Ijumaa, 26 Januari 2024

WANANCHI MBEYA JITOKEZENI KWA WINGI ELIMU YA SHERIA NI BURE: JAJI NDUGURU

Mwinga Mpoli – Mahakama, Mbeya 

Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Mbeya Mhe. Dunstan Ndunguru amewaomba wananchi kujitokeza kwa wingi katika mabanda ya kutolea elimu yaliyopo viwanja vya kabwe jijini Mbeya kwani elimu hiyo inatolewa bure bila malipo na amewapongeza taasisi zote zilizojitokeza kutoe elimu kwa wananchi. 


Ameyasema hayo jana tarehe 25 Januari, 2024 wakati alipotembelea viwanja vya Kabwe vitakavyotumika kutolea elimu ambapo Mahakama Kuu pamoja na wadau wengine wa Mahakama wameweka mabanda kwa ajili ya kufikisha elimu hiyo ya sheria kwa wananchi kwa kipindi hiki cha maadhimisho ya wiki ya sheria na kilele cha siku ya sheria nchini. 


“Niwaombe tu wananchi waendelee kujitokeza kupata elimu na msaada wa kisheria kwa wingi kwani ni nafasi adhimu ya kujipatia elimu na kupata uelewa pia wajue Mahakama ni sehemu salama” alisisitiza Mhe. Ndunguru


Aidha,Hakimu Mkazi Mahakama ya wilaya Mbeya Mhe. Paul Rupia akitoa elimu katika shule ya sekondari Mbeya amewaeleza wanafunzi juu ya makosa ya jinai haswa suala la matumizi ya madawa ya kulevya, madhara yake na adhabu zake pindi itakapothibitika. Pia alizungumzia makosa ya uchomaji moto majengo au jaribio la kuchoma moto jengo, athari zake na adhabu za makosa hayo. 


Mhe. Rupia aliongozana na Hakimu Mkazi Mhe. Miriam Kimwaga, Bw. Stephen Rusibamayila wakili wa serikali kutoka Ofisi ya Taifa ya Mashtaka, Isabela Lawrent na Ipyana Mwamtoto ambao ni Mawakili kutoka chama cha wanasheria Tanganyika (TLS).


Wakitoa elimu katika shule ya msingi Kambarage Mhe. Scout Andrew aliyeongozana na Mahakimu pamoja na wadau wengine wa Mahakama wao walianza kwa kuongea na walimu juu ya masuala ya kubadirisha warithi pia masuala ya ndoa, na baadae kuongea na wanafunzi juu ya masuala ya ukatili wa kijinsia kwa watoto mashuleni na majumbani.


 “Ndugu watumishi mara tunapoajiliwa kuna wakati tunaandika warithi wetu lakini tuna uwezo wa kubadirisha warithi hao ikiwa kuna sababu za msingi za kuwabadirisha” alisema Mhe. Andrew


Naye, Insp. Loveness Mtemi aliwaeleza watoto aina za ukatili wa kijinsia na viashiria vibaya vya ukatili na kuwashauri watoto watakapoona dalili za viashiria hivyo hatua zipi wazichukue.


Zoezi la utoaji elimu linaendelea kwa kasi mkoani Mbeya ambapo watumishi wa Mahakama na wadau wanapita maeneo mbalimbali ili kuhakikisha namba kubwa ya wananchi inafikiwa katika harakati za kuhakikisha haki inapatikana kwa wakati na kwa usawa.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Mbeya Mhe. Dunstan Ndunguru akiongea na wanahabari (hawapo pichani) wakati alipotembelea viwanja vya Kabwe jijini Mbeya eneo linalotumika kutolea elimu na msaada wa kisheria jana tarehe 25 Januari, 2023.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Mbeya Mhe. Dunstan Ndunguru (wa kwanza kulia), Jaji wa Mahakama Kuu kanda ya Mbeya Mhe. Aisha Sinda (wa pili kulia) na Jaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Mbeya Mhe. Emmanuel Kawishe (wa pili kushoto) wakisikiliza jambo kutoka kwa mdau katika viwanja hivyo.

 

Jopo la watoa elimu pamoja na walimu katika shule ya msingi Kambarage wakiongozwa na Hakimu Mkazi Mhe. Scout Andrew wa tatu kulia.

Insp. Loveness Mtemi akijaribu kuwaeleza jambo wanafunzi wa shule ya msingi Kambarage kwa vitendo.

Sehemu ya watoa elimu na walimu katika shule ya sekondari Mbeya.

Sehemu ya wanafunzi wa shule ya sekondari Mbeya wakisikiliza elimu wanayopatiwa.

Hakimu Mkazi Mhe. Paul Rupia akiwaeleza wanafunzi wa Shule ya Sekondari Mbeya Jambo.

Watoa elimu katika kituo cha redio Rock Fm 96.9 katikati ni Hakimu Mkazi Mhe. Dickson Mmasi.


Hakuna maoni:

Chapisha Maoni