Jumamosi, 27 Januari 2024

UFUNGUZI WIKI YA SHERIA WATANDA KILA KONA

Maadhimisho ya Wiki ya Sheria yamefunguliwa rasmi nchini kote leo tarehe 27 Januari, 2024, huku wananchi katika Mikoa mbalimbali wakijitokeza kwa wingi kushiriki katika matembezi maalum yaliyoongozwa na Viongozi mbalimbali.

Kutoka Mahakama Musoma, Mwandishi Wetu Francisca Swai anaripoti kuwa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Musoma imefungua rasmi maadhimisho ya Wiki ya Sheria kwa kuanza na matembezi yaliyoongozwa na Mkuu wa Mkoa wa Mara, Mhe. Said Mtanda akiambatana na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Musoma, Mhe. Fahamu Mtulya.

Matembezi hayo yameanzia katika Viwanja vya Mahakama ya Wilaya Musoma kuelekea Uwanja wa Shule ya Msingi Mukendo ambapo watumishi na wadau walipata fursa ya kusikiliza hotuba kutoka kwa Viongozi hao.

Akizungumza wakati wa ufunguzi huo, Jaji Mfawidhi amesema leo ni siku muhimu kwa Mahakama na Wadau wake ambapo Wiki ya Sheria huwawezesha hukutana na kuwahudumia wananchi kwa kuwapa msaada wa kisheria na elimu mbalimbali za kisheria bure.

Mhe. Mtulya amesema ‘‘Msingi wa maendeleo na ustawi wa jamii ni amani na hakuna amani pasipo haki. Hivyo, kwa kutambua jambo hili, Mahakama kwa mwaka huu imejikita katika haki jinai inayoanzia kwa mwanachi wa kawaida ambao Mahakama inataka kuwafikia katika Wiki ya Sheria,” amesema.

Jaji Mfawidhi ameeleza kuwa jinai nyingi zinafanywa katika mazingira ya kawaida ambapo huanza na mwananchi anayeshuhudia tukio, vyombo vyote vya Serikali vitakavyohusika katika uchunguzi hadi kufikia ushahidi mahakamani. 

“Ili Mahakama iweze kufikia maamuzi ya haki hujumuisha wadau ambao ndio wamelengwa. Wadau wote hawa ndio msingi wa kauli mbiu yetu mwaka huu isemayo Umuhimu wa dhana ya haki kwa ustawi wa Taifa: Nafasi ya Mahakama na wadau katika kuboresha mfumo jumuishi wa haki Jinai,” amesema.

Naye Mkuu wa Mkoa wa Mara amesema kauli mbiu ya mwaka huu 2024 inaonesha mustakabali wa haki jinai katika nchi yetu, hivyo maendeleo na ustawi wa Taifa yanategemea uwepo wa   amani, usalama na utulivu ambavyo vyote hiyo vinategemewa na uwepo wa haki katika jamii. 

“Mfumo wa haki jinai unarahisiha upatikanaji wa haki kwa wakati, hivyo wananchi watapata muda mwingi wa kufanya shughuli zao za kiuchumi na kijamii kuleta ustawi wa Taifa kwa ujumla. Ili kulitekeleza hili, Mahakama inashirikiana na wadau wa haki jinai kama Polisi, Mashtaka, Takukuru na wengine,” amesema.

Katika ufunguzi huo, Viongozi mbalimbali wa Mahakama na Serikali ya Mkoa wa Mara walipata nafasi ya kutembelea mabanda yaliyoandaliwa kwa ajili ya utoaji elimu na kujionea namna Mahakama na Wadau wake walivyojipanga vyema katika zoezi hilo.




Mkuu wa Mkoa wa Mara, Mhe. Said Mtanda akiongea na watumishi na wadau wa Mahakama (hawako pichani) waliohudhuria ufunguzi wa maonesho ya Wiki ya Sheria katika uwanja wa Shule ya Msingi Mukendo Musoma Mjini.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Musoma, Mhe. Fahamu Mtulya akiongea na watumishi na wadau wa Mahakama (hawako pichani) waliohudhuria ufunguzi wa maonesho ya Wiki ya Sheria katika uwanja wa Shule ya Msingi Mukendo Musoma Mjini.

Mkuu wa Mkoa wa Mara, Mhe. Said Mtanda (wa pili kushoto) na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Musoma, Mhe. Fahamu Mtulya (wa tatu kulia) wakiwa na Viongozi, watumishi na wadau wa Mahakama Kanda ya Musoma katika matembezi ya amani kuashiria uzinduzi wa Wiki ya Sheria nchini.

Viongozi, watumishi na wadau wa Mahakama Kanda ya Musoma wakifuatilia kwa makini hotuba za Viongozi katika uzinduzi wa Wiki ya Sheria.

Meza Kuu, Mkuu wa Mkoa wa Mara, Mhe. Said Mtanda (katikati), Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Musoma, Mhe. Fahamu Mtulya (wa pili kushoto), Jaji wa Mahakama Kuu Musoma, Mhe. Marlin Komba (wa pili kulia), Jaji wa Mahakama Kuu Musoma, Mhe. Kamazima Idd (wa kwanza kushoto), Mkuu wa Wilaya Musoma, Mhe. Halfan Haule (wa kwanza kulia) pamoja na Viongozi wa Mahakama na Taasisi mbalimbali katika ufunguzi wa Wiki ya Sheria.

Mkuu wa Mkoa wa Mara, Mhe. Said Mtanda (wa pili kulia), Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Musoma, Mhe. Fahamu Mtulya (wa tatu kulia) wakisikiliza kwa makini maelezo ya mtafsiri wa lugha ya alama, Bw. Novatus Mjalifu (wa kwanza kulia) aliyekuwa akitafsiri maelezo, maswali na majibu kati ya Viongozi hao na kundi la watu wenye ulemavu wa kusikia waliohudhuria katika hafla hiyo.

 Naye Aidan Robert kutoka Mahakama Kigoma anaripoti kuwa leo tarehe 27 Januari, 2024, Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Mhe. Thobias Andengenye, ambaye alikuwa Mgeni Rasmi ameongoza mamia ya wananchi na wadau wa Mahakama katika matembezi ya ufunguzi wa Wiki ya Sheria mkoani hapo.

Matembezi hayo yameanzia Viwanja vya Mahakama Kuu Kigoma na kuelekea katika Viwanja vya Mwanga Community Centre, ambako kuna mabanda ya wadau mbalimbali ambayo yameandaliwa kwa ajili ya kutolea elimu ya sheria iliyoanza toka tarehe 24 Januari, 2024.

Akizungumza baada ya matembezi hayo, Mkuu wa Mkoa ameelezea kufurahishwa na kauli mbiu ya mwaka huu 2024 inayosema,‘Umuhimu wa dhana ya haki kwa ustawi wa Taifa nafasi ya Mahakama na wadau katika kuboresha mfumo jumuishi wa haki jinai.’ 

Amesema kuwa haki ni nguzo kubwa katika ustawi wa Taifa la Tanzania, na kunukuu toka katika maandiko Matakatifu ya Biblia toka katika Kitabu cha Methari:14:34, ambacho kinasema, “Haki huinua Taifa bali dhambi ni aibu ya watu wote.’

Mhe. Andengenye ameipongeza Mahakama ya Tanzania kwa maboresho makubwa ya kiteknolojia ambayo yamekuja kurahisisha shughuli za Mahakama kwa kiasi kikubwa kwa maendeleo ya Taifa.

Kadhalika, amempongeza Rais wa Jamhuri ya Mungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuisaidia Mahakama kuboresha haki ambayo imeleta majawabu makubwa katika kutoa haki kwa wananchi.

Naye Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Kigoma, Mhe. Augustine Rwizile, akiwakaribisha wadau na wananchi kwa ujumla, amesema kwa kawaida Mahakama ya Tanzania huenda likizo na kabla ya shughuli zake huanza na maadhimisho ya Wiki ya Sheria.

Amesema kuwa katika kipindi hicho, Mahakama hushiriki na wadau kwa ujumla ili kupokea mrejesho wa masuala mbalimbali toka kwa wananchi ili Mahakama iweze kuwa karibu nao.

Mahakama imeungana na wadau wake kuadhimisha ufunguzi wa Wiki ya Sheria wakiwemo Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali, Ofisi ya Taifa ya Mashataka, Jeshi la Zimamoto na Uokoaji, Jeshi la Kujenga Taifa, Jukwa la Mawakili wa Kujitegemea, Jukwaa la Polisi Wanawake Tanzania, Baraza la Ardhi na Nyumba Wilaya, Baraza la Usuluhishi na Uamuzi, Jeshi la Magereza, Kitengo cha Damu Salama, Kitengo cha Lishe Bora, Taasisi ya Kuzuia na Kipambana na Rushwa, Mamlaka ya Hifadhi Gombe na wengine.



Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Kigoma, Mhe. Augustine Rwizile akizungumza wakati wa maadhimisho hayo.

Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Mhe. Thobias Andengenye akizungumza wakati wa ufunguzi wa Wiki ya Sheria katika viwanja vya Community Centre Mwanga Kigoma.


Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Mhe. Thobias Andengenye (kushoto) akiongoza matembezi ya ufunguzi wa Wiki ya Sheria mkoani Kigoma. Wengine katika picha ni Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Kigoma, Mhe. Augustine Rwizile na Mkuu wa Wilaya ya Kigoma, Mhe. Sallum Kally na nyuma yao ni wadau na wananchi waliojitokeza katika matembezi hayo.

Picha ya maandamano ya wadau na wananchi waliojitokeza katika matembezi.

Picha ya watumishi wa Mahakama na wadau wakisikiliza kwa makini hotuba ya Mgeni Rasmi.

Kutoka Mahakama Kuu Moshi, Mwandishi Wetu Paul Pascal anaeleza kuwa Mahakama Kuu Kanda ya Moshi imefanya ufunguzi wa Wiki ya Sheria ikiwa ni utamaduni ambao Mahakama ya Tanzania imejiwekea kila mwaka kabla ya kuanza shughuli rasmi za Mahakama kwa mwaka husika.

Akizungumza wakati wa kufungua maadhimisho hayo, Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Mhe. Nurdin Babu, ambaye alikuwa Mgeni Rasmi ameiomba Mahakama pamoja na wadau wake hutumia muda huo kutoa elimu kwa umma juu ya jukumu zima la utoaji haki nchini, kutoa msaada wa kisheria, kusikiliza kero na kupokea maoni mbalimbali kutoka kwa wananchi kuhusu huduma nzima ya utoaji haki na utendaji wa shughuli za kimahakama. 

“Hii husaidia wananchi kutambua haki zao za kisheria na taratibu za kimahakama. Vile vile, maadhimisho haya yanalenga kuwajengea uelewa wananchi wote juu ya uendeshaji wa mashauri mahakamani,” amesema. 

Amebainisha pia kuwa Mahakama imekuwa ikitoa kauli mbiu mbalimbali kila mwaka kwa ajili ya maadhamisho ya Wiki na Siku ya Sheria ambayo kwa mwaka huu 2024 inasema, “Umuhimu wa Dhana ya Haki kwa Ustawi wa Taifa: Nafasi ya Mahakama na Wadau katika Kuboresha Mfumo Jumuishi wa Haki Jinai.”

“Pamoja na kuwa kila mmoja wetu anaweza kutafsiri haki kwa namna yake lakini kwa tafsiri ya kawaida haki ni jambo ambalo mtu anastahiki au kitu anachostahili kuwa nacho,” amesema. 

Naye Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Moshi, Mhe. Dkt Lilian Mongella amewahakikishia wananchi wote kuwa Mahakama na wadau wake wako tayari kuwahudumia wakati wote wa maadhimisho hayo na hata baada ya hapo, kwani bado wanayo nafasi ya kufikisha kero, malalamiko na maoni yao kwenye madawati maalum ambayo yapo katika kila Mahakama. 

Wiki ya Sheria kwa Mahakama Kanda ya Moshi imeanza kutekelezwa kuanzia tarehe 24 Januari, 2024 kwa kutoa elimu sehemu za Mkoa wa Kilimanjaro kwenye mabanda yaliyopo kwenye Viwanja vya Mahakama Kuu Moshi, mashule, vyuoni, kwenye masoko, viwandani, vituo vya mabasi, nyumba za ibada na vyombo vya habari kwa lengo la kufikisha elimu ya masuala mbalimbali ya kisheria kwa wananchi.






(Habari hii imehaririwa na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Dodoma)

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni