Jumamosi, 27 Januari 2024

WIKI YA SHERIA YAZINDULIWA RASMI; WANANCHI WAALIKWA KUPATA ELIMU YA SHERIA

Na Amani Mtinangi-Mahakama Kuu Tabora

Matembezi ya uzinduzi wa Wiki ya Sheria kwa upande wa Kanda ya Tabora yameongozwa na Mkuu wa Wilaya ya Sikonge, Mhe. Simon Chacha ambaye amemwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Tabora.

Akizungumza katika ufunguzi wa Maadhimisho ya Wiki ya Sheria Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Tabora, Mhe. Dkt. Adam Mambi ameeleza jinsi Mahakama ilivyojipanga kufikisha elimu kwa umma kuhusu masuala ya kisheria na haki, na kuwaalika wananchi wa Mkoa huo kushiriki katika Maonesho ya Wiki ya Sheria ili kila wenye uwezo kufika kwenye maonesho wafike ili waelimishwe, watoe maoni na waitumie Mahakama kama chombo huru cha maamuzi ya migogoro yao.

“Mahakama imejipanga kufikisha elimu kwa umma na zoezi hili kimsingi limeshaanza hivyo kila mwenye uwezo asogee katika viwanja hivi ili aweze kuelekezwa, kufunzwa na kuelimishwa kuhusu huduma na milango ipo wazi kwa maoni, malalamiko, pongezi na mapendekezo.” amesisitiza Jaji Mambi.

Naye Mgeni Rasmi, Mkuu wa Wilaya ya Sikonge, Mhe. Chacha ameipongeza Mahakama kwa maboresho makubwa inayoyafanya kumlenga mwananchi ili kuhakikisha haki inapatikana kwa wakati na hivyo kuchochea uwepo wa utulivu wa kisiasa, maendeleo na ustawi wa Taifa.

“Naipogeza Mahakama ya Tanzania kwa maboresho makubwa inayoyafanya kwani maendeleo na ustawi wa Taifa yanategemea uwepo wa amani, usalama na utulivu wa kisiasa. Katika kuhakikisha nchi inaendelea kuwa na amani, usalama na utulivu wa kisiasa, maboresho ya kimkakati katika tasnia ya utoaji haki yanatakiwa kuwa jumuishi katika kuboresha Sheria, Kanuni na Sera kwenye Sekta ya Sheria na mfumo wa makosa ya jinai nchini kwa ujumla wake kama inavyofanya Mahakama. Maboresho haya yanalenga kuhakikisha kwamba, mwananchi anapata huduma stahiki.” Alisema Mhe. Chacha.

Wakati huohuo washiriki wa Maonesho wameishukuru Mahakama ya Tanzania kwa kufanya tukio kubwa la ufunguzi Maadhimisho ya Wiki ya Sheria kuahidi kushirikiana katika kuwahudumia wananchi watakaofika katika maonesho hayo.

“Mahakama ya Tabora haijawahi kutuangusha kuhusu maandalizi ya Wiki ya Sheria. Sisi tunaishukuru sana kwani inatukutanisha kumhudumia mwananchi, tunaomba utaratibu huu uendelee kwani tupo tayari kumhudumia kila mwananchi atakayefika,” amesema mmoja wa Wadau wa Mahakama.

Mwakilishi wa Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Mhe. Simon Chacha (wa tatu kulia) akiwa tayari kuongoza matembezi ya ufunguzi wa Wiki ya Sheria Nchini, wa pili kushoto ni Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Tabora, Mhe. Dkt.Adam Mambi, wa pili kulia ni Jaji Mahakama Kuu Kanda ya Tabora, Mhe. Dkt. Zainab Mango na kulia kwa Jaji Mfawidhi ni Jaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Tabora, Mhe. Mhe. Mwajuma Kadilu. Majaji wa Mahakama Kuu Tabora Wengine ni Viongozi wa Mahakama na wakuu wa Taasisi mbalimbali za Mkoa wa Tabora, wadau na wananchi wakiwa tayari kuanza walioshiriki katika matembezi yaliyofanyika leo tarehe 27 Januari, 2024.
Naibu Msajili wa Mahakama Kuu Kanda ya Tabora, Mhe. Pamela Mazengo (kushoto) na  Kanda ya Tabora, Bw. Emmanuel Munda wakiwa wamebeba bango la maandamano wakati wa matembezi ya uzinduzi rasmi wa Wiki ya Sheria leo tarehe 27 Januari, 2024. Nyuma yao ni Umma ulioshiriki katika matembezi hayo.
Watumimishi wa Mahakama wakifuatilia kwa karibu hotuba za viongozi wakati wa ufunguzi wa maadhimisho ya Wiki ya Sheria nchini.
Mkuu wa Wilaya ya Sikonge, Mhe. Simon Chacha wa pili kushoto akikata utepe kuashiria ufunguzi rasmi wa Maadhimisho ya Wiki na ya Sheria mkoani Tabora.

Mhe. Chacha (kushoto kwa Jaji Mfawidhi) akisikiliza maelezo ya jinsi huduma mbalimbali zinavyotolewa kidijitali katika banda la Mahakama.

Mahakama ya Hakimu Mkazi Simiyu nayo haikuwa nyuma katika shamrashamra za uzinduzi wa Wiki ya Sheria ambapo Mwandishi wetu Naumi Shekilindi kutoka Mkoa huo anaripoti kuwaWatumishi wa Mahakama Mkoa wa Simiyu wameadhimisha matembezi ya Wiki ya Sheria nchini leo tarehe 27 Januari, 2024.

Matembezi hayo yameongozwa na Mgeni Rasmi, Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Dkt. Yahaya Nawanda kutoka katika viwanja vya Mahakama ya Hakimu Mkazi Simiyu kuelekea katika viwanja vya stendi ya zamani ambapo ufunguzi ulifanyika. 

Katika matembezi hayo Mgeni Rasmi aliambatana na Mkuu wa Wilaya ya Bariadi, Mhe. Simon Simalenga, Kaimu Hakimu Mkazi Mfawidhi Mahakama ya Hakimu Mkazi Simiyu, Mhe. Caroline Kiliwa, Mtendaji Mahakama ya Hakimu Mkazi Simiyu, Bw. Gasto Kanyairita, watumishi wa Mahakama na wadau wa Mahakama kutoka katika Taasisi mbalimbali Mkoani humo.

Akizungumza wakati wa ufunguzi rasmi wa Wiki ya Sheria Mgeni Rasmi, Mhe. Dkt. Nawanda ameshukuru kufuatia hatua ya ujenzi wa Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki katika Mkoa huo.

"Kwa mara ya kwanza Mkoa wa Simiyu tunaenda kuwa na Mahakama Kuu na hatimaye wananchi hawataenda tena Shinyanga kwani huduma zote zitakuwa zinapatikana hapa, Kituo hiki ni rafiki kwa wananchi kwani unapata huduma zote  katika jengo moja yaani kuanzia Mahakama ya Mwanzo mpaka Mahakama Kuu, hii ni fahari kwa sisi wananchi wa Mkoa wa Simiyu," amesema Mhe. Nawanda.

Amewakumbusha Mahakimu juu ya utoaji haki kwa wananchi, ambapo amesema "Mahakimu mnatakiwa kutenda haki kwa wananchi  na sio kubatilisha haki, ni jukumu la kila Hakimu kuhakikisha mteja anapata haki yake na isiwe badala yake batili iwe haki na haki iwe batili.”

Mkuu wa Mkoa huo ametembelea mabanda ya Mahakama na ya wadau waliokuwepo katika ufunguzi huo na kuwapongeza kwa kazi kubwa wanayoifanya kwa wananchi wa Mkoa wa Simiyu.

Mwisho Mgeni Rasmi amewashukuru Viongozi wa Mahakama kwa kutambua umuhimu wake kuja kujumuika na watumishi wa Mahakama pamoja  na wadau katika kuadhimisha uzinduzi wa Wiki ya Sheria nchini na kusisitiza kuendeleza  uhusiano mzuri baina ya Mahakama na wadau katika utoaji haki kwa wananchi. 

Mgeni Rasmi, Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Dkt. Yahaya Nawanda akisaini kitabu cha wageni mara baada ya kuwasili katika viwanja vya Mahakama ya Hakimu Mkazi Simiyu kwa ajili ya kuongoza matembezi na kuzindua rasmi Wiki ya Sheria leo tarehe 27 Januari, 2024.

Watumishi wa Mahakama Simiyu wakiwa katika picha ya pamoja tayari kwa kuanza matembezi kuelekea viwanja vya stendi ya zamani mkoani Simiyu.

Watumishi wa Mahakama-Simiyu na wadau wakiwa katika matembezi kuelekea katika viwanja vya stendi ya zamani ambapo ufunguzi umefanyika.

Mgeni Rasmi mwenye koti jeusi akiongoza matembezi wakati wa kuadhimisha uzinduzi wa Wiki ya Sheria nchini mkoani Simiyu.

Mgeni Rasmi ambaye ni Mkuu wa Mkoa wa Simiyu,  Mhe. Dkt. Yahaya Nawanda akihutubia wananchi na wadau wa Mahakama katika viwanja vya stendi ya zamani Mkoani Simiyu.

Mwanza nao hawakuwa nyuma, Mwandishi wetu Stephen Kapiga anaripoti kuwa Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu ya Tanzania kanda ya Mwanza, Mhe. Dkt. Ntemi Kilekamajenga amewaongoza watumishi na Wadau mbalimbali katika matembezi ya Pamoja katika siku ya uzinduzi wa wiki ya sheria katika Mkoa wa Mwanza matembezi yalioanzia katika Mahakama ya wilaya Nyamagana na kupokelewa na Mkuu wa Wilaya Ilemela, Mhe. Hassan Masala katika viwanja vya Furahisha.

Licha ya uwepo wa mvua zinazoendelea kunyesha jijini humo haikuwazuia watumishi, Wadau na Wananchi wa maeneo ya karibu kuweza kushiriki matembezi hayo ambayo yalikuwa na umbali wa takribani kilomita tano kwa lengo la kuonesha kuunga mkono uzinduzi huo uliofanyika katika viwanja vya Furahisha ambapo elimu mbalimbali za kisheria zinaendelea kutolewa.

Mara baada ya kuwasili katika viwanja hivyo, Mhe. Dkt. Kilekamajenga, Majaji wengine, watumishi na wadau wengine walifanya mazoezi mafupi ya mwili kwa ajili ya kuweka mwili sawa baada ya matembezi hayo.

Akihutubia katika ufunguzi huo, Mhe. Dkt. Kilekamajenga ameelezea juu ya uboreshaji wa Mifumo jumuishi iliyofanywa na Mahakama ya Tanzania katika utoaji haki kwa wananchi ikiwemo uwepo wa akili bandia ambayo inasaidia kufanya unukuzi na utafsiri wa kile alichoongea mdaawa mahakamani.

“Mahakama katika utendaji kazi wake, hushirikiana na Taasisi au wadau mbalimbali katika utoaji haki na hivyo ili ushirikiano na wadau hawa uweze kuwa wenye tija, ni lazima uboreshwaji wa mifumo ya kitehama itakayowezesha ushirikishwaji na muingiliano wenye tija kurahisisha utendaji kazi pamoja na upatikanaji wa haki jinai nchini," amesema. 

Ameongeza kuwa, katika karne hii ambayo dunia iko kwenye mapinduzi ya teknolojia, Mahakama pamoja na wadau wake hawapaswi kubaki nyuma ili kufanya Mhimili huo kuwa wa kisasa, ”amesema Dkt. Kilekamajenga

Akitoa hotuba yake, Mkuu wa Wilaya Ilemela, Mhe. Hassan Masala ameipongeza Mahakama ya Tanzania kwa mapinduzi makubwa ya ki-TEHAMA inayofanya na hivyo kuweza kwenda na kasi ya ulimwengu wa kidijitali unaotawala sasa katika mapinduzi ya nane ya viwanda na hivyo kuzishauri Taasisi zingine katika mfumo mzima wa haki jinai kuweza kujifunza kutokana maendeleo ya TEHAMA yanayofanywa na Mahakama ya Tanzania.

“Ni rai yangu kwa Mahakama kutumia vyema miundombinu wezeshi kwani imegharimu Serikali fedha nyingi sana, miundombinu hiyo itumike kwa malengo yaliyokusudiwa ili kuhakikisha haki inatendeka na pia wadau waendelee kuhakikisha wanatimiza wajibu wao katika kusimamia haki jinai. Kwa mfano,  Polisi na TAKUKURU kujikita zaidi katika kuzuia utendekaji wa makosa na mamlaka za ukamataji kufanya hivyo kwa kuzingatia sheria, kufanyika upelelezi wa kina kwa wakati pamoja na waendesha mashtaka," amesema. 

Ameongeza kuwa, jamii iwe na utayari wa kutoa taarifa za  makosa ya jinai pamoja na kutoa ushahidi mahakamani. Kwa kufanya hivyo, wadau wa haki jinai wataendelea kuchangia katika kuboresha mfumo wa utoaji haki jinai,”amesema Mhe. Masala.

Aidha, wakati wa kutembelea mabanda yaliyopo katika viwanja hivo Mkuu wa wilaya ya Ilemela alioneshwa kwa vitendo mifumo ya uendeshaji na uratibu wa mashauri Mahakamani (e-CMS) jinsi unavofanya kazi kuanzia hatua ya mdau kutuma shauri lake mahakamani, jinsi linavyopokelewa na hatimaye kupangiwa kwa Jaji.

Si hayo tu, bali ameoneshwa mfumo wa Unukuzi na Kutafsiri wa mienendo wa mashauri mahakamani kutoka mfumo wa sauti na kubadilishwa kwenda kwenye maandishi kwa kutumia mfumo wa TTS.



Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu Kanda ya Mwanza, Mhe. Dkt. Ntemi Kilekamajenga akiwaongoza watumishi wa Mahakama ya Tanzania Kanda ya Mwanza pamoja na wadau wengine wa Mahakama katika matembezi ya uzinduzi wa Wiki ya Sheria mkoani Mwanza. matembezi hayo yalianzia katika viwanja vya Mahakama ya Wilaya Nyamagana na kumalizikia katika viwanja vya Furahisha.


Mkuu wa Wilaya ya Ilemela Mhe Hassan Masala akiwaongoza Majaji wa Mahakama kuu ya Tanzania Kanda ya Mwanza pamoja na Viongozi wengine wa Haki Jinai Mkoa wa Mwanza kuelekea jukwaa kuu tayari kwa uzinduzi wa Wiki ya Sheria katika Mkoa wa Mwanza. Maadhimisho yanayoendelea katika viwanja vya Furahisha.

Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Mwanza, Mhe. Dkt. Ntemi Kilekamajenga (wa pili kushoto )akiwa pamoja na Mkuu wa Wilaya Ilemela (kulia) katika jukwaa kuu wakati wa uzinduzi wa wiki ya sheria Mkoani Mwanza.

(HABARI HIZI ZIMEHARIRIWA NA MARY GWERA, MAHAKAMA-DODOMA)

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni