Na Mary Gwera, Mahakama-Dodoma
Mwenyekiti wa Chama cha Majaji na Mahakimu Wanawake Tanzania (TAWJA) ambaye pia ni Jaji wa Mahakama ya Rufani (T), Mhe. Barke Sehel leo tarehe 26 Januari, 2024 ametembelea mabanda ya maonesho ya Wiki ya Sheria yanayofanyika katika Viwanja vya Nyerere ‘Square’ Dodoma.
Katika ziara yake, Mhe. Sehel ameambatana na Jaji wa Mahakama ya Rufani, Mhe. Rehema Mkuye, Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dodoma, Mhe. Dkt. Juliana Masabo na Majaji wengine wa Mahakama hiyo.
Mhe. Sehel ametembelea mabanda mbalimbali yaliyopo katika maonesho hayo ikiwa ni pamoja na banda la Chama cha Majaji na Mahakimu Wanawake Tanzania (TAWJA), Kurugenzi ya Usimamizi wa Mashauri, TEHAMA, Wadau wa Haki Jinai.
Akiwa banda la TEHAMA, Mhe. Sehel ameelezwa kuhusu Mfumo mpya wa Unukuzi na Tafsiri Mienendo ya Mashauri (TTS) ambapo Mhe. Sehel aliuliza jinsi Mfumo huo unavyofanya kazi.
Mabanda mengine aliyotembelea ni Wizara ya Katiba na Sheria, Ofisi ya Taifa ya Mashtaka na kituo Jumuishi cha Utoaji Haki (IJC) Dodoma.
Leo ni Siku ya tatu ya Maonesho ya Wiki ya Sheria yanayoendelea kufanyika katika Mahakama zote nchini, Wiki hii inatarajiwa kuzinduliwa rasmi kesho tarehe 27 Januari, 2024.
Kwa upande wa Dodoma ambapo maonesho haya yanafanyika Kitaifa, yatazinduliwa na Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Tulia Ackson.
Kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Sheria itakuwa tarehe Mosi, Februari, 2024 ambapo kitaifa itafanyika katika Viwanja vya Chinangali jijini Dodoma ambapo Mgeni Rasmi anatarajiwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni