Jumapili, 28 Januari 2024

MATEMBEZI UZINDUZI WIKI YA SHERIA YATIA FORA ARUSHA

Na Seth Kazimoto - Mahakama Kuu Arusha

Mahakama Kuu Kanda ya Arusha imezindua rasmi Wiki ya Sheria nchini kwa kufanya matembezi maalum yaliyoongozwa na Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mhe.  John Mongela.

Matembezi hayo yalianzia Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki (IJC) Arusha hadi viwanja vya TBA mkoani humo.

Jaji Mfawidhi wa Kanda hiyo, Mhe. Joachim Tiganga amewashukuru wananchi na wadau kwa kujitokeza kwa wingi katika uzinduzi wa Wiki ya Sheria Tanzania. Amewahimiza wananchi mkoani humo kuendelea kutembelea maonesho ya Wiki ya Sheria ili waelewe haki zao na namna ya kuzipata.

Wakati huohuo, Mgeni Rasmi wa uzinduzi wa Wiki ya Sheria, Mhe. Mongela ameshukuru Uongozi wa Mahakama wa Kanda hiyo kwa kuandaa maonesho hayo ambapo amekiri kuwa ameona muamko mkubwa wa wananchi katika kufuatilia elimu ya sheria inayoendelea kutolewa kwa njia mbalimbali ikiwemo Redio zilizopo mkoani humo.

Mkuu wa Mkoa ameipongeza pia Mahakama katika maeneo manne ambayo ni kuimarika na kuboreshwa kwa miundombinu na mifumo ya utoaji Haki, Usikilizaji mashauri kwa kiasi kikubwa na kuisha kwa wakati, Matumizi ya Usuluhishi katika kutatua migogoro inayoletwa mahakamani na kutokuwepo kwa ucheleweshaji wa nakala za hukumu.

Pia amesema kuwa anafurahia kuona uwepo wa ushirikiano mzuri wa Mahakama na Wadau wake katika kuhakikisha kazi za Mahakama hazikwami na hatimaye wananchi kupata huduma za kimahakama kwa wakati na bila vikwazo. Mhe. Mongela ametembelea mabanda ya maonesho ya sheria yaliyopo katika viwanja vya TBA.

Aidha, katika zoezi la utoaji elimu ya sheria linaloendelea mkoani Arusha Mhe. Tiganga amefungua mafunzo maalum kwa Viongozi wa Serikali za Mitaa katika Halmashauri za Wilaya Arusha na Jiji Arusha ambapo Maafisa Watendaji wa Kata, Vijiji na Mitaa wamepewa mafunzo maalum ya sheria yatakayowasaidia katika kazi zao za kila siku. 

Mhe. Tiganga amesema kuwa, Viongozi wa Serikali za Mitaa ndio ngazi ya kwanza ya kuhudumia wananchi na migogoro mingi ya wananchi hushughulikiwa katika ngazi hizo, hususani Mabaraza ya Kata ya Ardhi na yale ya usuluhishi wa ndoa. 

“Viongozi hawa ndio walinzi wa amani na usalama katika maeneo wanayosimamia, kwa msingi huo, tumeona ni muhimu tuandae mafunzo maalum ya sheria kwa Viongozi hawa ili kuwaongezea ujuzi na uwezo wa kufanya kazi zao kwa ufanisi” alisisitiza Mhe. Tiganga.

Katika uzinduzi huu wa Wiki ya Sheria Tanzania, watu mbalimbali wameshiriki wakiwemo Jaji na Rais wa Mahakama ya Afrika ya Haki za Watu na Binadamu, Mhe. Imani Aboud na Jaji Mstaafu wa Mahakama ya Rufani Tanzania (T), Mhe. Januari Msoffe. 

Jaji na Rais wa Mahakama ya Afrika ya Haki za Watu na Binadamu, Mhe. Imani Aboud ( kushoto), Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu Kanda ya Arusha, Mhe Joachim Tiganga (kulia) pamoja na Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mhe John Mongela (katikati) kwa pamoja wakiwa wameshika bango la Mahakama wakati wa matembezi ya uzinduzi wa Wiki ya Sheria tarehe 27 Januari, 2024.

Washiriki wa Matembezi ya uzinduzi wa Wiki ya Sheria nchini wakishiriki kikamilifu na kwa ukakamavu. Mwenye mavazi ya kijivu upande wa kulia kabisa ni Jaji Mstaafu wa Mahakama ya Rufani, Mhe. Januari Msoffe.

Wananchi na Wadau mbalimbali walioshiriki uzinduzi wa Wiki ya Sheria Tanzania uliofanyika tarehe 27 Januari, 2024 katika viwanja vya TBA mkoani Arusha.

Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Arusha, Mhe. Joachim Tiganga (katikati),  Jaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Arusha Mhe. Dkt. Dafina Ndumbaro (wa tatu kulia), Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Arusha, Mhe. Suleiman Msumi (wa tatu kushoto), Naibu Msajili wa Mahakama Kuu Kanda ya Arusha, Mhe. Fredrick Lukuna (wa pili kushoto),  Naibu Msajili Mahakama Kuu Kanda ya Arusha, Mhe. Mariam Mchomba (wa pili kulia), Hakimu Mkazi Mfawidhi Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha, Mhe. Erasto Philly  (wa kwanza kulia) na Hakimu Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya Arumeru, Mhe. Theresia Sedoyeka (wa kwanza kushoto) wakiwa katika picha ya pamoja muda mfupi kabla ya kuanza mafunzo ya sheria kwa Maafisa Watendaji wa Kata na Vijiji wa Wilaya hiyo yaliyofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Halmashauri ya Wilaya Arusha.

Naibu Msajili wa Mahakama Kuu Kanda ya Arusha, Mhe. Fredrick Lukuna akifafanua jambo wakati wa mafunzo ya sheria kwa Maafisa Watendaji wa Kata na Vijiji wa Halmashauri ya Wilaya ya Arusha.
Maafisa Watendaji wa Kata na Vijiji katika Halmashauri ya Wilaya Arusha wakipatiwa mafunzo ya Sheria yaliyotolewa wakati wa Wiki ya Sheria inayoendelea nchini.


(Habari hii imehaririwa na MARY GWERA, Mahakama-Dodoma)

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni