Jumanne, 9 Januari 2024

WATUMISHI MAHAKAMA MOROGORO WAPIGWA MSASA MATUMIZI YA AKILI BANDIA

Na Evelina Odemba – Mahakama, Morogoro

 

Watumishi wa Mahakama katika Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki Morogoro hivi karibuni walipewa elimu ya namna ya kutumia mfumo wa Akili Bandia wakati wa usikilizaji wa mashauri.

 

Elimu hiyo ilitolewa na Mkurugenzi wa Mashauri wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Desdery Kamugisha ambaye alikuwa sehemu ya wawezeshaji kwa kushirikiana na Afisa toka Mahakama Kitengo cha Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA), Bw. Wittiness Ndeza.

 

Akizungumza wakati wa zoezi la utoaji elimu, Mhe. Kamugisha alisema kuwa baada ya elimu kutolewa wanategemea kuona Mahakama zilizofungwa vifaa zinaanza kutumia mfumo huo ambao unarahisisha usikilizaji wa mashauri na kupelekea utoaji wa haki kufanyika kwa wakati.

 

“Ofisi yetu ipo wazi kutoa msaada wa elimu ya mfumo huu kwa yeyote atakayekumbana na changamoto wakati wa matumizi yake, tuufanyie mazoezi lakini pia tuutumie katika usikilizaji wa mashauri,” alisisitiza.

 

Naye Kaimu Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Morogoro, Mhe. Hadija Kinyaka alitoa shukurani kwa wawezeshaji kwa kuwapatia elimu hiyo wezeshi na kuwataka watumishi walioshiriki kufanyia mazoezi mara kwa mara ili waweze kuwa wabobezi katika utumiaji wa mfumo huo.

 

“Naamini kwamba tumeelewa sana, tunachohitaji zaidi ni mazoezi kwa kuwa vitu hivi vya mifumo vinahitaji kufanyia mazoezi, usipofanya hivyo ni rahisi kusahau. Changamoto zozote tutakazokabiliana nazo wakati wa mazoezi tuzichukue kama sehemu ya kujifunza,” alieleza Mhe. Kinyaka.

 

Elimu hiyo ilitolewa kwa Majaji, Naibu Wasajili, Mahakimu, Maafisa TEHAMA, Wasaidizi wa Kumbukumbu, Waandishi na Waendesha Ofisi wanaohudumia ofisi ya Majaji ambao kwa pamoja waliweza kupata ujuzi wa namna ya kuutumia mfumo huo.

 

Mafunzo hayo ya matumizi ya Akili Bandia yamefanyika kwa awamu ya pili ambapo katika awamu ya kwanza iliyofanyika mwishoni mwa mwaka 2022 iligusia namna ya kuutumia mfumo huo kunakili sauti ya kila kilichozungumzwa mahakamani wakati wa usikilizaji wa mashauri.

Awamu hii ya pili ilihusisha namna ya kuutumia mfumo huo kunakili sauti na kubadili sauti zilizonakiliwa kuzipeleka katika maandishi. 

 

 

Kaimu Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Morogoro, Mhe. Hadija Kinyaka akifuatilia mafunzo ya matumizi wa mfumo wa Akili Bandia.


Mkurugenzi wa Mashauri wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Desdery Kamugisha akitoa elimu kwa watumishi wa Mahakama Kanda ya Morogoro juu ya matumizi ya mfumo wa Akili Bandia katika usikilizaji wa mashauri.

Naibu Wasajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Morogoro, Mhe. Fadhili Mbelwa (kulia) na Mhe. Susan Kihawa (kushoto) wakifuatilia mafunzo.

 

Afisa TEHAMA toka Mahakama ya Tanzania, Bw. Wittiness Ndeza akitoa elimu kwa watumishi wa Mahakama Kanda ya Morogoro juu ya matumizi ya mfumo wa Akili bandia.

Watumishi wakifuatilia elimu (juu na chini).



Watumishi wa Mahakama wakifanya mazoezi kwa vitendo namna ya matumizi ya mfumo wa Akili Bandia unavyofanya kazi wakati wa usikilizaji wa mashauri.

 

Mkurugenzi wa Mashauri wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Desdery Kamugisha akionesha namna sauti zinavyonakiliwa kwenye mfumo wakati akitoa  elimu kwa watumishi wa Mahakama Kanda ya Morogoro juu ya matumizi ya mfumo wa Akili Bandia katika usikilizaji wa mashauri.

(Habari hii imehaririwa na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Dar es Salaam)



 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni