Sumbawanga kwa ushirikiano wanaoendelea kumpa tangu nifike katika Mkoa huo.

Pia amepongeza jitihada zinazofanyika katika kuboresha miundombinu ya majengo ambayo inaiwezesha Mahakama, hususani katika Mkoa huo kutoa haki katika mazingira bora.

“Nichukue nafasi hii kwa niaba ya Serikali kuipongeza Mahakama ya Tanzania kwa kuweka Wiki na Siku ya Sheria kila mwaka,” amesema na kubainisha kuwa kauli mbiu ya maadhimisho hayo ni muhimu yenye lengo la kujenga ushirikiano baina ya Mahakama na wadau wake katika mnyororo wa utoaji wa haki kwa wananchi.







Habari hizi zimehaririwa  na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Dodoma

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni