Jumapili, 28 Januari 2024

MWANASHERIA MKUU AFURAHISHWA NA UWEPO WA WADAU HAKI JINAI WIKI YA SHERIA DODOMA

Na Mary Gwera, Mahakama-Dodoma

Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Mhe. Dkt. Eliezer Mbuki Feleshi amefurahishwa na uwepo wa banda la Wadau wa Haki Jinai katika Maonesho ya Wiki ya Sheria yanayoendelea Kitaifa katika Viwanja vya Nyerere ‘Square’ jijini Dodoma.

Mhe. Dkt. Feleshi ameeleza kufurahishwa leo tarehe 28 Januari, 2024 mara baada ya kutembelea mabanda mbalimbali ya Mahakama yaliyopo katika maonesho yanayoendelea kufanyika katika viwanja hivyo.

“Mimi kama Mjumbe ya Kamati ya Maaboresho ya Mfumo wa haki jinai nakiri kufurahishwa na uwepo wa banda ya Wadau wa Haki jinai ambao wote wanatoa maelezo ya namna taratibu zinatakiwa kuwa, na ni kwa jinsi gani utekelezaji wa mapendekezo ya mfumo wa haki jinai unavyofanyika,” amesema Mwanasheria Mkuu.

Amesema pia kuwa, anaona mafanikio makubwa katika Wiki ya Sheria kwakuwa kumekuwa na muitikio wa Wadau katika kutoa elimu, na kuwataka wananchi kujitokeza kupata elimu ya sheria na kutoa malalamiko yao.

“Kwanza napenda kuishukuru Mahakama kutualika sisi kama moja na Wadau wake kushiriki katika maonesho haya, napenda pia kukiri kuwa mwitikio wa Wadau katika maonesho haya umeongezeka, hivyo nitoe rai kwa wananchi wenye malalamiko kujitokeza,” ameeleza Mwanasheria Mkuu.

Kadhalika, Mhe. Dkt. Feleshi ameipongeza Mahakama kwa kuzindua Mfumo wa Unukuzi na Kutafsiri (TTS) huku akisema kwamba, Mfumo huo utawasaidia kuwapunguzia kazi ya kuandika Majaji na Mahakimu kwakuwa huchukua muda mwingi kuandika ushahidi na kadhalika.

Akizungumzia kuhusu malalamiko mbalimbali ya wananchi kuhusu Sheria, Mwanasheria Mkuu amesema Serikali inaangalia uwezekano wa kuanzisha Kituo cha kudumu cha kushughulikia kero za wananchi.

“Pamoja na maadhimisho ya Wiki ya Sheria yanayofanywa na Mahakama kila mwaka, Serikali imejitahidi kutumia njia tofautitofauti za kuwafikia wananchi katika kuelimisha na kushughulikia masuala mbalimbali ya kisheria ikiwemo njia za TEHAMA kupitia Tovuti, Mama Samia ‘Legal Aid’, vipindi vya TV na redio lakini bado kuna malalamiko, hivyo ni muhimu kuwa na Kituo cha kudumu ambacho kitakuwa kikitoa huduma wakati wote,” amesema Mhe. Dkt. Feleshi.

Maonesho ya Wiki ya Sheria yanaendelea hadi tarehe 30 Januari, 2024 na kilele cha Siku ya Sheria itakuwa tarehe 01 Februari, 2024 ambapo Kitaifa itafanyika katika Viwanja vya Chinangali jijini Dodoma na Mgeni Rasmi anatarajiwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Mhe. Dkt. Eliezer Mbuki Feleshi (kulia) akizungumza na Wadau wa Haki Jinai alipotembelea banda hilo leo alipotembelea Maonesho ya Wiki ya Sheria leo tarehe 28 Januari, 2024 yanaoendelea katika Viwanja vya Nyerere 'Square' jijini Dodoma na nchi nzima. 

Mwanasheria Mkuu, Mhe. Dkt. Eliezer Mbuki Feleshi akisaini kitabu cha wageni alipowasili katika viwanja vya Nyerere 'Square' leo tarehe 28 Januari, 2024 kutembelea mabanda yaliyopo katika Maonesho ya Wiki ya Sheria.

Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Mhe. Dkt. Eliezer Mbuki Feleshi akipata maelezo kutoka Maafisa kutoka Wizara ya Katiba na Sheria leo alipotembelea Maonesho ya Wiki ya Sheria yanayoendelea katika Viwanja vya Nyerere 'Square' jijini Dodoma.

Mwanasheria Mkuu akipata maelezo kutoka Wadau mbalimbali wa Mahakama wanaoshiriki katika Maonesho ya Wiki ya Sheria yanayoendelea katika Viwanja vya Nyerere 'Square' jijini Dodoma.

Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Mhe. Dkt. Eliezer Mbuki Feleshi (kushoto) akiwa pamoja na Maafisa wa Mahakama alipowasili katika kwenye Maonesho ya Wiki ya Sheria yanayofanyika kwenye Viwanja vya Nyerere 'Square' jijini Dodoma. Kulia ni Mtendaji Mahakama Kuu ya Tanzania, Bw. Leonard Magacha.

(Picha na Faustine Kapama-Mahakama)





Hakuna maoni:

Chapisha Maoni