Jumatatu, 29 Januari 2024

TIMU YA MAHAKAMA TABORA YAIZABUA CHUO CHA UTUMISHI WA UMMA

Na Amani Mtinangi, Mahakama Kuu Tabora

Mtoto akililia wembe muache auchezee, ukimkata atajifunza. Kazi ya Mahakama ni kuwafunga na ndicho walichofanya kwenye uwanja wa Shule ya Wavulana Tabora ambapo timu ya mpira wa pete ya Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Tabora ilipocheza mechi yake na timu ya Chuo cha Utumishi wa Umma ambapo Mahakama iliwacharaza wanachuo hao bao 17 kwa tano. 

Kipute hicho kilipigwa mkoani Tabora jana tarehe 28 Januari, 2024. Katika mchezo huo Timu ya Mahakama ilikutana na timu ngumu ya Chuo cha Utumishi wa Umma na kuipiga kipigo cha mbwa koko na kuiacha ikiwa hoi bin taaban huku wachezaji na mashabiki wake wakishikwa na bumbuwazi wasiamini kilichotokea. 

Hapo ndipo ilipojidhihirisha ile kauli ya wahenga kuwa mchelea mwana kulia, hulia mwenyewe. Laiti wangejua wasingeingiza timu uwanjani, wenye hekima husema bora lawama kuliko fedheha. Ilikuwa ni timu ya Mahakama iliyotia tena goli lingine la timu hiyo lililowatoa kidedea na kulinda heshima ya Mhimili huo.

Katika mchezo mwingine timu ya mpira wa miguu ya Mahakama Kuu Tabora imefungwa kwa mbinde penati na timu ya Uhuru Veteran. Hadi kufikia mapumziko matokeo yalikuwa tatu bila timu ya Mahakama ikiongoza mtanange huo uliokuwa mkali na wa kuvutia huku timu ya Mahakama ikionesha ufundi na ujuzi wake tangu dakika ya kwanza ya mchezo. 

Kipindi cha pili kilianza kwa kasi huku timu ya Mahakama ikilisakama lango la Maveterani, katika kipindi hicho, Maveterani walijikongoja na kwa mbinde sana wachezaji wao walifanikiwa kufunga magoli yasiyo na mvuto na kusawazisha. 

Baada ya kusawazisha, Timu ya Mahakama iligeuka nyuki. Safari hii haikuwa na kazi ya kutengeneza asali bali kushambulia lango la wapinzani wao kwa miba ya sumu na kuwatoa kabisa relini timu ya Uhuru lakini haikufanikiwa kupata goli. 

Akizungumza baada ya mchezo huo kumalizika, Kocha wa timu hiyo, Bw. Ngongo Ngongo amesema kuwa hizi ni rasharasha mvua itamnyeshea kila atakayeiomba.

“Nikuhakikishie hizi ni rasharasha tu japo bahati haikuwa yetu, lakini kazi yetu wameiona na kuanzia sasa anayeitaka mvua, itakuja na mavuno yake. Hebu fikiria hii ilikuwa ni mechi ya kirafiki tumewafanya hivi yangekua mashindano je?” alisema Bw. Ngongo.

Nao mashabiki waliofika uwanjani walitanabaisha kuwa timu ya Mahakama inatisha na wakaomba Mahakama ya Tanzania ianzishe timu itakayoshiriki michuano mbalimbali ikiwemo Ligi Kuu ya Tanzania.

“Kiwango timu ya Mahakama ni kizuri mno. Mimi nafikiria mfikirie kuwa na timu itakayokuwa inacheza kwenye michezo mbalimbali hata ligi kuu ikiwezekana” alisema shabiki huyo wa mpira.

Michezo hiyo ni sehemu ya maadhimisho ya Wiki ya Sheria na utekelezaji wa nguzo ya tatu ya Mpango Mkakati wa Mahakama ya kuboresha ushirikiano na wadau.

Jaji mfawidhi Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Tabora, Mhe. Dkt. Adam Mambi akikabidhi kombe kwa Timu ya netiboli ya Mahakama Kuu Tabora baada ya kuwapiga kama ngoma timu ya Utumishi wa Umma katika Bonanza la Michezo lililofanyika jana tarehe 28 Januari, 2024.

Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu Kanda ya Tabora, Mhe. Dkt. Adam Mambi akizungumza mara baada ya mchezo kati ya Timu ya Kanda hiyo na ya Chuo cha Utumishi wa Umma uliofanyika jana tarehe 28 Januari, 2024 ikiwa ni sehemu maadhimisho ya Wiki ya Sheria.
 Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu Kanda ya Tabora, Mhe. Dkt. Adam Mambi (katikati), Jaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Tabora, Mhe. Dkt. Zainab Mango (kushoto) na wengine wakiwa tayari kwa michezo ya Bonanza iliyofanyika tarehe 28 Januari, 2024 ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya Wiki ya Sheria.


(Habari hii imehaririwa na Mary Gwera Mahakama-Dodoma)


Hakuna maoni:

Chapisha Maoni