Ijumaa, 26 Januari 2024

SPIKA WA BUNGE MGENI RASMI UZINDUZI WA WIKI YA SHERIA KITAIFA 2024

Na Tiganya Vincent-Mahakama, Dodoma

Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambaye pia ni Rais wa Umoja wa Mabunge Duniani, Mhe. Dkt. Tulia Ackson kesho tarehe 27 Januari, 2024 atakuwa Mgeni Rasmi kwenye uzinduzi wa maonesho ya Wiki ya Sheria yanayofanyika kitaifa jijini hapa.

Uzinduzi huo utatanguliwa na matembezi maalumu yatakayoanzia katika Viwanja vya Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki Dodoma na kupitia maeneo ya Polisi, Kanisa Katoliki, Mirembe, Njia Panda ya Iringa na Singida, Sokoni, Uwanja wa Jamhuri na kumalizikia katika Viwanja vya Nyerere Square.

Matembezi kama hayo ya uzinduzi wa Wiki ya Sheria yatafanyika pia kuanzia ngazi za Wilaya, Mikoa na Kanda mbalimbali za Mahakama Kuu kabla ya kuendelea na maonesho kwenye mabanda ambayo yameandaliwa na Mahakama na wadau kwa lengo la kutoa elimu na huduma kwa wananchi.

Wadau wanaoshiriki katika maonesho hayo yakayohitimishwa tarehe 30 Januari, 2024 ni pamoja na Wizara ya Katiba na Sheria, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali, Ofisi ya Taifa ya Mashtaka, Jeshi la Polisi, Jeshi la Magereza, Mamlaka ya Udhibiti wa Madawa ya Kulevya, Ofisi ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali na wengine. 

Ni muhimu kwa wananchi na wadau mbalimbali kutembelea maonesho hayo kwa kuwa yatawawezesha kufahamu masuala ya kimahakama ikiwa ni pamoja na Uandishi wa Wosia, Usimamizi wa Mirathi na huduma nyingine. 

Kaulimbiu ya Wiki na Siku ya Sheria ya mwaka huu 2024 ni “Umuhimu wa Dhana ya Haki kwa Ustawi wa Taifa: Nafasi ya Mahakama na Wadau Katika Kuboresha Mfumo Jumuishi wa Haki Jinai.”

Kilele cha Maonesho ya Wiki ya Sheria kitafanyika tarehe 1 Februari, 2024 katika Viwanja vya Chinangali jijini Dodoma ambapo Mgeni Rasmi anatarajiwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.


 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni