Na Stephen Kapiga-Mahakama Mwanza
Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Mwanza, Mhe. Dkt. Ntemi Kilekamajenga amewaongoza watumishi mbalimbali wa Kanda hiyo katika zoezi la upandaji miti ndani ya eneo la Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki Jijini humo.
Akizindua zoezi hilo jana tarehe 29 Januari, 2024, Mhe. Dkt. Kilakemajenga aliwasihi watumishi wote kuwa na kawaida ya kupenda mazingira hata wawapo majumbani kwao kwani hii itasaidia hata vizazi vyao pia kupenda mazingira katika maeneo yanayowazunguka.
“Nawasihi ndugu zangu tuwe na jadi ya kupanda miti kwani mbali ya kuwa miti ndio chanzo cha hewa nzuri ya oksijeni pia hutupatia vivuli na faida nyingi ikitegemeana na aina ya miti, mfano hapa ‘IJC’ tumepanda miti ya matunda kwa hiyo ni mategemeo yangu kuwa baada ya miaka miwili kila mmoja wetu atakula tunda kutoka katika mti alioupanda leo” alisema Mhe Jaji, Dkt. Kilekamajenga.
Kwa upande mwingine watumishi walimpongeza Jaji Mfawidhi kwa kuweza kuwahamasisha na kufanikisha zoezi hilo ambalo lilikuwa na muitikio mkubwa kwa watumishi hao.
“Kwa kweli ni hamasa kubwa sana kwetu kama watumishi kuweza kushiriki zoezi hili na pia ukizingatia changamoto kuhakikisha kila mmoja wetu anautunza mti wake, kwa upande wangu imenipa moyo sana ukizingatia kama, Mfawidhi yupo tayari kuutunza mti wake na kuhakikisha unakuwa na kuzaa matunda sasa mimi ni nani nishindwe kutimiza hilo” alisema Bwana Sweertber Kasosa.
Hii imekuwa ni kawaida kwa watumishi wa Kanda hiyo kuwa na zoezi hilo kila mwaka wa Wiki wa Sheria na hivyo, kuendelea kulipendezesha eneo la la Kituo hicho kwa uoto wa kijani kuweza kuonekana kwa wingi na hivyo kuweza hata kuwashawishi baadhi ya wananchi waishio Jirani na jengo hilo nao kuwa na kawaida ya upandaji miti katika maeneo yao.
Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Mwanza, Mhe. Dkt Ntemi Kilekamajenga akiwaongoza watumishi mbalimbali wa Kanda katika zoezi la upandaji miti ndani ya eneo la kituo Jumuishi cha Utoaji Haki jijini Mwanza. Zoezi hilo lilifanyika jana tarehe 29 Januari, 2024.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni