Na. Eunice Lugiana- Mahakama, Pwani
Katibu tawala wa Wilaya ya Kibaha Mhe. Moses Magogwa ameipogeza Mahakama kwa jitihada zinazochukuliwa kuimarisha huduma ya utoaji haki kwa wananchi kwani kasi ya kusikiliza mashauri imeongezeka sana katika ngazi zote za Mahakama.
Akizungumza mapema leo tarehe 27 Januari, 2024 katika hafla ya uzinduzi wa wiki ya sheria nchini iliyoadhimishwa kimkoa katika Wilaya ya Kibaha Mhe. Magogwa amesema ukiisikiliza na kuielewa kauli mbiu ya wiki ya sheria utaona kabisa imetoa nafasi kwa tasisi za haki jinai kutafakali maoni na mapendekezo ya tume ya Rais kuangalia jinsi ya kuboresha tasisi za haki jinai.
“Tunaipongeza sana Mahakama maana tumeona kuna mapinduzi mkubwa sana katika ushughulikiaji wa mashauri kwa haraka na pia unasaidia kupunguza msongamano magereza” amesema katibu Tawala huyo.
Naye, Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Pwani Mhe. Joyce Mkhoi amesema katika wiki ya sheria Mahakama inapata nafasi ya kuuelimisha umma na wananchi wote taratibu za msingi za kimahakama zikiwemo ufunguaji wa mashauri kwa njia ya mtandao kwa mahakama ya Wilaya na Hakimu Mkazi na kwa njia ya kawaida kwa Mahakam za mwanzo.
Aidha, Mhe Mkhoi amesema, utoaji wa elimu kupitia mada zilizotangulia kwa umma na utoaji wa maoni, kero na uibuaji wa changamoto kutoka kwa wananchi, kumewezesha Mahakama kuweza kijitathimini katika utendaji kazi wake kupitia changamoto hizo kuendelea kuboresha utendaji kazi kwa kuimarisha miundombinu na kufanya kazi kwa bidii.
Mhe Mkhoi amesema maadhimisho ya siku ya sheria yamekua yakitumika kujadili maudhui kulingana na mwelekeo wa dunia na nchi katika kuelekea kwe ya mifumo ya kiteknolojia, hii inajidhihirisha wazi kwa kauli mbiu ya mwaka huu ambayo inatokana na mapungufu yanayopelekea malalamiko kutoka kwa wananchi kuhusiana na mfumo wa haki jinai.
“Mapungufu haya yamepelekea Rais wetu Mhe. Samia Suluhu Hassan kuunda tume ya kukusanya maoni na mapendekezo ya namna bora ya kuboresha mfumo wa haki jinai. Tume hiyo iliweza kukamilisha shughuli yake na katika moja ya mapendekezo ya tume hiyo ndiyo imepelekea uwepo wa kauli mbiu hii”, amesema Mhe. Mkhoi.
Uzinduzi huo ulitanguliwa na matembezi yalioanzia
katika viwanja vya Mahakama ya mwanzo Mlandizi kupitia kituo cha afya Malandizi
na kutokezea stend ya mabasi Mlandizi mpaka viwanja vya shule ya msingi
Mtongani Mlandizi. Maandamano hayo yameongozwa na bend ya JKT Mgulani.
Mwanasheria wa Takukuru Bi. Beatrice Ngogo akitoa Maelezo kwa Mgeni Rasmi Katibu Tawala Wa Wilaya Kibaha Mhe. Moses Magogwa na Meza Kuu.
Watuimishi Wa Mahakama Ya Hakimu Mkazi Kibaha mkoani Pwani Wakimsikiliza Mgeni Rasmi Katibu Tawala Wa Wilaya Kibaha Bw. Moses Magogwa (hayupo Pichani).
Watumishi Wa Mahakama Ya Hakimu Mkazi Kibaha Wakijiandaa Kuanza Matembezi Katika Viwanja Vya Mahakama Ya Mwanzo Mlandizi.
Bandi ya JKT Mgulani ikiongoza Matembezi ya Uzinduzi wa Wiki ya Sheria
Mgeni rasmi wa hafla ya uzinduzi wa wiki ya sheria Katibu Tawala Wa Wilaya Kibaha Mhe. Moses Magogwa (katikati) akiwa kwenye picha pamoja sehemu ya viongozi wa mahakama mkoa wa Pwani. Wengine ni Hakimu Mkazi Mfawidhi Wa Mahakam Ya Hakimu Mkazi Kibaha Pwani Mhe. Joyce Mkhoi (wa pili kulia), Hakimu Mkazi Mfawidhi Wa Wilaya kibaha Mhe. Emmael Lukumai (wa pili kushoto), Mtendaji Mahakama Ya Hakimu Mkazi Kibaha Pwani Bw. Moses Minga (wa kwanza kushoto) na Kaimu Mkuu mwendesha Mshitaka kutoka Ofisi ya Taifa ya Mashtaka Mkoa Wa Pwani Bi. Aurelia Makundi (wa kwanza kulia).
Mgeni Rasmi Katibu Tawala Wa Wilaya Kibaha Mhe. Moses Magogwa akipata Maelezo Katika Banda La Jeshi La Polisi
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni