Na Amani Mtinangi-Mahakama Kuu, Tabora
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Tabora, Mhe. Adam Mambi juzi tarehe 24 Januari, 2024 aliongoza Majaji na Viongozi wengine kutoka Kanda hiyo kutembelea mabanda ya maonesho ya Wiki ya Sheria yanayofanyika katika Viwanja vya Chipukizi vilivyopo katika eneo la Chuo Kikuu Kishiriki AMUCTA mkoani hapa.
Majaji wengine wa Mahakama Kuu ya Tanzania kutoka Kanda hiyo waliokuwepo kutembelea mabanda hayo ni Mhe. Dkt. Zainab Mango na Mhe. Dkt. Mwajuma Kadilu.
Wakati akitembelea mabanda hayo, Mhe. Mambi amewashukuru na kuwapongeza wadau, Taasisi za Umma na zisizo za kiserikali, asasi za kiraia, Taasisi za kifedha na makampuni ya mawasiliano kwa maandalizi na kazi nzuri wanavyoendelea nayo ya kuhudumia na kutoa elimu kwa Umma kupitia maonesho hayo.
“Ninawashukuru sana wadau wote mliofika kwa ajili ya kushiriki maonesho ya Wiki ya Sheria katika Viwanja hivi vya Chipukizi, ni wazi kwa mwitikio huu mmejiandaa vyema na mnafanyakazi nzuri ya kuelimisha wananchi wanaofika katika maonesho haya. Rai yangu kubwa ni kuwaomba muendelee na kazi hii nzuri mnayoifanya,” alisema.
Kwa upande wao, wadau waliwaeleza Majaji kuhusu shughuli mbalimbali za Taasisi zao na kuwa wapo tayari kuendelea kuwahudhumia watu watakaofika kwenye maonesho hayo na kuwasihi wananchi kufika ili wajipatie elimu na huduma.
Kila mwaka, maadhimisho ya Wiki ya Sheria hufanyika katika Mahakama zote kuashiria mwanzo wa mwaka wa sheria nchini ambapo kaulimbiu ya mwaka huu inasema, “Umuhimu wa Dhana ya Haki kwa Ustawi wa Taifa: Nafasi ya Mahakama na Wadau katika Kuboresha Mfumo Jumuishi wa Haki Jinai.”
Viongozi wa Mahakama Kuu Kanda ya Tabora wakijadili jambo baada ya kumaliza ukaguzi wa mabanda ya maonesho. Pichani wa tatu kulia ni Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Tabora, Mhe. Dkt. Adam Mambi, kushoto kwake ni Jaji wa Mahakama Kuu, Dkt. Zainab Mango na wa kwanza kulia ni Jaji wa Mahakama Kuu, Mhe. Dkt. Mwajuma Kadilu. Wengine katika picha ni Naibu Msajili wa Mahakama Kuu Kanda ya Tabora, Mhe. Rhoda Ngimilanga na kushoto kwake ni Mtendaji wa Mahakama, Bw. Emmanuel Munda na wa kwanza kushoto ni Hakimu Mkazi Mahakama ya Hakimu Mkazi Tabora, Mhe. Gabriel Ngaeje.
(Habari hii imehaririwa na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Dodoma)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni