Na.
Evelina Odemba – Mahakama, Morogoro
Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Morogoro leo Tarehe
27 Januari, 2024 imefanya uzinduzi wa maadhimisho ya wiki ya sheria kwa
matembezi makubwa yaliyowajumuisha mamia ya wakazi wa Morogoro.
Sherehe ya Uzinduzi ilianzia kwa matembezi katika Kituo
Jumuishi cha Utoaji Haki Morogoro hadi ilipo stendi ya zamani ya Dalala
Morogoro Mjini. Matembezi hayo yaliongozwa na Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Adam
Maliama sanjali na mwenyeji wake ambaye ni Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya
Tanzania Kanda ya Morogoro Mhe. Latifa Mansoor ambaye aliambatana na Majaji wa
Mahakama Kuu Kanda ya Morogoro Mhe. Devotha Kamzola na Mhe. Hadija Kinyaka.
Akizungumza wakati wa kufungua maazimisho hayo Mkuu wa
Mkoa wa Morogoro Mhe. Adam Malima alitoa pongezi kwa Mahakama ya Tanzania kwa
kuwa na kauli mbiu inayoendana na wakati wa sasa kwakuwa mfumo wa haki ni shirikishi
kwa Mahakama na wadau.
“Kauli mbiu hii itasaidia kuleta taifa linalojali utu,
usawa na haki na ikizingatiwa kuwa suala la haki limezungumzwa mahali pengi
katika vitabu vitakatifu mmekuwa na jitihada nzuri sana katika kupeleka ujumbe kwa
jamii kupitia kauli mbiu mbalimbali mnazozitoa katika vipindi vya wiki ya
sheria, pia nimefurahishwa baada ya kupata taarifa kuwa mmeipandisha kauli mbiu
hii ya wiki ya sheria kileleni, hongereni sana,” alisema Mgeni rasmi Mhe.
Malima.
Alitoa rai yake kwa wananchi wa mkoa wa Morogoro kusogea
katika mabanda ya maonesho ili waweze kujifunza mambo ambayo mahakama imeandaa
kwa ajili yao katika mwaka huu wa 2024.
“Tuwasaidie wadau kupitia mifumo mbalimbali ya mahakama
inatusaidia kujua mahakama zetu na huduma zinazotolewa na mahakama, kwahiyo niwapongeze
sana kwa maboresho makubwa ya Mahakama upande wa TEHAMA kwakuwa mmeturahisishia
huduma ya haki sanjari na kumtambua wakili na kishoka kwa kupitia mfumo wa E-
wakili.
Akizungumza na vyombo vya Habari mara baada ya
maadhimisho uzinduzi wa wiki ya sheria Mhe. Mansoor alisema kuwa huu ni uwanda
wa wananchi kusogea katika mabanda ya kutolea elimu ili waweze kujifunza na
kupata uelewa wa sheria na namna ambavyo Mahakama inafanya kazi ikishirikiana
na wadau wake na pia namna matumizi ya TEHAMA yanaweza kuwasaidia kupunguza
gharama za kutembea ili kuisogelea huduma ya Mahakama.
“Mwananchi afike hapa apewe elimu na atapata uelewa wa
namna kesi inavyopokelewa mpaka kufika Mahakamani na hata inapomalizika
Aidha, katika ufunguzi huo wasanii mbalimbali waliburudisha
akiwemo Afande Sele, Tabu Mtingita, Mau Fundi na Dulla Makabila Pamoja na watumishi
wa Mahakama, wadau, wananchi na wanafunzi baada ya ufunguzi huo pia walipata
nafasi ya kupanda miti katika mto Mindu ikiwa ni sehemu ya kuunga jitihada za
serikali katika kutunza Mazingira ambapo miti zaidi ya mia tatu imepandwa.
Maadhimisho ya wiki ya sheria yanatarajiwa kuhitimishwa tarehe 30 Januari, 2024 na kilele chake kinatarajiwa kuwa tarehe 1 Februari,2024 na kauli mbiu yake ni “Umuhimu wa dhana ya haki kwa ustawi wa Taifa:Mahakama na Wadau katika kuboresha mfumo jumuishi wa haki Jinai”
Mgeni
rasmi Mkuu wa Mko awa Morogoro Mhe. Adam Malima akizungumza wakati hafla akizindua wiki
ya sheria leo tarehe 27 Januari, 2024.
Jaji
Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Morogoro Mhe. Latifa Mansoor
akizungumza wakati akimkaribisha Mgeni Rasmi kuzindua wiki ya sheria.
Majaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Morogoro wakiwa wameketi meza
kuu kushoto ni Mhe. Devotha Kamzola na kulia ni Jaji Mhe. Hadijah
Kinyaka wakifuatilia
sherehe za uzinduzi wa wiki ya sheria
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Morogoro
Mhe. Latifa Mansoor akitoa zawadi wa msanii afande Sele wakati akitumbuiza.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni