·Jaji Mfawidhi aonesha kwa vitendo usajili, upangaji mashauri kielekroniki
Na Seth Kazimoto – Mahakama Kuu Arusha.
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Arusha, Mhe. Joachim Tiganga amewaalika wananchi wote mkoani hapa kujitokeza kwa wingi katika maonesho ya Wiki ya Sheria ili kujifunza mambo mbalimbali katika masuala yote yanayohusiana na utoaji haki.
Mhe. Tiganga ametoa wito huo jana tarehe 24 Januari, 2024 katika viwanja vya Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) wakati akizungumza na wananchi na wadau wa Mahakama waliofika viwanjani hapo kuanza maadhimisho ya Wiki na Siku ya Sheria Tanzania kwa mwaka 2024.
Jaji Mfawidhi alibainisha kuwa wakati wa maadhimisho hayo wananchi watapata fursa ya kuzungumza, kuuliza maswali na kujadiliana na maafisa wa Mahakama na wadau wake kwa lengo la kujifunza kuhusu huduma mbalimbali zinazotolewa na Mahakama na wadau.
Mhe. Tiganga ametaja kauli mbiu itakayoongoza maadhimisho hayo inayosema, “Umuhimu wa Dhana ya Haki kwa Ustawi wa Taifa: Nafasi ya Mahakama na Wadau Katika Kuboresha Mfumo Jumuishi wa Haki Jinai.”
Alisema ni muhimu wananchi kutembelea maonesho hayo kwa kuwa yatawawezesha kufahamu masuala mbalimbali ya kimahakama ikiwemo yale yanayohusiana na ardhi, umuhimu wa wa wosia, usimamizi wa mirathi, haki za watoto na huduma nyingine.
Wadau wanaoshiriki katika maonesho hayo yanayofanyika hadi tarehe 30 Januari, 2024 kuwa ni na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali, Ofisi ya Taifa ya Mashtaka, Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), Chama cha Wanasheria Wanawake Tanzania (TAWLA) na Chama cha Mawakili cha Tanganyika (TLS).
Wengine ni Chama cha Wanawake cha Msaada wa Kisheria na Haki za Binadamu Arusha (AWLAHURIO), Chama cha Majaji na Mahakimu Wanawake Tanzania (TAWJA), Kikosi Dhidi ya Ujangili (KDU), Madalali wa Mahakama, Mfuko wa Ukwasi na Kujikimu (UTT AMIS), Tume ya Usuluhishi na Uamuzi (CMA) na Idara ya Huduma za Uangalizi Adhabu Mbadala wa Kifungo.
Aidha, Jaji Mfawidhi alitembelea mabanda ya wadau wote wanaoshiriki maonesho hayo na kusaini vitabu vya wageni. Akiwa katika Banda la Mahakama, Mhe. Tiganga alipewa maelezo toka kwa Hakimu Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha, Mhe. Erasto Philly na Afisa Tehama, Bi. Rehema Awet, juu ya mifumo ya kitehama inayotumika mahakamani.
Mhe. Tiganga ameshiriki kuonesha namna mashauri yanvyosajiliwa kielektroniki na kusajili mashauri mawili na kuyapanga kwa Majaji akiwa katika banda la Mahakama.
Naye Naibu Msajili wa Mahakama Kuu Kanda ya Arusha, Mhe. Fredrick Lukuna alitaja shughuli zitakazofanyika wakati wa Wiki ya Sheria kama kutembelea Ofisi za Serikali, Shule na Taasisi mbalimbali kwa lengo la kutoa elimu ya sheria juu ya mambo mbalimbali, kufanya maonesho ya sheria kupitia mabanda yaliyopo katika viwanja vya TBA na katika Mahakama ya Mwanzo Arusha Mjini.
Kadhalika, wamepanga kutumia Radio zilizopo mkoani Arusha kuelimisha wananchi, kufanya bonanza la michezo litakalohusisha wadau wa Mahakama, wakiwemo Mawakili na Jeshi la Polisi. Michezo itakayochezwa ni pamoja na mpira wa miguu, mpira wa pete, kuvuta Kamba na kukimbiza kuku.
Mhe. Lukuna alibainisha kuwa maadhimisho ya Wiki ya Sheria yatazinduliwa rasmi kwa matembezi maalum yatakayofanyika tarehe 27 Januari, 2024 kuanzia Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki-Arusha hadi Viwanja vya TBA mkoani Arusha, na kilele cha Maonesho ya Wiki ya Sheria kitafanyika Februari 1, 2024 Mahakama Kuu Arusha ambapo Mgeni Rasmi anatarajiwa kuwa Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mhe. John Mongela.
Mwananchi aliyetembelea banda la Chama cha Mawakili wa Kujitegemea (TLS) akihudumiwa kikamilifu katika Maadhimisho ya Wiki ya Sheria yaliyoanza jana tarehe 24 Januari, 2024 katika Viwanja vya TBA mkoani Arusha.
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Arusha, Mhe. Joachim Tiganga (kushoto) akitoa elimu ya sheria kwa wananchi kupitia Radio 5 wakati wa Wiki ya Sheria Tanzania 2024. Alioambatana nao ni Wakili Mkuu wa Serikali Mkoa wa Arusha, Bw. Peter Museti (katikati) na Mwenyekiti wa Chama cha Mawakili (TLS) Mkoa wa Arusha, Bw. George Njooka (kulia).
(Habari hii imehaririwa na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Dodoma)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni