Na. Evelina Odemba – Mahakama Morogoro
Mahakama Kuu Kituo Jumuishi cha utoaji haki mkoani Marogoro kwa kushirikiana na wadau wameendelea kutoa elimu katika maeneo mbalimbali ya mji huo ili kuhakikisha wanawafikia wananchi wengi zaidi katika kipindi hiki cha maadhimisho ya wiki ya sheria nchini.
Akizungumza na waandishi wa Habari Mratibu wa kamati ya elimu ambaye ni Hakimu Mkazi Mfawidhi Mahakama ya Hakimu Mkazi Morogoro Mhe. Asha Waziri alisema, wamejipanga vyema kuwafikia wananchi wa Mkoa wa Morogoro na kutoa elimu ya sheria kwa kushirikiana na wadau wa Mahakama.
“Tayari mwitikio ni mkubwa kwakuwa wananchi mbalimbali wanajitokeza kupata elimu hiyo na pia mrejesho kutoka kona mbalimbali za Morogoro unadhihirisha namna ambavyo wananchi walikuwa na kiu ya elimu hiyo”, alisema Mhe. Waziri.
Mhe. Waziri amebainisha maeneo yaliyofikiwa na mada
zilizotolewa kama vile Mabanda ya kutolea elimu yaliyopo standi ya zamani ya Daladala,
Shule, Vyuo, Magereza, pamoja na kutumia vyombo vya Habari kutoa mada
mbalimbali zilizofundishwa ikiwemo ukatili wa kijinsia, matumizi mabaya ya dawa
za kulevya, migogoro ya wakulima na wafugaji, makosa dhidi ya wanyamapori
ambapo wananchi walipata fursa ya kujifunza na kuuliza maswali na kupatiwa majibu.
Kwa upande wa Mahakama ya Wilaya Gairo Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya ya Gairo Mhe. Irene Lyatuu anaeleza kuwa wananchi wa Wilaya hiyo wamepatiwa elimu na mwitiko wao ni mkubwa tangu siku ya uzinduzi mpaka sasa maonesho yanapoelekea kuhitimishwa.
“Nipende kutoa shukurani zangu kwa kuwa tumepata ushirikiano
wa kutosha toka kwa viongozi wa Selikari wilayani wikiongozwa na Mkuu wa Wilaya
Mhe. Makame Jabir, wadau pamoja na wananchi na kufanikiwa kutoa elimu katika
maeneo kadhaa kama vile kwenye Masoko, Shule na Vitu vya Mabasi,” alieleza Mhe.
Lyatuu.
Naye, Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya ya
Malinyi Mhe. Samuel Obasi
anaeleza kuwa elimu ya sheria katika kipindi hiki cha maadhimisho wameweza
kufika sehemu mbalimbali kutoa elimu ikiwemo shule za msingi na sekondari.
“Wito wangu wananchi wasisite kuuliza maswali
mbalimbali yanayohusu Mahakama na wataweza kujibiwa vyema, wadau na watumishi
wa Mahakama wanaendelea kufanya vyema” alieleza Mhe. Obasi.
Nako
Wilaya ya
Ulanga Hakimu Mkazi
Mfawidhi wa Wilaya hiyo Mhe. Christopher Bwakila anaeleza kuwa licha ya kutoa
elimu kwenye stendi za magari, mashuleni na sokoni pia wameweza kutoa elimu
kupitia vyombo vya Habari ikiwemo Ulanga Fm.
“Niwasilishe pongezi zangu kwa uongozi wa Mahakama
Kanda ya Morogoro na Mahakama ya Tanzania kutoka kwa wadau kwa ushirikiano
mkubwa wanaoupata toka Mahakama na kuongeza kuwa elimu itaendelea kutolewa hadi
siku maadhimisho haya yatakapofungwa rasmi,” alisema Mhe. Bwakila.
Sanjali na Mahakama ya Wilaya ya Kilombero nayo iliungana na Mahakama kote nchini katika
maadhimisho ya wiki ya sheria kwa mwaka 2024, Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama
ya Wilaya Kilombero Mhe. Regina Futakamba anasema kuwa wametoa elimu ya masuala
ya jinsia mashuleni pamoja na kwenye radio iliyoko Wilayani humo.
Alikadhalika Mahakama ya Wilaya ya Mvomero Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya Mvomero
Mhe. Antony Ngowi anaeleza kuwa kwa kushirikiana na wadau wameweza kutoa elimu katika
shule za msingi na sekondari, kwenye mabanda ya huduma za kisheria, sokoni,
mnadani, turiani na soko la Mtibwa.
“Ni furaha yetu kuwa kila tulipokuwa tunafika kiu ya watu kutaka kujua masuala ya kiheria kwa undani zaidi ilikuwa kubwa na hata wengine walidiriki kutusimamisha na kuomba ufafanuzi zaidi” anaeleza Mhe. Ngowi.
Kwa upande wa Mahakama ya Wilaya ya Kilosa Hakimu Mkazi Mfawidhi Mahakama ya Wilaya Kilosa Mhe. Agnes Ringo anasema, wamefanikiwa kutoa elimu katika maeneo mbalimbali wilayani humo na miongozi mwa mada zilizofundishwa ni elimu kuhusu migogoro ya Ardhi.
“Tumefanikiwa kuwaelimisha wananchi juu ya masuala ya migogoro ya ardhi, elimu hii ilitolewa na Mahakama kwa kushirikiana na Mwenyekiti wa Baraza la Nyumba na Ardhi, tumefanya hivi kwakuwa miongoni mwa kesi nyingi zinazotufikia mahakamani zinatokana ama zinahusu masuala ya Ardhi” alisisitiza Mhe. Ringo.
Mratibu wa kamati ya elimu Mahakama Kuu Kanda ya Morogoro ambaye ni
Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Morogoro Mhe. Asha Waziri
akitoa elimu ya sheria kwa mwananchi aliyekaa kushoto.
Sehemu ya wananchi wakijipatia elimu katika mabanda ya Mahakama katika
viwanja vya stendi ya daladala ya zamani iliyoko Morogoro mjini
Maonesho ya vifaa vya zima moto na uokoaji katika maadhimisho ya wiki ya
sheria 2024
Wa tatu kushoto ni Mkuu wa Wilaya ya Gairo Mhe. Jabir Makame kulia kwake
ni Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya ya Gairo Mhe. Irene Lyatuu
wakiongoza mamia ya wananchi wa Gairo kwenye matembezi ya uzinduzi wa wiki ya
sheria
Mhe. Irene Lyatuu Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya Gairo
akitoa zawadi kwa mshindi wa michezo ya bonanza katika maadhimisho ya wiki ya
sheria.
Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Wilaya ya Ulanga Mhe. Christopher
Bwakila akitoa elimu katika maadhimisho ya wiki ya sheria.
Wanafunzi wa shule ya Sekondari Nawenge iliyoko Wilayani Ulanga
wakifuatilia elimu kutoka kwa wawezeshaji(hawapo pichani) katika maadhimisho ya
wiki ya sheria.
Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya ya Kilombero Mhe.regina
Futakamba (kushoto) akiongoza wataalamu katika Utoaji wa elimu kupitia redio katika maadhimisho ya wiki ya sheria.
Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Mhe. Agnes Ringo (wa
pili kulia) akiweka mambo sawa na mlinda amani muda mfupi kabla ya kuanzwa kwa
matembezi ya uzinduzi wa wiki ya sheria Wilayani humo.
Muwezeshaji toka baraza la ardhi na Nyumba (mwenye suti nyeusi) akiwa katika
picha ya Pamoja na wananchi wa Wilaya ya Kilosa mara baada ya kumaliza kutoa
elimu.
Wataalamu toka Mahakama ya Wilaya ya Mvomero wakitoa elimu ya sheria
mnadani katika maadhimisho ya wiki ya sheria.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni