Na Mwinga Mpoli, Mahakama-Mbeya
Mkuu wa Wilaya ya Chunya, Mhe. Mbaraka Batenga ameipongeza Mahakama ya Tanzania kwa kuja na kaulimbiu inayolenga kuhamasisha Mahakama na wadau juu ya umuhimu wa kufungamanisha na kusomana na ule wa wadau wa haki jinai.
Mhe. Batenga ameyasema hayo leo tarehe 27 Januari, 2024 kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Bw. Juma Zuberi Homera wakati wa uzinduzi rasmi wa Wiki ya Sheria uliofanyika katika viwanja vya Kabwe jijini Mbeya.
“Natoa wito kwa Taasisi zinazoshiriki katika Maonesho hayo ni pamoja na Ofisi ya Taifa ya Mashtaka, Chama cha Mawakili wa Kujitegemea (TLS), Jeshi la Polisi, Uhamiaji, Magereza pamoja na TAKUKURU kwa kuhakikisha mifumo yao inasomana na alitoa rai kwa wananchi kutumia fursa hii kutembelea maonesho ya Wiki ya Sheria kwani yanatokea mara moja na kwa kipindi kifupi cha wiki moja ili hali matatizo yanaendelea kila siku," amesema Mhe. Batenga.
Ametoa rai kwa Wadau kama Ofisi ya Taifa ya Mashtaka, Chama cha Mawakili wa Kujitegemea (TLS), Jeshi la Polisi, Uhamiaji, Magereza pamoja na TAKUKURU kwa kuhakikisha mifumo yao inasomana.
Kwa upande wake Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Mbeya, Mhe. Dunstan Ndunguru amemshukuru Mgeni rasmi kwa kuweza kujumuika na Mahakama Kanda hiyo katika uzinduzin wa Wiki ya Sheria.
“Natoa shukrani zangu kwako kwa kukubali mwaliko wetu katika uzinduzi wa wiki ya sheria kwa kanda yetu pamoja na kushiriki nasi katika matembezi yaliyoanzia viunga vya Mahakama na kuhitimishwa hapa katika viwanja vya kabwe”
Aidha, Mhe. Ndunguru amewaeleza wananchi kuwa, Mahakama pamoja na wadau wamejipanga kuhakikisha kuwa wananchi wanapata elimu ipasavyo kuhusu masuala ya sheria katika maeneo mbalimbali kama Mirathi, ndoa, ardhi, jinai, migogoro ya kikazi na masuala yote yanayohusu sheria.
Ufunguzi wa Wiki ya Sheria umehudhuriwa na Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Mbeya, Mhe. Dunstan Ndunguru, Majaji wa Kanda hiyo, Naibu Wasajili, Kaimu Mtendaji Mahakama Kuu Mbeya, Mahakimu, Wakili wa Serikali, Mkuu wa Ofisi ya Taifa ya Mashtaka Mbeya, Wakili Mkuu wa Serikali Mfawidhi, Mkoa wa Mbeya, Mwenyekiti Baraza la Ardhi, Msuluhishi Migogoro ya Kazi, Mawakili wote wa Serikali, Wajumbe wa Kamati ya Ulinzi na Usalama Mkoa wa Mbeya, Viongozi wa Serikali, viongozi wa madhehebu ya dini, watumishi wa Mahakama na wananchi.
Ufunguzi huo ulitanguliwa na matembezi yaliyoanzia viunga vya Mahakama mpaka viwanja vya Kabwe ambapo Mgeni Rasmi aliongoza matembezi hayo.
Mgeni Rasmi ambaye ni Mkuu wa Wilaya ya Chunya, Mhe. Mbaraka Batenga akizungumza katika hafla ya ufunguzi wa Wiki ya Sheria.
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Mbeya, Mhe. Dunstan Ndunguru akizungumza jambo katika viwanja vya kabwe wakati wa hafla ya uzinduzi wa Wiki ya Sheria. Watumishi wa Mahakama na wadau wa Mahakama wakisikiliza jambo.
Sehemu ya Watumishi wa Mahakama wakiwa katika matembezi ya uzinduzi wa Wiki ya Sheria yaliyoanzia viunga vya Mahakama mpaka viwanja vya Kabwe jijini Mbeya.
Majaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Mbeya pamoja na wadau wa Mahakama wakiwa katika matembezi ya uzinduzi wa Wiki ya Sheria yaliyoanzia viunga vya Mahakama Kuu mpaka viwanja vya Kabwe Mbeya.
Christopher Msagati wa Mahakama Kuu Kanda ya Manyara anaripoti kuwa Maadhimisho ya Wiki ya Sheria kwa upande wa Kanda hiyo yamefanikiwa kwa kiasi kikubwa ukilinganisha na mwaka jana.
Hayo yamebainishwa na Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu Kanda ya Manyara, Mhe. John Kahyoza katika ufunguzi wa Wiki ya Sheria uliofanyika leo tarehe 27 Januari, 2024.
Ufunguzi huo ulitanguliwa na matembezi yaliyoanzia viwanja vya Mahakama Kuu Manyara hadi katika viwanja vya Stendi ya zamani Babati yakiwajumuisha watumishi wa Mahakama pamoja na wadau wa Haki Jinai.
“Katika maadhimisho haya pamoja na kujivunia kumaliza kesi kwa wakati pia tunaweza kujivunia kwa kujitahidi kukua kwa matumizi ya TEHAMA na kupungua kwa kiasi kubwa kwa malalamiko ya wananchi tofauti na mwaka uliotangulia,” amesema Mhe. Kahyoza.
Kwa upande wake Mgeni Rasmi katika tukio hilo ambaye ni Mkuu wa Wilaya ya Babati, Mhe. Lazaro Twange ameipongeza Mahakama ya Tanzania kwa kuamua kuwafuata wananchi kwa karibu zaidi katika kuwasikiliza na kutatua kero zao, jambo ambalo limepunguza malalamiko pia katika ofisi yake.
“Zamani tulikuwa tukipokea malalamiko mengi sana yanayohusu Mahakama lakini kwa sasa yamekwisha kutokana na huduma mnayoitoa, tafadhali endeleeni na moyo huohuo” amesema Mhe. Twange.
Mahakama hii inaendelea na zoezi la utoaji elimu kwa wananchi katika wiki yote ya Sheria kwa kushirikana na wadau kama vile Ofisi ya Mashtaka Mkoa, TAKUKURU, Uhamiaji, Jeshi la Magereza, Ustawi kwa Jamii, Watoa Huduma za Kibenki pamoja na wengine katika maeneo mbalimbali yaliyochaguliwa.
Mkuu wa Wilaya ya Babati, Mhe. Lazaro Twange (katikati) ambaye ni Mgeni Rasmi wa uzinduzi wa Wiki ya Sheria kwa upande wa Kanda ya Manyara akiwa katika picha ya pamoja na Watumishi wa Kanda hiyo. Kushoto ni Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Manyara, Mhe. John Kahyoza na kulia ni Jaji Mahakama Kuu Kanda ya Manyara, Mhe. Frank Mirindo. Watumishi wa Mahakama Kuu Kanda ya Manyara wakifuatilia hotuba za Viongozi (hawapo katika picha) katika hafla ya Ufunguzi rasmi wa Wiki ya Sheria nchini. Mkuu wa Wilaya ya Babati, Mhe. Lazaro Twange akisikiliza maelezo yanayohusu utendaji kazi wa Mahakama kutoka kwa Hakimu Mkazi Mahakama Kuu Kanda ya Manyara, Mhe. Estomihi Haule.
Naye, Emmanuel Oguda kutoka Mahakama Kuu Kanda ya Shinyanga anaripoti kuwa, Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Mhe. Christina Mdeme ameupongeza Uongozi wa Kanda hiyo kwa kuwafikia wananchi wengi katika wiki ya elimu ya sheria inayoendelea katika maeneo mbalimbali ikijumuisha pia Wadau wa Haki Jinai wanaofanya kazi kwa karibu na Mahakama ya Tanzania.
Mhe. Mdeme ameeleza hayo wakati akizindua rasmi Wiki ya Sheria leo tarehe 27 Januari, 2024 katika Viwanja vya Zimamoto Manispaa ya Shinyanga ambapo amewataka wananchi kutumia nafasi hiyo kupata elimu ya sheria bure, hivyo wananchi wajitokeze kwa wingi katika maeneo hayo.
Akielezea ujumbe uliobebwa na Kaulimbiu ya mwaka huu, Mhe. Mndeme amesema kuwa kaulimbiu hiyo imebeba maana kubwa kwa Taasisi za Haki Jinai, hivyo ni vema Taasisi zote za Haki Jinai kuizingatia kaulimbiu hiyo na kuhakikisha zinasomana ili kutenda haki kwa wananchi.
Naye Jaji Mfawidhi, Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Shinyanga, Mhe. Frank Mahimbali amesema kuwa, kipindi cha Wiki ya Sheria ni kipindi ambacho Mahakama katika ngazi mbalimbali hujipambanua kwa wananchi namna inavyotoa haki kwa kushirikiana na wadau wake muhimu.
"Kipindi kama hiki cha utoaji wa elimu ya Sheria, ni kipindi ambacho wenye kiu ya kutaka kujifunza masuala yahusuyo sheria wanapata fursa hiyo bure, hivyo, ni rai yangu kuwa, baada ya uzinduzi rasmi leo, wananchi mtaendelea kujitokeza kwa wingi kupata elimu hiyo, Wataalamu wetu wapo kuwahudumia’’, amesema Mhe. Mahimbali.
Aidha, Jaji Mahimbali amewataka wananchi kuelewa kwa kina dhana nzima ya Haki Jinai ili kuondokana na dhana ya kulaumu Mahakama au Taasisi nyingine ya Serikali bila kuangalia kwa makini mnyororo wa Haki Jinai kuanzia kukamatwa kwa mshtakiwa hadi kufikia kupata adhabu.
Katika uzinduzi wa Wiki ya Sheria Mkoa wa Shinyanga, Wadau mbalimbali kutoka Ofisi ya Taifa ya Mashtaka, Wakili Mkuu wa Serikali, Magereza, Polisi, Uhamiaji, TAKUKURU, Madalali wa Mahakama, Vyuo mbalimbali vya elimu wamejitokeza kuungana na Mahakama Kuu Kanda hiyo katika uzinduzi wa Wiki ya Sheria.
Uzinduzi huo ulitanguliwa na matembezi yaliyoanzia katika Viwanja vya Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Shinyanga ukitumia barabara za Mohamed 'Trans', Katemi 'Hotel', Liga 'Hotel', Lyakale 'Hotel' kisha kutokea mzunguko 'Roundabout' yalikuwa kivutio cha wengi hasa baada ya wadau katika matembezi hayo kutembea kilomita sita bila kuchoka.
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Mhe. Christina Mndeme akizungumza na wananchi wa Shinyanga (hawapo katika picha) wakati wa hafla ya uzinduzi wa Wiki ya Sheria mkoani Shinyanga leo tarehe 27 Januari, 2024.
Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Shinyanga, Mhe. Frank Mahimbali akitoa salaam za Kanda ya Shinyanga wakati wa uzinduzi wa Wiki ya Sheria mkoani Shinyanga leo tarehe 27 Januari, 2024. Sehemu ya wageni waalikwa wakisikiliza Hotuba ya Mgeni Rasmi (hayupo katika picha) wakati wa Uzinduzi wa Wiki ya Sheria leo tarehe 27 Januari, 2024. Sehemu ya Watumishi na wananchi wakisikiliza kwa makini hotuba ya Mgeni Rasmi (hayupo katika picha) wakati wa uzinduzi wa Wiki ya Sheria mkoani Shinyanga. Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Mhe. Christina Mndeme (katikati) akiongoza matembezi ya uzinduzi wa Wiki ya Sheria, kulia ni Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Shinyanga, Mhe. Frank Mahimbali na kushoto ni Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga, Mhe. Johari Samizi. Matembezi kuelekea viwanja vya Zimamoto Shinyanga yakiongozwa na Brassband.
Tukiangazia Kanda ya Geita, Mwandishi wetu Charles Ngusa anaripoti kuwa, Mkuu wa Mkoa wa Geita, Mhe. Martin Shigela ameongoza maandamano ya uzinduzi wa Wiki ya Sheria ambapo pia ameipongeza Mahakama ya Tanzania kwa kuanzisha Mahakama Kuu katika Mkoa huo.
"Naipongeza sana Mahakama ya Tanzania kwa kuanzisha Mahakama Kuu katika Mkoa huu pamoja na kwamba majengo ya Mahakama Kuu bado hayajakamilika lakini imeamua kuwateua Majaji ili waje kutoa huduma katika Mkoa wetu jambo ambalo limesaidia sana katika kuwapunguzia gharama wananchi wetu waliokuwa wakilazimika kufuata huduma za Mahakama Kuu Mkoani Mwanza," amesema Mhe. Shigela.
Amepongeza pia Mahakama kwa kuja na mfumo mpya wa kufanya maadhimisho kwa njia ya maonesho kwani yanasaidia kuwafikia walengwa wengi zaidi katika eneo moja tofauti na miaka ya nyuma ilivyokuwa ikifanyika kwa njia ya utoaji wa elimu kwa wadau wachache.
Kwa upande wake, Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu Kanda ya Geita, Mhe. Kevin Mhina amemkabidhi zawadi mgeni rasmi ili kuendeleza huduma ya utoaji elimu kwa wananchi.
“Napenda kukukabidhi zawadi ambayo sisi kama Mahakama Kuu Kanda ya Geita tumeamua kutengeneza vipeperushi ambavyo vinaelezea shughuli mbalimbali za Mahakama kuanzia Mahakama za Mwanzo hadi Mahakama Kuu, naomba nikukabidhi kama zawadi ili wananchi wanapotembelea katika ofisi yako utatusaidia kuwapatia ili nao wapate elimu juu ya mifumo yetu ya Mahakama na muundo wake,” amesema Mhe. Mhina.
Jaji Mfawidhi amempongeza Mkuu wa Mkoa kwa kuendelea kuwapa ushirikiano na wao kama Mahakama watajitahidi kutoa huduma iliyo bora zaidi na zaidi na kuwakaribisha wananchi waendelee kutembelea eneo la maonesho ili waweze kujifunza vitu vingi zaidi.
Mahakama Kuu Kanda ya Geita leo tarehe 27 Januari, 2024 imeungana na Mahakama nyingine nchini kuzindua rasmi maadhimisho ya Wiki ya Sheria nchini.
Uzinduzi huu umetanguliwa na maandamano ya wadau wote wa Mahakama ambayo yalianzia katika viwanja vya Mahakama Kuu Kanda ya Geita na kuhitimishwa katika viwanja vya EPZA yakiongozwa na Mkuu wa Mkoa wa Geita, Mhe. Martin Shigela akiwa sambamba na mwenyeji wake Mhe. Jaji Mfawidhi Kanda ya Geita, Mhe. Kevin Mhina pamoja na Wadau mbalimbali walioshiriki katika maandamano hay kama vile Polisi, Magereza, Uhamiaji, Zimamoto, Ofisi ya Mashtaka, TAKUKURU, Uhamiaji na wengine.
Baada ya kuwasili katika viwanja vya maonesho, Mhe. Shigela alipata wasaa wa kukagua mabanda mbalimbali ambayo yapo katika eneo hilo ambayo yamekuwa vituo vya kutolea elimu tangu tarehe 24 Januari , 2024. Mabanda aliyotembelea ni pamoja na Mahakama ya Mwanzo Nyankumbu ambapo alipata fursa ya kuelezewa shughuli mbalimbali ambazo zimekuwa zikitolewa katika Mahakama za Mwanzo.
Awali mwenyeji wake Jaji Mfawidhi alimweleza kuwa Kanda ya Geita kwa sasa ni Kanda ambayo imeanzishwa ili iwe mfano wa kuendesha shughuli za Kimahakama Kidijitali hivyo basi shughuli zote zinazofanyika mkoani Geita zinafanyika Kidijitali ikiwemo usajili wa mashauri.
Baada ya hapo alitembelea banda la Mahakama ya Wilaya Geita, Mahakama ya Hakimu Mkazi Geita, Mahakama Kuu Kanda ya Geita. Kadhalika alipata nafasi ya kupitia mabanda yote yaliyokuwa katika eneo la maonesho ikiwa ni pamoja na banda la Ofisi ya Mashtaka, Mawakili wa Kujitegemea, PSSSF, NSSF, Idara ya kazi, RITA, banda la wajasiriamali na banda la Madalali wa Mahakama na Wasambaza nyaraka.
Wananchi, Watumishi pamoja na Wadau wengine wa Mahakama wakishiriki katika maandamano wakati wa uzinduzi wa Wiki ya Sheria mkoani Geita leo 27 Januari, 2024.
Vyombo vya Ulinzi na usalama vikishiriki katika Maandamano ya uzinduzi wa Wiki ya Sheria. Watumishi na wadau mbalimbali wakisikiliza hotuba zilizokuwa zikitolewa wakati wa uzinduzi wa Wiki ya Sheria nchini.
Wadau pamoja na wananchi wakifuatilia hotuba mbalimbali kutoka kwa Viongozi wakati wa hafla ya uzinduzi wa Wiki ya Sheria leo tarehe 27 Januari, 2024. Mkuu wa Mkoa wa Geita, Mhe. Martin Shigela akiwasilisha hotuba yake mbele ya wananchi na wadau mbalimbali wa Mahakama waliohudhuria katika uzinduzi wa Wiki ya Sheria. Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu Kanda ya Geita, Mhe. Kevin Mhina (katikati) akikabidhi zawadi ya vipeperushi kwa Mkuu wa Mkoa wa Geita, Mhe. Martin Shigela (kushoto).
Mwakilishi wetu kutoka Mahakama ya Hakimu Mkazi Singida Eva Leshange anaripoti kuwa, Mahakama na Wadau wa Haki Jinai mkoani humo nao wamefanya matembezi ya amani kwa ajili ya uzinduzi rasmi wa Wiki ya Sheria nchini.
Matembezi hayo yalianzia katika viwanja vya Mahakama ya Hakimu Mkazi Singida na kupitia Barabara ya Dodoma, Benki ya NMB, Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na kurudi na njia ya Arusha na kumalizia katika viwanja vya Mahakama hiyo.
Matembezi hayo yaliongozwa na Katibu Tawala Mkoa wa Singida, Bi Naima Chondo aliyekuwa akimwakilisha Mkuu wa Wilaya Singida, aidha aliambatana na viongozi wengine wa Kiserikali kutoka Ofisi za Uhamiaji, Usalama, TAKUKURU, Ofisi ya Mashtaka Mkoa wa Singida, Magereza na Chama cha Mawakili Tanganyika (TLS).
Akitoa neno la ufunguzi, Hakimu Mkazi Mfawidhi Mahakama ya Hakimu Mkazi Singida, Mhe. Allu Nzowa katika hafla hiyo amesema, "Jukumu kubwa la Mahakama kikatiba ni kutoa haki ikiongozwa na Dira yake ya Utoaji Haki kwa wakati na kwa watu wote hivyo basi Mahakama imEkuwa ikifanya maboresho kwenye huduma zake kupitia utekelezaji wa Mpango Mkakati wa Mahakama wa Miakata mitani(2020/2021-2024/2025)."
Aidha, amewaeleza wananchi kwamba, Mahakama sio kisiwa imekuwa ikishirikiana kwa dhati na wadau wake wa Haki Jinai katika kutekeleza Dira yake kwa mustakabali wa ustawi wa Taifa.
"Kwa kutambua umuhimu huo maadhimisho ya Wiki na Siku ya sheria Nchini 2024 yanaongozwa na kaulimbiu isemayo "Umuhimu wa Dhana ya Haki na ustawi wa Taifa: Nafasi ya Mahakam ana wadau katika kuboresha mfumo jumuishi wa Haki Jinai"
Vilevile amewajulisha wananchi kuwa, Mahakama kwa sasa imewekeza katika suala la TEHAMA ili kuhakikisha mifumo iliyopo mahakamani inasomana na wadau wake na hii itasaidia kubadilishana taarifa kwa wakati kuanzia katua ya uchunguzi/upelelezi, uendeshaji wa shauri na utoaji wa Maamuzi ambapo amebainisha kuwa jitihada zilizopo kwa sasa ni kuwekeza kwenye miundombinu ya kisasa ya TEHAMA, kuajiri wataalam wa kutosha, kutoa mafunzo kwa watumishi na kuwawezesha wadau vifaa vya TEHAMA.
Naye Katibu Tawala Wilaya ya Singida, Mhe. Naima Chondo ameipongeza Mahakama ya Tanzania kwa juhudi za dhati inayofanya kuhakikisha mnyororo wa utoaji haki kwa wakati unafanikiwa ipasavyo pasipo kucheleweshwa kwani haki ilicholeweshwa ni sawa na Haki iliyonyimwa.
Pia amewasisitiza wananchi kufuata sheria mbalimbali za Nchi na watumie maadhimisho hayo vizuri kujua sheria mbalimbali ili kuepuka kukinzana na Sheria, amesisitiza watembelee mabanda ya elimu kwakuwa kuna wataalamu mbalimbali kutoka Taasisi tofautitofauti zinazofanya kazi na Mahakama ili kuongeza maarifa zaidi.
Naye Mtendaji wa Mahakama Mkoa wa Singida amewashukuru sana wa wadau na wanachi waliojitokeza katika uzinduzi wa Wiki ya Sheria nchini na kuwakaribisha Siku ya Kilele tarehe 01 Februari, 2024 katika viwanja vya Mahakama ya Hakimu Mkazi Singida.
Hakimu Mkazi Mfawidhi, Mahakama ya Hakimu Mkazi Singida, Mhe. Allu Nzowa akitoa neno la ufunguzi katika hafla ya ufunguzi wa Wiki ya Sheria nchini leo tarehe 27 Januari, 2024 katika viwanja vya Mahakama hiyo.
Katibu Tawala Wilaya ya Singida, Mhe. Naima Chondo (aliyeshika kipaza sauti) akizungumza na wananchi na watumishi (hawapo katika picha) waliohudhuria ufunguzi wa Wiki ya Sheria leo tarehe 27 Januari, 2024 katika viwanja vya Mahakama ya Hakimu Mkazi Singida. Sehemu ya wadau wa Haki Jinai waliofika katika sherehe za ufunguzi wa Wiki ya Sheria nchini 2024 katika viwanja vya Mahakama ya Hakimu Mkazi Singida. Sehemu ya watumishi waliohudhuria hafla ya uzinduzi wa Wiki ya Sheria katika viwanja vya Mahakama ya Hakimu Mkazi Singida. Sehemu ya watumishi wa Mahakama na Wadau walioshiriki maandamano ya uzinduzi wa Wiki ya Sheria nchini 2024 wakiwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Singida.
(HABARI HIZI ZIMEHARIRIWA NA MARY GWERA, MAHAKAMA-DODOMA)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni