Ijumaa, 26 Januari 2024

MAHAKAMA MOROGORO YAPANDISHA KAULI MBIU YA WIKI YA SHERIA KILELENI MLIMA BONDWA

 

Na Evelina Odemba – Mahakama, Morogoro

 

Watumishi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Morogoro, kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wa Mahakama mkoani hapa katika kuelekea uzinduzi rasmi wa Wiki ya Sheria, wamefanikiwa kupandisha kauli mbiu ya maadhimisho hayo katika kilele cha Mlima Bondwa kwenye safu za Milima ya Uluguru.

 

Msafara wa kupandisha kauli mbiu hiyo uliokuwa na watu zaidi ya 120 uliongozwa na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Morogoro, Mhe. Latifa Mansoor, ambapo watu 70 kati yao walifanikiwa kufika katika kilele hicho chenye mwinuko wa mita 2161 toka usawa wa bahari.

 

Akizungumza mara baada ya kufika katika Kilele hicho, Mhe Mansoor amesema kuwa lengo la kupelekea kauli mbiu hiyo ni kutoa wito kwa wananchi kushiriki kikamilifu  katika maadhimisho hayo na kupata elimu ya masuala mbalimbali ya kisheria.

 

“Niwapongeze wale wote waliofanikisha kupandisha kauli mbiu hii hadi hapa kwenye kilele cha Mlima Bondwa, hakika halikuwa jambo jepesi ni uzalendo mkubwa mmeuonesha na pia tumeutangaza utalii,” alieleza Jaji Mfawidhi.

 

Miongoni mwa walioshiriki kupandisha kauli mbiu hiyo, mbali na watumishi wa Mahakama, ni wadau toka Bondwa Hiking Club, Chama Cha Mawakili wa Kujitegemea (TLS) na wanafunzi wa vyuo mbalimbali wa fani ya sheria, ikiwemo Chuo Kikuu Jordani na Mzumbe na MUM. 

 

Baadhi ya washiriki wa zoezi hilo wameipongeza Mahakama Kuu Kanda ya Morogoro kwa kuja na wazo hilo la kupanda Mlima Bondwa, jambo lililowawezsha pia kufanya utalii wa ikolojia

 

Naye Muongozaji Watalii katika Mlima huo kutoka Wakala wa Huduma za Misitu (TFS) na Hifadhi ya Mazingira Asilia Uluguru, Bw. Edson Jackson, alisema Mhe. Mansoor ameweka historia kwa kuwa Jaji wa kwanza wa Mahakama ya Tanzania kupanda katika Mlima huo hadi kileleni, umbali wa zaidi ya kilomita 17 toka liliko Jengo la Mahakama Kuu.

 

Maadhimisho ya Wiki ya Sheria kwa Mahakama Kanda ya Morogoro yatazinduliwa rasmi Januari 27, 2024 na Mkuu wa Mkoa, Mhe. Adam Malima ambapo ataongoza matembezi ya kilometa nne kutoka katika jengo la Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki, ‘IJC’, hadi katika kituo cha daladala cha zamani mkoani huo.

 

Wakati huo huo, zoezi la utoaji elimu ya sheria linaendelea katika viwanja hivyo na wadau zaidi ya 34 wameungana na Mahakama kushiriki katika maadhimisho hayo.

 

Kauli mbiu ya Wiki na Siku ya Sheria mwaka 2024 ni “Umuhimu wa dhana ya Haki kwa ustawi wa Taifa: Nafasi ya Mahakama na Wadau katika kuboresha mfumo jumuishi wa Haki Jinai.”



Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Morogoro, Mhe. Latifa Mansoor (aliyevaa koti jeusi) akizungumza na wadau na watumishi wa Mahakama muda mfupi kabla ya safari ya kupanda kilele cha Mlima Bondwa haijaanza.

 

Kauli Mbiu ya Wiki ya sheria kwa mwaka 2024 tayari ikiwa juu ya kilele cha Mlima Bondwa.


 

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Morogoro, Mhe. Latifa Mansoor (aliyevaa koti jeusi) akiwa katika picha ya pamoja na wadau na watumishi wa Mahakama baada ya kuwasili kwenye kilele cha Mlima Bondwa.


 

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Morogoro, Mhe. Latifa Mansoor (aliyetangulia mbele) akiwa katika jitihada za kukitafuta kilele cha Mlima Bondwa ili kuifikisha kauli mbiu ya Wiki ya Sheria 2024.


 

Mapumziko kidogo katika safari ya kuupanda Mlima Bondwa.

 Mazoezi ya kuweka sawa mwili baada ya kufika katika kilele cha Mlima Bondwa.

 


Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Morogoro, Mhe. Latifa Mansoor (aliyevaa koti jeusi) akiwa pamoja na Viongozi wa Bondwa Hiking Club baada ya kuwasili katika kilele cha Mlima Bondwa.


 


Sehemu ya wadau wa Mahakama wakiwa katika zoezi la utoaji elimu kwenye mabanda yaliyoko kwenye eneo la stendi ya zamani ya daladala Morogoro Mjini wakati wa maadhimisho ya Wiki ya Sheria 2024.


 

Elimu ikiendelea kutolewa kwa wananchi.

(Habari hii imehaririwa na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Dodoma)

 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni