Alhamisi, 25 Januari 2024

MTENDAJI MKUU WA MAHAKAMA ATEMBELEA MABANDA WIKI YA SHERIA DODOMA

·Asisitiza mambo matatu kwa wananchi

Na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Dodoma

Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel leo tarehe 25 Januari, 2024 ametembelea mabanda ya maonesho ya Wiki ya Sheria yanayofanyika kitaifa katika Viwanja vya Nyerere Square jijini hapa na kuonyesha kuridhishwa na maandalizi yaliyofanyika.

Akizungumza na Waandishi wa Habari baada ya kutembelea mabanda hayo ambayo yameandaliwa na Mahakama na wadau, Prof. Ole Gabriel amewaomba wananchi kujitokeza kwa wingi ili kupata elimu kwenye masuala mbalimbali ya kisheria na haki kwa ujumla.

“Sisi kama Mahakama tumejiandaa kwa kiasi kikubwa na kwa kuzingatia mwongozo kutoka kwa Kiongozi wetu mkuu, Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma, tupo tayari kuwahudumia wananchi na kuwaonyesha hatua kubwa ambazo tumefikia katika suala zima la utoaji haki nchini,” amesema.

Mtendaji Mkuu wa Mahakama alitumia nafasi hiyo kuwafahamisha wananchi kuwa Mahakama ya Tanzania inazidi kupiga hatua kwenye masuala ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA), lengo ni kupeleka huduma za haki kwa haraka kadri inavyowezekana.

“Kama mnavyofahamu, nia ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ni kuhakikisha wananchi wanapata huduma kwa haraka na kwa wakati,” amesema na kuipongeza Serikali kwa kuiwezesha Mahakama kupata miundombinu mbalimbali wezeshi.

Amewaomba wananchi kuwa tayari kifikra na kutambua kuwa Mahakama waliyoizoea wakati ule wa makaratasi siyo ya sasa ambapo mwananchi anaweza kufungua shauri popote alipo masaa 24 kwa kutumia simu janja.

Kadhalika, Mtendaji Mkuu wa Mahakama amewaomba wadau mbalimbali kutambua kuwa Mahakama haiwezi kufanya kazi peke yake, kwani wahenga walisema, “Ukitaka kwenda mbali, nenda na wenzako, ukitaka kwenda haraka, nenda peke yako.”

Akabainisha kuwa Mahakama ya Tanzania inataka kufika mbali, hivyo inatamani wadau wake waelewe kasi wanayokwenda nayo na wao wajitahidi kadri inavyowezekana kwenda nao sambamba, hususan katika masuala ya matumizi ya kidigiti ili wawe na kasi moja ya kumhudumia mwananchi kwa ufanisi mkubwa.

“Niwahakikishie kuwa Mahakama ipo tayari wakati wote kuendelea kushirikiana nao ili kuhakikisha haki inapatikana kwa wakati, kwa urahisi na kwa gharama nafuu zaidi,” amesema.

Prof. Ole Gabriel alitumia nafasi hiyo pia kuwashukuru waandaaji wa maonesho hayo ya Wiki ya Sheria, wakazi na Viongozi wa Mkoa wa Dodoma kwa ushirikiano walioutoa ili kufanikisha maadhimisho hayo.

Ufunguzi rasmi wa Wiki ya Sheria utakuwa tarehe 27 Januari, 2024 utakaofanyika kwa matembelezi maalum yatakayoanzia kwenye Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki Dodoma na kutamatishwa katika Viwanja vya Nyerere Square. 

Mgeni rasmi katika hafla ya ufunguzi wa maadhimisho hayo atakuwa Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Rais wa Umoja wa Mabunge Duniani, Mhe. Dkt. Tulia Ackson.

Wakati wa maonesho hayo, wadau mbalimbali watashirikiana na Mahakama katika zoezi la utoaji wa elimu na huduma mbalimbali za kimahakama, wakiwemo Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali, Ofisi ya Taifa ya Mashtaka, Ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali, Tume ya Haki za Binadamu, Chama cha Majaji na Mahakimu Wanawake (TAWJA), Polisi, Magereza na Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS).

Elimu itakayotolewa inahusu taratibu za ufunguaji wa mashauri hasa kwa njia ya mtandao, sheria na taratibu zinazotumika katika kuendesha mashauri mbalimbali kama yale ya Ndoa na Talaka, Ardhi, migogoro ya Kazi pamoja na utekelezaji wa hukumu, Sheria za Watoto na taratibu za mashauri ya mirathi.

Vilevile wanananchi watapata fursa ya kujifunza huduma zitolewazo na Mahakama inayotembea “Mobile Court” na Mahakama za Vituo Jumuishi, watajifunza jinsi Mahakama ya Tanzania imejipanga kutoa haki katika Karne ya 21 kwa kutumia matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA).

Maonesho hayo yanatarajiwa kuhitimishwa tarehe 30 Januari, 2024 kuelekea kilele cha Siku ya Sheria tarehe 1 Februari, 2024 ambapo mgeni rasmi atakuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan. 

Kauli mbiu ya Wiki na Siku ya Sheria kwa mwaka huu 2024 inasema, “"Umuhimu wa Dhana ya Haki kwa Ustawi wa Taifa: Nafasi ya Mahakama na Wadau katika Kuboresha Mfumo Jumuishi wa Haki Jinai."

Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel akisisitiza jambo alipokuwa anaongea na Waandishi wa Habari leo tarehe 25 Januari, 2024 baada ya kutembelea mabanda ya maonesho ya Wiki ya Sheria yanayofanyika kitaifa katika Viwanja vya Nyerere Square jijini Dodoma.


 Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel akisalimiana na wadau wa haki jinai alipotembelea banda lao kwenye maonesho hayo. Anayeonekana kwa nyuma ni Mtendaji wa Mahakama ya Rufani ya Tanzania, Bw. Victor Kategere.
 Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel akiteta jambo alipokuwa kwenye banda la Mahakama la huduma bora kwa mteja. Picha chini akitia saini kwenye kitabu cha wageni kwenye banda la Magereza.


 Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel akisalimiana na wadau kwenye banda la TANAPA (juu) na banda la Benki ya NMB (chini).



 Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel akiwa katika banda la Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto. Anayeonekana kwa nyuma ni Mtendaji wa Mahakama ya Rufani ya Tanzania, Bw. Victor Kategere.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni