Na. Christopher Msagati – Mahakama, Manyara
Jaji
Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Manyara, Mhe. John Kahyoza jana
tarehe 3 Januari, 2024 amewaongoza wajumbe wa Chama cha Majaji na Mahakimu
Nchini (JMAT) na sehemu ya watumishi wa
Mahakama Kuu Kanda ya Manyara katika ziara ya kutoa mkono wa pole kwa waathirika
wa mafuriko yaliyotokea wilayani Hanang katika maeneo ya Katesh na Gendabi
mnamo tarehe 3 Desemba, 2023.
Ziara
hiyo iliyoandaliwa na Chama cha Majaji na Mahakimu Tanzania (JMAT) na watumishi
wa Mahakama Kuu Kanda ya Manyara kwa pamoja waliamua kwa hiari kuchanga fedha
ambazo ziliweza kununua mabati na misumari kwa ajili ya kusaidia kujenga nyumba
za waathirika wa mafuriko hayo.
Katika
kukabidhi vifaa hivyo Mhe. Kahyoza ambaye pia ni Rais wa JMAT alisema kuwa, Mahakama
miongoni mwa taasisi ambazo tunatoa huduma kwa watanzania, hivyo Mahakama
imeguswa sana na tukio hili ambalo limewapata wananchi wa maeneo hayo.
“Tumeona
kuwa siyo jambo jema kukaa kimya pasipo kutoa msaada miongoni mwa jamii
iliyoathirika na maafa haya. Huduma tunayotoa haiishii tu kwenye kutoa haki
bali hata kwenye masuala ya kijamii kama haya yanapojitokeza”, aliongeza Rais
wa JMAT.
Aidha,
Mkuu wa Wilaya ya Hanang Bi. Janeth Mayanja alimshukuru Mhe. Kahyoza na watumishi
wa Mahakama Kuu Kanda ya Manyara pamoja na JMAT kwa ujumla kwa kuguswa kwao na
tukio lililowapata wananchi wa Hanang.
“Tunawashukuru
sana Mahakama kwa kutukumbuka katika suala hili, kwa kweli tumefarijika sana na
tunawaahidi kuwa vitu hivi mlivyotupatia vitawasaidia walengwa wote kwa usahihi”,
alisema Mkuu wa Wilaya.
Katika
hatua nyingine, ujumbe huo kutoka Mahakama Kuu Kanda ya Manyara ikiongozwa na Mhe.
Kahyoza iliweza kutembelea katika eneo la Gendabi na kujionea madhara
yaliyojitokeza baada ya kutokea kwa mafuriko hayo ambayo yalisababisha vifo kwa
baadhi ya wananchi pamoja na uharibifu mkubwa wa mali na mindombinu.
Jaji
Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Manyara na Rais wa Chama cha
Majaji na Mahakimu Tanzania (JMAT) Mhe. John Kahyoza (wa pili kushoto) akikabidhi msaada wa
mabati kwa Katibu Tawala wa Wilaya ya Hanang Bw. Mwalimu Athumani (wa kwanza kushoto) jana tarehe 3 Januari, 2024
Rais
wa Chama cha Majaji na Mahakimu Tanzania (JMAT) na Jaji Mfawidhi wa Mahakama
Kuu, Kanda ya Manyara Mhe. John Kahyoza (wa nne kutoka kulia) akiwa kwenye
picha ya pamoja na Mkuu wa Wilaya ya Hanang Bi. Janeth Mayanja (wa tano kutoka kushoto)
na baadhi ya Watumishi wa Mahakama Kuu Kanda ya Manyara katika ziara ya kutoa
pole kwa wananchi wa Wilaya ya Hanang waliokumbwa na mafuriko.
Rais
wa Chama cha Majaji na Mahakimu Tanzania (JMAT) na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Manyara Mhe. John Kahyoza (wa
tatu kushoto) akiangalia madhara yaliyojitokeza katika eneo la Gendabi mara baada
ya kukumbwa na mafuriko.
Ujumbe
kutoka Mahakama Kuu Kanda ya Manyara wakiwa katika picha ya pamoja katika eneo
la Gendabi wilayani Hanang lililoathirika na mafuriko.
(Habari Hii Imehaririwa na Innocent Kansha - Mahakama)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni